Saturday, December 1, 2012

Jaji mkuu aeleza sababu za kujitoa kesi ya Kamanda Lema...


JAJI Mkuu, Mohamed Chande Othman ameeleza sababu za kutokuwa kwenye jopo la majaji waliopangwa kusikiliza kesi ya aliyekuwa mbunge wa Chadema mkoani Arusha, Godbless Lema.
Jaji mkuu, alitoa maelezo haya jana alipozungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu kwenye mahafali ya 12 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).
“Ngoja nitolee ufafanuzi suala hilo ili jamii itambue utaratibu wa uendeshaji wa Mahakama ya Rufani, ambayo ina majaji 16 nchini,” alisema Jaji Othman.
Jaji Othman alisema kimsingi hajajitoa kushughulikia kesi hiyo, ila siku ambayo kesi hiyo inatajwa, atakuwa nchini India kuhudhuria Mkutano Mkuu wa 13 wa Majaji Wakuu Duniani.
Maelezo hayo ya Jaji Chande yamekuja siku tatu baada ya gazeti hili kuripoti kuwa, mkuu huyo wa mhimili wa Mahakama nchini amejitoa kusikiliza kesi hiyo na nafasi yake imechukuliwa na Jaji Bernard Luanda.
“Kwanza ifahamike kwamba, jaji wa Mahakama ya rufani hana ubia na kesi yoyote kwa mujibu wa utaratibu. Jaji yeyote kati ya majaji 16 wa mahakama ya rufani nchini ana mamlaka ya kusikiliza kesi yoyote ya rufani,” alieleza Jaji Othman.
Jaji Othman alifafanua kuwa, rufani ya Lema ni miongoni mwa kesi tatu za uchaguzi zilizobaki ambazo kwa mujibu wa taratibu za kisheria, huanza kusikilizwa baada ya muda wa mwaka mmoja na hukumu yake ni lazima itolewe ndani ya mwaka mmoja tangu kuanza kwake.
“Hivyo basi, kwa vile Jaji yeyote wa Mahakama ya Rufaa anaweza kuisikiliza kesi hiyo, hakukuwa na sababu inisubiri mimi,” alisema.
Jaji Othman alitaja kesi nyingine za uchaguzi zitakazoanza kufanyiwa vikao vya rufani na jopo la majaji wa Mahakama ya Rufani kuwa, ni ile ya Jimbo la Ubungo kati ya Hawa Ng’umbi na John Mnyika ambayo itakuwa chini ya jopo la majaji watatu; Jaji Nathalia Kimaro, Jaji Salum, Salum Masati na Jaji Katherine Oriyo.
Nyingine ni ya Jimbo la Ilemela ya Yusuph Yussuph Masengela Lupilya na wenzake wawili dhidi ya Highness Kiwia na wenzake wawili, ambayo itakuwa chini ya jopo la Majaji Januari Msofe, Jaji Beard Luanda na Jaji Salum Massati.
Alisema rufani ya Lema haijaanza kusikilizwa kwa jaji yeyote, hivyo yeye asingeweza kujitoa kwa kuwa hajapangiwa.
“Kinachotatiza hapa ni kwamba, watu wanaifungamanisha rufani hii na ile ya Arusha ambayo mimi nilikuwa miongoni mwa jopo la majaji kama mwenyekiti.
“Ile ilikuwa ni pingamizi ya rufani, wakati hii ya Dar es salaam ni rufani ambayo lazima isikilizwe hadi kufikia hukumu,” alisema Jaji Chande.
Alisisitiza kuwa, hajajitoa wala hajaombwa kujitoa kwenye rufani kwa kuwa haifungamani na ile ya Arusha ambayo alikuwa mwenyekiti wa Jopo la Majaji, huku akifafanua kuwa kesi hiyo ya Arusha ilikuwa ya kupinga rufani na hii ya sasa inayosikilizwa Dar es salaam ni ya rufaa na inaanza upya kisheria.
Alieleza kuwa, Desemba 4, mwaka huu vitaanza vikao vya majaji wa mahakama ya rufaa vya kupitia kesi za rufani za uchaguzi zilizopangwa kufanyika Dar es Salaam, Zanzibar na Iringa wakati atakuwa kwenye mkutano mkuu wa majaji duniani utakaofanyika Lucknow, India.
Kuhusu kesi hiyo kuhamishiwa Dar es Salaam, Jaji Othman alisema wanasheria wa Godbles Lema ndiyo walioomba ihamishiwe huko.
“Suala la kuhamishiwa rufani hiyo Dar es Salaam si la Mahakama ya Rufani bali waaliomba wanasheria wa Lema na hii inakubalika kwa lengo la kukimbizana na muda kabla ya kufikia tamati, kwani mahakama imepewa muda wa kumaliza kesi zote za uchaguzi kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao,” alisema Chande.
Mahakama hiyo ilikubali hoja ya wajibu rufaa kuwa, rufaa hiyo ilikuwa na dosari kutokana na tofauti ya vifungu vya sheria vilivyotumika katika hukumu iliyomvua ubunge Lema na vilivyotumika katika hati ya kukaza hukumu, iliyowasilishwa mahakamani sambamba na rufaa hiyo.
Hata hivyo, kilichomwokoa Lema ni kifungu cha 111 cha Kanuni za Mahakama, ambapo mahakama hiyo ilisema kuwa chini ya kanuni hiyo, dosari hizo zinaweza kurekebishwa.
Jaji Chande ndiye aliyekuwa kiongozi wa jopo la majaji watatu katika kesi hiyo akiwamo Salum Massati na Natalia Kimaro. Jaji Mkuu aliingia kwenye kesi hiyo akichukua nafasi ya Jaji Mbarouk Salim Mbarouk aliyekuwa amepangwa awali, ambaye sababu za kuondolewa hazikuwekwa wazi.
Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment