Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Monduli,Mh.
Edward Lowassa ( Pichani juu wa pili kushoto) akijumuika pamoja na Baadhi ya
Wabunge wanaounda timu ya Bunge Sports inayoundwa na wabunge kutoka Baraza la
Wawakilishi na Bunge la Jamhuri,wakati wa Chakula cha Mchana alichowaandalia
Nyumbani kwake,Ngarashi Wilayani Monduli juzi.Wengine kwenye picha ya kwanza
juu kutoka kushoto ni Naibu Waziri wa Habari,Vijana Utamaduni na Michezo,Mh.
Amos Makalla,Mbunge wa Jimbo la Kinondoni,Mh. Iddi Azzan pamoja na Mwenyekiti
wa CCM, Wilaya ya Monduli, Reuben ole Kunai. ( Picha: Othman Michuzi)
Hapa namuona Halima Mdee mbunge wa kawe (chadema) na wabunge wengine wakila nyama......Huyu kama sio Prof majimarefu wa korogwe vijijini (CCM) basi macho yangu hayana shabaha... nae alikuwepo.
WAZIRI Mkuu mstaafu na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa
amewashauri wabunge wa timu ya Bunge Sports kufikiri juu ya kutunga sera ya
michezo itakayoruhusu kuanzishwa kwa Shule za Michezo (Sports Academy) hapa
nchini. Lowassa ameyasema hayo jana, baada ya kuialika nyumbani kwake timu hiyo
iliyopiga kambi ya jijini Arusha tayari kwa mashindano ya Mabunge ya Afrika
Mashariki jijini Nairobi.
“Nilisikitika kweli Timu ya Taifa ya
Kilimanjaro Stars ilipofungwa na Burundi kwenye mchezo wa pili wa Mashindano ya
CECAFA huni Uganda, pamoja na juhudi za Rais Jakaya Kikwete kuleta makocha bado
tumefungwa na Burundi iliyotoka kwenye vita juzi!.
“Nyinyi ni watunga Sera, ni
wachezaji mnajua changamoto zinazofanya tusifike juu, umefika wakati wa kuwa na
Shule za Michezo zinazotambuliwa na Sera zetu.
“Mpira ni chakula cha Watanzania,
wanapenda mpira sana. Napendekeza baada ya kurejea anzeni kufikiria juu ya
kutunga Sera ya kuwa na Shule za Michezo. Kipingu amejitahidi kuwa na kitu kama
hiki lakini amebakia peke yake hakuna anayemuunga mkono,” alisema Lowassa.
Alisema kuwapo kwa Timu ya Bunge
Sports kutasaidia kufikiria juu ya mafanikio ya mchezo wa mpira wa miguu, pete
na michezo mingine. Kwa upande wake Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni
na Michezo, Amos Makalla aliyeongozana na timu hiyo alimwambia Lowassa kwamba
serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha Sera za michezo.“Sera na
sheria za sasa za michezo kweli haziendani kabisa na wakat,zote ni za zamani.
Serikali imejipanga kuzifanyia kazi.
“Changamoto uliyoitoa ya kuanzisha
Shule za Michezo na kuendeleza michezo nchini tunaipokea na tutaifanyia kazi.
“Nilipoteuliwa kuwa Naibu Waziri
kwenye Wizara hii niliwaambia watu na binafsi namshukuru Rais Kikwete, kwamba
upele ulipata mkunaji kwani mimi ni mwanamichezo na uwanjani ni kiungo
mchezeshaji,” alisema Makala.Naye Mwenyekiti wa Timu hiyo ya Bunge Sports
inayoundwa na wabunge kutoka Baraza la Wawakilishi na Bunge la Jamhuri, Iddi
Azan alimshukuru Mh. Lowassa kwa mawazo yake na kuahidi kuyafanyia kazi.
“Kwanza tunaahidi ushindi kwa nchi,
Bunge letu na haya uliyoyasema tunaahidi kuendelea kuyafanyia kazi kwani
tunatambua sheria na Sera za michezo zimepitwa na wakati,” alisema Azan.
Timu hiyo ya Bunge Sports ilikuwa na
wachezaji wake wote waliopo kwenye kambi jijini Arusha wanaounda timu ya Mpira
wa miguu na Pete.
Chanzo: Mjengwa blog
No comments:
Post a Comment