watoto wa kaka yake mwanasiasa mkongwe Steven Wasira wakichukua kadi za chadema wiki iliyopita.
Tarehe 30/09/2012 mimi
Esther Wasira na dada yangu Lilian Wasira tulijiunga na CHADEMA na kukabidhiwa
kadi na Katibu Mkuu wa CHADEMA Mh. Dr Willibrod Slaa. Tulielezea kwa kirefu
sababu za sisi kujiunga CHADEMA na tukasisitiza kuwa tumeridhika kuwa CHADEMA
ni chama chenye dhamira safi ya kuiongoza Tanzania na kwamba ni chama kinacholeta
matumaini mapya ya kuijenga Tanzania
mpya yenye neema. Waandishi wa habari walijaribu sana kutudodosa kujua tuna uhusiano gani na
Waziri Steven Wasira. Tulielezea wazi kuwa mahusiano yetu ya kifamilia
hayahusiki na sababu na dhamira yetu ya kujiunga CHADEMA. Hata hivyo tulielezea
kuwa Waziri Steven Wasira ni baba yetu mdogo ambaye alinyang'anyana ziwa na
baba yetu mzazi, wakili George Wasira. Tulidhani hiyo ilitosha na lisingekuwa
swala tena la kujadili na badala yake hoja ya kujadiliwa ingeweza kuwa sababu
tulizozieleza za kujiunga CHADEMA. Tunasikitishwa sana
na malumbano yaliyofuata baada ya hapo kuhusu kama
sisi ni watoto wa Wasira au la. Kama
tulivyoeleza, tumejiunga CHADEMA kwa sababu tulizozieleza hapo awali na wala si
kwa sababu nyingine yeyote. Hatujajiunga CHADEMA kumdhalilisha mtu,
kumfedhehesha mtu au kukipatia umaarufu CHADEMA kwa vile tu tunatumia jina la
Wasira. CHADEMA ni chama cha siasa tena chenye wanachama na wafuasi wengi Tanzania hivyo
si kashfa bali ni fahari kubwa mtu kujiunga CHADEMA na tena ni ushahidi wa mtu
kujitambua. Pia CHADEMA ni Chama maarufu sana Tanzania kwa
sasa hata pengine ni maarufu kuliko CCM hivyo hakihitaji kujipatia umaarufu kwa
mgongo wetu. Sisi tunawaheshimu sana wazee wetu
na tutaendelea kuwaheshimu ila linapokuja swala la chama cha kujiunga linabaki
kuwa hiari yetu kwa kuzingatia sera za chama na uwezo wa chama husika katika
kujenga Tanzania tunayoitaka
na hilo ndilo
lililotupeleka CHADEMA. Na hii ni haki yetu ya msingi kabisa inayolindwa na
Katiba ya nchi hii chini ya ibara ya 20(1). Ikumbukwe kuwa mmoja wa Waanzilishi
wa CHADEMA ni Mzee Wasira. Dhamira ya kuanzisha CHADEMA ilikuwa ni kushika dola
na hili ndilo CHADEMA imekuwa siku zote inajaribu kuwashawishi Watanzania kuwa
sasa wamekomaa na wanastahili kuchukua dola. Kwa vile kuchukua dola ilikuwa
ndio ndoto ya baba yetu mzazi Mwanzilishi wa CHADEMA, sisi kama watoto
tumejiunga na M4C ya CHADEMA ili tuweze kutimiza ndoto ya baba yetu kuwa
CHADEMA siku moja ichukue jukumu la kuiongoza Tanzania.
Kwa maelezo zaidi
wasiliana na: Lilian Wasira 0719 604156 Esther Wasira 0655 048797
Kwa hisani ya Mjengwa blog.
No comments:
Post a Comment