"NI saa 12:45
asubuhi, bado kiza kimetanda katika eneo hili la Msitu wa Mabwepande. Mbele
yangu namwona mtu akiwa amekaa chini, pembeni ya barabara akiwa amelowa damu
mwili mzima.
"Ninapomkaribia
nasikia sauti ya mtu huyo ikisema kwa taabu; naomba msaada jamani… naomba
msaada jamani, hivi ndivyo anavyoanza kusimulia Juma Mgaza Abdallah, mtu wa
kwanza kumwona Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania , Dk Steven Ulimboka baada
ya kutekwa, kupigwa na kutupwa katika Msitu wa Mabwepande nje kidogo ya Jiji la
Dar es Salaam.
Abdallah, anasema mara
baada kumwona daktari huyo akiwa katika hali hiyo, alijaribu kumkokota kumtoa
eneo hilo ,
lakini alishindwa kutokana na hali mbaya aliyokuwa nayo.
Baada ya hapo, aliamua
kusubiri mtu mwingine apite eneo hilo
ili amwombe wasaidiane kumpeleka Kituo cha Polisi Bunju.
Anasema muda mfupi
baadaye aliona gari likija mbele yao ,
akalinyooshea mkono kulisimamisha. Liliposimama, akamweleza dereva hali
aliyokuwa nayo Dk Ulimboka na kwamba anahitaji msaada wa haraka.
Abdallah ambaye hadi
wakati huo alikuwa hamfahamu mtu ambaye alikuwa akimsadia kuwa ni kiongozi wa
madaktari kutokana na sura yake kuvimba, anasema walimwingiza katika gari hilo na kumpeleka Kituo
Kidogo cha Polisi Bunju.
Anasema, Dk Ulimboka
wakati huo alikuwa akiendelea kuvuja damu katika baadhi ya majeraha yake huku
akiwa hana suruali na kubaki na bukta tu, huku akizungumza kwa taabu.
Kituo cha Polisi Bunju
Baada ya kumfikisha
kituoni hapo, walitoa maelezo namna walivyomwokota na kumsaidia kumfikisha
hapo.
Polisi baada kumhoji Dk
Ulimboka, aliwatajia namba ya simu ya rafiki yake aitwaye Dk Deo. Walipompigia
na kumweleza tatizo hilo ,
aliamua moja kwa moja kwenda Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, kutoa
taarifa hizo na hatimaye kuandamana na watu kadhaa kutoka hapo akiwamo
Mkurugenzi wake, Hellen-Kijo Bisimba.
Wawasili kituoni
Mratibu wa Mtandao wa
Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania wa kituo hicho, Onesmo Olengurumwa,
anasema waliwafika Polisi Bunju saa 3:36 asubuhi na kumkuta Dk Ulimboka akiwa
amekalishwa kwenye benchi huku damu ikiwa imeganda kwenye majeraha mwilini.
Olengurumwa anasema
waliwahoji polisi waliokuwa kituoni hapo kwa nini wakae na mtu aliyeumia kiasi
hicho muda mrefu bila ya kuita gari la wagonjwa kumchukua ili kuwahi kupatiwa
matibabu.
Olengurumwa anasema
polisi walisema kwamba, walikuwa wanawasubiri ndugu zake wafike.
Baada ya muda mfupi,
akiwa ameingizwa kwenye gari kupelekwa hospitali, Dk Ulimboka aliomba maji ya
kunywa akisema ana kiu sana ,
lakini alipopewa, alikunywa kidogo akashindwa.
Anasema wakiwa njiani,
alikuwa akilalamika kuwa anasikika maumivu makali huku akisisitiza kuwa tukio
la kutekwa na kupigwa lilikuwa la kumuua.
"Jamani hawa watu
walitaka kuniua walikuwa wamepanga kuniua," alisikika mara kwa mara
akisema Dk Ulimboka wakati anapelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kupatiwa
matibabu.
Maelezo ya Dk Ulimboka
Baada ya Dk Ulimboka
kuokotwa aliweza kuzungumza na kurekodiwa muda mfupi baada ya kutolewa msituni
na mazungumzo yake yalikuwa hivi;
“Nilikamatwa na watu hao
usiku wa Jumanne nikiwa maeneo ya Leaders Club, Kinondoni na daktari mwenzangu
baada ya kupigiwa simu na mtu mmoja ambaye alidai kuwa anafanya kazi Ikulu.
“Kuna jamaa mmoja
anafanya kazi Ikulu, kama siku tatu mfululizo
alikuwa akitaka kukutana na mimi ila nilishindwa kukutana naye kwa kuwa
nilikuwa na kazi nyingi na wakati mwingine mpaka usiku,” alisema Dk Ulimboka.
Huku akizungumza kwa
taabu kutokana na mdomo wake kuvimba, alisema siku hiyo mtu huyo alimpigia tena
simu na kumtaka wakutane.
“ Jana (Jumanne)
alinipigia simu na nikamwambia daktari mwenzangu twende tukaonane naye, wakati
huo alitueleza kuwa alikuwa maeneo ya Kinondoni Stereo,” alisema Ulimboka na
kuongeza:
“Tulipofika maeneo hayo
tukampigia simu na akatueleza kuwa alikwisha ondoka, baadaye tukamweleza sehemu
tulipo mimi pamoja na mwenzangu.”
Alisema kuwa, wakati
anakutana na mtu yule maeneo ya Leaders Club, hakuwa na amani.
“Kwa kweli siku ile
nilivyoonana na mtu yule sikuwa na amani kabisa ya kukaa eneo lile,” alisema Dk
Ulimboka.
Alisema kuwa wakati
wakiendelea na maongezi ya kawaida, bado aliendelea kuwa na mashaka na mtu
yule.
“Katikati ya maongezi
nikaona ameanza kuzungumza na simu, kila tukitaka kuagana alikuwa akizungumza
na simu, sijui nini kilikuwa kinachelewesha sisi kuagana,” alisema Dk Ulimboka
na kuongeza:
“ Ghafla walitokea watu
kama watano na kusema kuwa hawana tatizo na mtu yeyote katika eneo hilo isipokuwa mimi.
Wakati sijakaa sawa,
waliniburuza hadi barabara ya lami kwa kuwa eneo hilo lilikuwa karibu na barabara.”
Aliongeza,
“Nilipowauliza wananipeleka wapi, wakaniambia kuwa mimi nasumbua sana na nitajua hukohuko,
waliniingiza katika gari jeusi, lakini halikuwa na namba. Niliwauliza kosa gani
nimefanya? Hawakunijibu kitu na kusema, we twende utajua hukohuko.’’
Alisema alipokuwa ndani
ya gari hilo
watu hao walimpiga na kwamba walipofika maeneo ya Victoria, walichukua sweta
nyeusi na kumfunga usoni, jambo lililomfanya ashindwe kuona kinachoendelea
ikiwa ni pamoja na alikokuwa akipelekwa.
“Walinipiga mateke ya
mbavuni, wakati mwingine walitumia vitako vya bunduki, kila nilipokuwa najaribu
kuangalia ninapokwenda nilishindwa,” alisimulia Dk Ulimboka.
Alisema kuwa watu hao
walimpeleka katika nyumba moja ambayo hakujua iko sehemu gani ambapo walimshusha
na kuanza kumshambulia kwa mateke mfululizo kila sehemu ya mwili. Wakati huo,
wote walimshinikiza awaambie nani yupo nyuma ya mgomo wa madaktari.
“Tangu saa sita usiku
mpaka saa 9:00 alfajiri walikuwa wananipiga tu, kuna wakati nilijaribu kukimbia
wakapiga risasi juu nikasimama na sikuweza kukimbia tena,” alisema Dk Ulimboka
na kuongeza:
“Nilisimama, wakaendelea
kunipiga, niliwasikia wakisema ama wanichome sindano ya sumu nife au
kunikanyaga na gari. Baadaye wakaanza kuning’oa meno na kucha kwa kolea huku
wakinilazimisha kusema nani yupo nyuma ya mgomo wa madaktari."
Alisema kuwa, watu hao
walikuwa na bunduki kubwa ambayo hakuweza kuitambua ni aina gani.
“Waliniambia kuwa
ninajua ninachokifanya hivyo wanaweza kunichoma sindano ya sumu nife au wanikanyage
na gari nife,” alisimulia.
Dk Ulimboka alisema kuwa
awali hakuwa na shaka na watu hao kwa kuwa alidhani ni polisi, lakini baadaye
alishindwa kuwaelewa kwani watu hao walimchanganya.
“Sikuweza kuwatambua ila
naweza kusema ni askari, walipokuwa wananipeleka niliwauliza mnanipeleka wapi
na wakati huo nilikuwa sioni mbele ila ilikuwa kama
maeneo ya Mwenge hivi,” alisema Dk Ulimboka.
Alisema kuwa baadaye
alipoteza fahamu na hakuweza kuona chochote zaidi ya kusikia sauti za watu hao
kwa mbali.
“Nilikuwa sioni na
nilipoteza fahamu nikawa nasikia tu wakinibeba, gari lilitembea muda mrefu,
sikujua ni wapi tunakwenda, kumbe ndio huko Mabwepande,” alisema.
Alisema kuwa walifika
maeneo ya barabara ya vumbi na baadaye wakamshusha na kumbeba hadi msituni.
“Waliniburuza na
kuniacha huko na muda wa saa kumi alfajiri ndipo nikazinduka na kuanza
kujiburuza kuelekea barabarani ambako nilisaidiwa na mtu mmoja ambaye
simtambui,” alisema Dk Ulimboka.
No comments:
Post a Comment