Mheshimiwa Spika;
Kwa heshima naomba
kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kukutana hapa leo
tukiwa wazima na wenye afya njema. Pili, naomba nichukue nafasi hii adhimu
kukushukuru wewe Mheshimiwa Spika kutupatia fursa hii adhimu ili kuwasilisha
mbele ya Baraza lako Tukufu taarifa ya maafa ya kuzama kwa meli ya MV. Skagit iliyotokea katika bahari ya Chumbe tarehe
18.07.2012.
1.0 Utangulizi
Mheshimiwa Spika, Meli
ya MV. Skagit ilitengenezwa nchini Marekani mwaka 1989 na imesajiliwa Zanzibar tarehe
25/10/2011, na kupewa nambari ya usajili 100144. Meli hiyo ina uzito wa GRT96
ambayo inamilikiwa na kampuni ya Seagull Sea Transport Limited ya Zanzibar .
Mheshimiwa Spika, Mnamo
tarehe 18.07.2012 majira ya saa saba na nusu za mchana ilipatikana taarifa ya
ajali ya kuzama kwa meli ya MV. Skagit katika bahari ya chumbe nje kidogo ya
mji wa Zanzibar .
Meli hiyo ilikuwa katika safari zake za kawaida ya kutoka Dar-es-Salaam kuja Zanzibar .
Kwa mujibu wa manifest
ya abiria iliyowasilishwa na wamiliki wa meli kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (Tanzania Ports Authority-TPA) na
Mamlaka ya Usafiri wa Baharini na Nchi Kavu Tanzania (Surface and Marine
Transport Authority-SUMATRA), meli hiyo ilikuwa imechukua jumla ya watu 290
wakiwemo abiria watu wazima 250, watoto 31 na mabaharia 9.
Mheshimiwa Spika,
Taarifa hii inaelezea kwa kina juu ya hali halisi ya tukio pamoja na hatua zote
zilizochukuliwa kuanzia tarehe 18/07/2012 hadi hivi sasa.
Mheshimiwa Spika, Mara
baada ya tukio hili, Kamati ya Kukabiliana na Maafa ya Taifa ilikutana kwa
ajili ya kuweka mikakati ya hatua za kuchukua pamoja na kuandaa taarifa rasmi
ya Serikali kwa wananchi kupitia vyombo vya habari.
Aidha, Baraza la
Mapinduzi lilikaa usiku wa tarehe 18.07.2012, na kutoa maagizo juu ya hatua za
kuchukua ikiwemo kuwepo kwa matayarisho katika hospitali ya mnazi Mmoja ya
kupokea majeruhi, kutayarisha eneo la Maisara kwa ajili ya mapokezi na utambuzi
wa maiti; kutayarisha eneo la kuzika miili ya marehemu huko Kama; kuweka
takwimu sahihi za majeruhi na waliofariki katika ajali hiyo; pamoja na kutolewa
kwa taarifa rasmi ya hali ya uokozi iliyokuwa inaendelea.
2.0 HATUA
ZILIZOCHUKULIWA
Mheshimiwa Spika
Kufuatia maagizo hayo ya Serikali, hatua zifuatazo zilichukuliwa: -
• Vituo cha mapokezi ya
wahanga wa ajali hiyo vilifunguliwa katika maeneo ya Bandari ya Malindi,
Hospitali ya Mnazi Mmoja na uwanja wa Maisara.
• Vikosi vya Ulinzi na
Usalama vilipelekwa katika maeneo mbalimbali ili kuimarisha huduma za ulinzi na
uokozi wa haraka.
• Kazi ya uchimbaji wa
makaburi katika eneo la Kama ilifanyika kwa
mashirikiano makubwa ya viongozi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Vikosi vya Ulinzi
na Usalama pamoja na wananchi. Jumla ya makaburi 80 yalichimbwa.
• Sala na dua maalum ya
kuwaombea marehemu wote ilifanyika baada ya sala ya Adhuhuri jana tarehe
22.07.2012 katika misikiti yote ya Unguja na Pemba na Kitaifa ilifanyika katika
Msikiti wa Mwembeshauri mjini Zanzibar .
• Kuorodhesha majina ya
wale wote ambao wanasadikiwa walikuwemo ndani ya chombo kilichopata ajali na
hadi sasa hawajulikani walipo.
Taarifa hizi
zinakusanywa kupitia ngazi ya Shehia na Wilaya kwa Unguja na Pemba na kwa Ofisi
za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam
kwa Tanzania Bara.
• Kutoa huduma ya
kuwasafirisha majeruhi baada ya kupata matibabu kurudi makwao. • Kutoa huduma
za usafiri kwa walioshiriki katika shughuli zote za operesheni.
3.0 MATOKEO YA
OPERESHENI
3.1 Shughuli za uokozi
Mheshimiwa Spika;
Kutokana na operesheni iliyofanywa na vikosi vya ulinzi na usalama kwa
mashirikiano makubwa ya wananchi yamepelekea hadi kufika tarehe 22.07.2012 kuwa
na idadi ya watu waliookolewa wakiwa hai kufikia 146 na miili ya waliofariki
dunia iliyopatikana kufikia 73.
Kati ya maiti hizo 68
zilipokelewa kituo cha Maisara na 5 zilipelekwa moja kwa katika eneo la
makaburi la Kama kwa vile maiti hizo zilikuwa
zimeshaharibika. Kwa waliookolewa wakiwa hai waliweza kufikishwa katika
Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa uchunguzi na matibabu. Hadi hii leo, majeruhi wote
walishatibiwa na kuruhusiwa kurudi majumbani mwao.
Mheshimiwa Spika; Katika
kituo cha Maisara maiti zilipangwa ili kuwawezesha ndugu na jamaa kutambua
maiti zao na kwa kurahisisha kazi hiyo, Shirika la Utangazaji kupitia kituo
chake cha Televisheni kilichukua picha za sura za marehemu na kuzionyesha
zikiwa tayari zimewekewa namba ili kurahisisha utambuzi na uchukuaji wa maiti
hizo.
Kupitia utaratibu huu,
jumla ya maiti 50 zilitambuliwa na kukabidhiwa jamaa na ndugu zao kwa ajili ya
mazishi. Idadi ya maiti ambao hawakutambuliwa ni 23 na mazishi yao
yalisimamiwa na Serikali katika eneo la Kama .
Aidha, maiti mmoja
aliyetambuliwa alilazimika kuzikwa Kama kwa vile mwili wake ulikuwa umeharibika
sana sambamba
na ndugu wa marehemu huyo kutochukuliwa na jamaa na ndugu zake. Kila maiti
alizikwa katika kaburi lake chini ya usimamizi wa mashekhe kutoka Ofisi ya Mufti
na Wakfu na Mali
ya Amana.
Aidha, katika kituo cha
Maisara huduma za uoshaji na sala ya maiti zilitolewa na pia wale wote
waliochukua maiti wao walipatiwa usafiri, sanda na ubao kwa ajili ya kuzikia.
3.2 Juhudi za kuitafuta
meli na watu waliokuwa hawajaonekana
Mheshimiwa Spika,
Katika jitihada za
Serikali za kuhakikisha miili zaidi ya marehemu iliyotokana na ajali ya meli
inapatikana, Serikali ilivitaka vikosi vyake ulinzi na usalama vikiongozwa na
KMKM kuendesha zoezi la kuitafuta meli na miili iliyosalia.
Kazi ya kuendesha
operesheni ya kuitafuta meli pamoja na abiria ilianza mara tu baada ya kusikia
kutokea kwa ajali hiyo. Jumla ya watu waliohai 146 waliokolewa siku hiyo na
maiti 31 zilipatikana. Asubuhi ya tarehe 19.07.2012, wazamiaji kutoka KMKM,
Jeshi la Wananchi wa Tanzania
na makampuni binafsi walifika katika eneo la tukio kwa ajili ya kuanza kazi
rasmi.
Wazamiaji hao
walifanikiwa kupata maiti 37 na hawakupata abiria aliye hai. Hata hivyo,
wazamiaji hao hawakuweza kuiona meli.
Mheshimiwa Spika,
Vikosi hivyo viliendelea
na jitihada za kuitafuta meli na watu waliokuwa hawajaonekana kwa kujigawa
katika makundi matatu. Makundi mawili yalihusika na kazi ya utafutaji wa watu
katika maeneo ya ukanda wa eneo la tukio. Kundi jengine lilijihusisha na kazi
ya uzamiaji (diving) kwa ajili ya kuitafuta meli chini ya bahari.
3.3 Kukusanya taarifa za
watu waliokuwa hawajaonekana kupitia Ofisi za Masheha na Wilaya:
Mheshimiwa Spika,
Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar iliziagiza ofisi zote za Wilaya na Shehia kuorodhesha majina ya watu
waliokuwa hawajaoneka na waliofariki na kuziwasilisha orodha hizo kwa Ofisi ya
Makamu wa Pili wa Rais ili kufanyiwa uhakiki na kupata orodha sahihi kwa ajili
ya matumizi na kumbukumbu za baadae.
Hadi kufikia tarehe
22.07.2012 zaidi ya watu 100 wameripotiwa hawakuonekana ama wakiwa hai au
maiti. Hata hivyo, kwa uhakiki wa awali imebainika kwamba baadhi ya watu
wameorodheshwa zaidi ya mara moja katika maeneo tofauti.
3.4 Viongozi Wakuu wa
Kitaifa kutoa mkono wa pole
Mheshimiwa Spika,
Viongozi Wakuu wa
Kitaifa pamoja na viongozi wengine wanatarajiwa kufanya ziara za kutoa pole na
kuzifariji familia zilizofiliwa na zilizopotelewa na ndugu zao kwa maeneo yote
yalizoathirika Unguja na Pemba . Kazi hiyo
inatarajiwa kufanyika hivi karibuni.
3.5 Kuratibu upokeaji wa
misaada
Mheshimiwa Spika
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kupitia Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa iliendelea
kupokea misaada ya kifedha na vifaa kutoka kwa watu binafsi, Mashirika ya
Kimataifa, Mashirika ya Umma, Mashirika yasiyo ya Kiserikali na taasisi
mbalimbali za ndani na nje ya nchi.
Hadi kufikia tarehe
22.07.2012 jumla ya Shilingi 320,000,000/-zimepokelewa na kuingizwa katika
akaunti ya Mfuko wa Maafa Zanzibar (Zanzibar Disaster Funds) ilioko Benki ya
Watu wa Zanzibar ,
ambayo imefunguliwa maalum kwa ajili ya michango ya aina hiyo. Aidha, vifaa na
bidhaa mbalimbali zimepokelewa kwa ajili ya kusaidia shughuli za operesheni ya
uokozi.
4.0 GHARAMA ZA
OPERESHENI Mheshimiwa Spika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliipatia Kamati ya Kitaifa ya
Kukabiliana na Maafa jumla ya shilingi milioni ishirini (20,000,000/-) kwa
ajili ya kugharamia shughuli za operesheni ambapo hadi kufikia tarehe
22.07.2012 fedha zote zilikwisha tumika.
5.0 TULICHOJIFUNZA
KUTOKANA NA TUKIO HILI (LESSONS LEARNED)
Mheshimiwa Spika
Kutokana na tukio hili la kuzama kwa meli ya MV. Skagit
tumeweza kujifunza mambo mbalimbali ambayo ni changamoto kwetu katika
kuimarisha kazi na huduma za kukabiliana na maafa nchini. Miongoni mwa mambo
hayo ni haya yafuatayo: –
• Umakini na maamuzi
sahihi na ya haraka yaliyochukuliwa na viongozi wetu yameweza kuleta ufanisi
mkubwa katika operesheni ya uokozi na hivyo kupelekea kuokoa maisha ya wananchi
wetu wengi.
• Muitikio wa haraka wa
taasisi mbalimbali za kukabiliana na maafa, zikiwemo taasisi za Serikali,
vyombo vya ulinzi na usalama, Sekta Binafsi na Jumuiya za Kiraia umepelekea
watu wengi kuweza kuokolewa wakiwa hai pamoja na kupatikana kwa maiti hali
ambayo imewezesha maiti wengi kuzikwa na familia zao.
• Kutokana na wananchi
wengi kutumia mtandao wa mawasiliano wa Zantel, kulisababisha ugumu wa
mawasiliano kutokana na minara ya kampuni hiyo kuzidiwa na matumizi.
• Udogo wa sehemu ya
kuhifadhia maiti (motuary) ulipelekea maiti wasiotambuliwa na jamaa zao kuzikwa
haraka na Serikali.
• Uhaba wa vifaa vya
kisasa vya uokozi pamoja na wataalamu wa uzamiaji (divers) umepelekea zoezi la
uokozi kuwa gumu na kuchukua muda.
• Kukosekana kwa taarifa
za uwezo wetu wa ndani wa kukabiliana na maafa ikiwemo uwezo wa vifaa na
wataalamu ni changamoto ambayo inapaswa kufanyiwa kazi.
6.0 SHUKRANI
Mheshimiwa Spika Kwa
mara nyengine tena kwa niaba ya Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa
naomba nimshukuru Rais wa zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein kwa juhudi zake
kubwa alizochukua ili kuhakikisha maisha ya wananchi yanaokolewa.
Tunamshukuru kwa
maelekezo yake na miongozo aliyotupatia ambayo kwa kiasi kikubwa ilitusaidia
kufanikisha kazi za uokozi.
Pia, tunamshukuru Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa maelekezo yao na msaada mkubwa walioutoa katika kukabiliana na
maafa hayo.
Aidha, tunamshukuru sana Waziri Mkuu,
Mheshimiwa Mizengo Kayanza Pinda kwa msaada mkubwa aliotupatia kupitia Ofisi
yake.
Tunawashukuru pia Makamu
wa Kwanza wa Rais Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi kwa kutupatia miongozo ya mara kwa mara katika
jitihada za kuokoa maisha ya wananchi na kupunguza athari za maafa yaliyotokea.
Vile vile tunatoa
shukrani za dhati kwa Baraza la Mapinduzi na Baraza la Usalama la Taifa kwa
maelekezo yao
juu ya hatua za kuchukuliwa katika kukabiliana na janga hili na majanga
yanayoweza kutokea baadae.
Shukrani za dhati pia
zinatolewa kwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa hatua zao za haraka zilizosaidia
kuokoa maisha ya wananchi wengi.
Pia tunaishukuru
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwa kuwa karibu nasi na kwa michango yao ya hali
na mali
katika kukabiliana na tukio hili la kusikitisha.
Mheshimiwa Spika
Shukrani pia zinatolewa kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri majini, angani na
nchi kavu kwa jinsi walivyoshirikiana na Serikali katika kulikabili tukio hili.
Wananchi wa maeneo ya
jirani hasa wavuvi na wamiliki wa hoteli na kampuni za kitalii wanapewa
shukrani za pekee kwa jinsi walivyoshiriki kikamilifu tokea hatua za awali
baada ya kupatikana taarifa za kuzama kwa meli ya Skagit .
Tunashukuru washirika wa
maendeleo na wawakilishi wa nchi marafiki kwa jinsi walivyolichukulia suala
hili na kutuunga mkono katika msiba huu wa kitaifa.
Vilevile tunazishukuru
taasisi za kidini hasa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana na Ofisi ya Mufti kwa
kusaidia maandalizi ya mazishi ya marehemu waliotokana na ajali hiyo.
Tunawashukuru madaktari
na wauguzi wa hospitali ya Mnazi Mmoja kwa namna walivyoshirikiana na Kamati.
Tunawashukuru wajumbe
wote wa Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa na wafanyakazi wa Idara ya
Kukabiliana na Maafa kwa kazi kubwa waliyoifanya kwa kipindi chote toka kutokea
kwa janga hili.
Tunawashukuru wamiliki
wa vyombo vya habari na wanahabari na wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania kwa
jumla kwa kupokea tokeo hili kwa masikitiko makubwa katika kukabiliana na janga
hili.
Aidha, tunawashukuru
wale wote walioweza kuchangia kwa hali na mali katika msiba huu.
7.0 HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, baada
ya kutoa maelezo hayo nawaomba wajumbe wa Baraza lako tukufu waipokee taarifa
hii na kutupatia ushauri ili uweze kutusaidia katika harakati za kukabiliana na
maafa hapa nchini. Mheshimiwa Spika, kwa heshima na taadhima naomba
kuwasilisha.
Ahsanteni sana ………………………………
MOHAMED ABOUD MOHAMED
[MBM]
WAZIRI WA NCHI OFISI YA MAKAMU WA PILI WA RAISZANZIBAR
�
WAZIRI WA NCHI OFISI YA MAKAMU WA PILI WA RAIS
No comments:
Post a Comment