Waandishi Wetu
SIKU moja baada ya Rais
Jakaya Kikwete kusema daktari anayeona kuwa hawezi kufanya kazi serikalini bila
ya kulipwa mshahara wa Sh3.5 milioni aache kazi, viongozi wa dini, wanasiasa, wabunge
na wasomi wamemtaka apunguze jazba.Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana
walisema mgogoro wa madaktari na Serikali bado unajadilika huku Mbunge wa
Ubungo (Chadema), John Mnyika akienda mbali zaidi na kusema Serikali iache
kisingizio cha Mahakama kulizuia Bunge kujadili mgogoro baina yake na
madaktari, wakati yenyewe inajadili na kutoa maelezo.
Juzi, katika hotuba yake
ya kila mwisho wa mwezi, Rais Kikwete alisema Serikali haiwezi kuahidi kuwa
inao uwezo wa kuwalipa madaktari mshahara huo na posho zote kwani ikifanya
hivyo malipo ya daktari anayeanza kazi yatakuwa Sh7.7 milioni kwa mwezi kitu
ambacho hakiwezekani.
Jana, wakizungumza kwa
nyakati tofauti, wadau hao walisema mgogoro huo kati ya Serikali na madaktari
bado unajadilika na kusisitiza kuwa hotuba ya Rais Kikwete haijajibu madai ya
madaktari.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ally alisema
ingekuwa jambo jema kama kungekuwa na
uwezekano wa mazungumzo kuendelea.
Alisema kauli ya Rais ni
upande wa Serikali hivyo, ingekuwa vyema kama
madaktari nao wangepata nafasi ya kujieleza.
Wanasiasa
Mbunge wa Kasulu Mjini
(NCCR-Mageuzi), Moses Machali alimtaka Rais apunguze hasira na kuitaka Serikali
ikubali kurudi katika meza ya mazungumzo hata kama
ndiyo iliyokuwa ya kwanza kuwapeleka mahakamani madaktari waliogoma.
Alisema kama Serikali
haiwezi kulipa kiwango cha mshahara kilichopendekezwa na madaktari, irudi
katika meza ya mazungumzo ili kutafuta suluhu ya mgomo huo unaowaumiza zaidi
wananchi.
“Warudi kwenye meza ya
majadiliano siyo kila mmoja kusema la kwake na kuacha mgomo kuendelea huku,
watu wakiteseka hospitalini bila msaada wowote,’’ alisema Machali.
Naibu Katibu Mkuu wa
Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro alisema Serikali haipaswi kuwafukuza
madaktari kwa kuwa imetumia gharama kubwa kuwasomesha.
“Ikiwafukuza madaktari
italazimika kuwaleta walio nje ya nchi ambao ni gharama kubwa… Serikali itatue
mgogoro huu,” alisema.
Mbunge wa Ubungo
(Chadema), John Mnyika alisema Serikali iache kutumia kisingizio cha Mahakama
kulizuia Bunge kujadili mgogoro wa madaktari wakati yenyewe ikitoa ufafanuzi.
“Uamuzi wa Serikali
kutoa kauli kupitia hotuba ya Rais una mwelekeo wa kukwepa wabunge kujadili
hotuba husika ambayo awali, ilielezwa kuwa ingetolewa na Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda bungeni. Inawanyima haki wabunge wasitimize wajibu wa kikatiba wa Ibara
63 (2) wa kuisimamia Serikali kwa niaba ya wananchi,” alisema Mnyika.
Mnyika alisema, kwa kuwa
Bunge litajadili mapitio ya utekelezaji wa Bajeti ya Ofisi ya Rais kwa mwaka wa
fedha 2011/2012 na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2012/2013
kuanzia leo, ni muhimu wabunge wakajadili pia masuala ambayo Rais ameyaeleza
kwa taifa na kutimiza wajibu wa kikatiba.
“Hotuba ya Rais
imeendeleza kauli za upande mmoja ambazo zimekuwa zikitolewa na Serikali kuhusu
mgogoro huo bila taifa kupewa fursa ya kupata maelezo na vielelezo vya upande
wa pili, hivyo Serikali imetoa kauli yake hadharani badala ya bungeni au
mahakamani.
Viongozi wa dini
Mchungaji wa Kanisa la
Maombezi (GRC) Ubungo Kibangu, Anthony Lusekelo alisema madaktari hao
wanatakiwa kurudi kazini kwa kuwa tayari Serikali imeshasema kuwa haina fedha
za kuwalipa na kuongeza kuwa hata kama wana madai yao , wadai wakiwa kazini.
“Asilimia kubwa ya
madaktari wamesomeshwa na Serikali… Serikali hiyohiyo inawaeleza kuwa haina
fedha za kuwalipa kama wanavyotaka, binafsi
nawaomba tu warudi kazini kwa kuwa mgomo wao unawaathiri zaidi wananchi kuliko
hata hao viongozi wa Serikali.
“Tunajua tulikotoka ila
hatujui tunakokwenda, kama ni kuboreshwa kwa sekta nzima ya afya, Serikali
imesema itatekeleza hilo ,
haiwezi kuyatekeleza kwa siku moja, haya mambo yanajadilika.
Alisema kama Serikali
itakuwa na makosa yake, itayajibu mbele za Mungu... “Madaktari watekeleze
wajibu wa kazi yao
kwa uwezo wa Serikali iliyopo madarakani.”
Askofu Msaidizi wa Jimbo
Katoliki la Kagera, Dk Methodius Kilaini alisema kanisa hilo haliwezi kuunga mkono mgomo huo.
Alisema pamoja na kuwa
madaktari wana madai yao , jukumu lao kubwa ni
kufuata maadili ya kazi yao
ambayo hayawaruhusu kugoma.
Katibu Mkuu wa Makanisa
ya Kipentekoste Tanzania ,
Askofu David Mwasota alisema madaktari wanatakiwa kutenganisha siasa na maadili
ya kazi yao .
“Hata kama Serikali ina
makosa yake lakini, wao kuendelea kugoma si jambo zuri kwa jamii na hata mbele
za Mungu, watumie njia nyingine kudai madai yao , lakini waendelee kutoa huduma. Madaktari
ni watu muhimu, kurudisha viungo vya binadamu katika hali ya kawaida si kazi
ndogo, warudi kazini kuokoa mamia ya Watanzania maskini.”
Katibu wa Baraza Kuu la
Waislamu wa Tanzania
(Bakwata), Mkoa wa Arusha Abdulkarim Jonjo alisema ipo haja kwa Serikali kukaa
meza moja na madaktari hao.
Askofu Mkuu wa Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mjini Kati, Thomas Laizer
alisema mgogoro wa madaktari umalizwe kwa mazungumzo.
Alisema Serikali
inapaswa kuwa wazi inapozungumza na madaktari kwa kueleza ni mambo gani yanawezekana
na kwa muda gani ili, kuondoa migogoro.
Akizungumza juzi katika
ibada maalumu katika kanisa la KKKT Kimandolu, alisema ili kuondoa hisia kuwa
Serikali inahusika na tukio la kutekwa Dk Ulimboka ni lazima iundwe tume huru.
“Nadhani ili kuondoa
haya maneno ambayo si jambo dogo, Serikali inapaswa kuunda tume huru kuchunguza
tukio hili, kwani inawezekana waliohusika ni watu wengine tu wenye nia mbaya na
Serikali lakini ili ukweli ujulikane ni muhimu kuwepo tume huru,” alisema Askofu
Laizer.
Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam , Alhaj
Mussa Salum aliwataka madaktari kutii agizo lililotolewa na Mahakama kwa kurudi
kazini.
“Rais ameshaeleza wazi
kwamba Serikali haina fedha za kuwalipa kama
wanavyotaka, warudi tu kazini na kuweka masilahi ya Watanzania mbele na kuacha
kutanguliza masilahi binafsi,” alisema Sheikh Salum.
Wanaharakati
Mkurungezi Mtendaji wa
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema
hotuba hiyo ya Rais haina jipya zaidi ya kurudia maelezo yake ya awali
alipokutana na Wazee wa Mkoa wa Dar es
Salaam .
“Nilitarajia kuwa hotuba
itakuwa tofauti lakini sivyo. Amerudia maelezo yaleyale aliyoyasema Machi 12
(mwaka huu) alipokutana na wazee katika Ukumbi wa Diamond Jubilee,” alisema
Bisimba.
Wakili Peter Jonathan
alisema kama kweli Serikali inataka kurudisha
imani kwa Watanzania kuhusu tukio la Dk Ulimboka ni lazima ijisafishe kwa
kuunda tume huru nje ya Serikali.
“Watafute hata Jaji
mstaafu, si lazima atoke Tanzania
kuongoza tume huru ikibidi tuchukue hata nje ya nchi ili wakitoa taarifa iweze
kuaminiwa na jamii na hiyo ndiyo dhana sahihi ya utawala bora,” alisema.
Mjumbe wa Chama cha
Watabibu wa Tiba Asili (ATME), Boniventure Mwalongo ameitaka Serikali kuacha
kutumia nguvu kushughulikia madai ya madaktari badala yake ipanue wigo wa
majadiliano ili kutatua tatizo hilo .
“Nimesikiliza hotuba ya
Rais lakini, haijaonyesha kama kuna jawabu la
mgomo hivyo wapanue wigo wa majadiliano ili kumaliza mgogoro huu,” alisema
Mwalongo.
Habari hii imeandikwa na
Fidelis Butahe,
Nora Damian, Bakari
Kiango, Freddy Azzah, Daniel Mwingira, Dar; Daniel Mjema, Moshi; Mussa Juma,
Arusha na Frederick Katulanda, Mwanza.
Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment