Bodi ya Wadhamini ya
Hospitali ya Taifa Muhimbili ilikutana tarehe 28 Juni 2012 kujadili na
kutathmini hali ya utendaji na utoaji wa huduma hivi sasa katika Hospitali.
Imebainika kwamba utoaji huduma umeathirika kutokana na mgomo wa baadhi ya
madaktari unaondelea kwa takriban wiki moja sasa tangu ulipoanza Jumamosi
yatarehe 23 Juni 2012.
Baada ya tathmini hiyo,
Bodi ya Wadhamini imeagiza yafuatayo:
(i) Madaktari waliopo
kazini waendelee na kazi kama kawaida;
(ii) Madaktari waliogoma
warejee kazini kutii amri ya Mahakama Kuu Kitengo cha kazi, kwa mujibu wa
Kifungu Na. 76 (1) na (2) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka
2004.
(iii) Madaktari waliopo
likizo warejee kazini mara moja. Utaratibu wa kufidia likizo na nauli zao
umeandaliwa.
(iv) Uongozi wa
Hospitali uwachukulie hatua za kinidhamu wafanyakazi wote watakaoendelea
kutokuhudhuria kazini na kufanya kazi bila sababu za msingi kwa mujibu wa
Sheria, Kanuni na taratibu za kazi;
(v) Uongozi wa Hospitali
ufute mara moja ‘rotations’ za Madaktari waliopo kwenye mafunzo kwa vitendo
(interns); na
(vi) Uongozi wa
Hospitali uwapange (re-deploy) Madaktari na Madaktari Bingwa waliopo kwenye
maeneo yaliyoathirika wakati huu wa mgomo.
Aidha, Bodi ya Wadhamini
inawashukuru sana
madaktari na wafanyakazi wote ambao wameendelea kuwahudumia wagonjwa wetu na
wananchi kwa ujumla. Vilevile, Bodi ya Wadhamini inawasihi madaktari na
wafanyakazi wote wawe na subira na waheshimu sheria, kanuni na taratibu
zilizopo pamoja na maadili ya taaluma zao.
_________________
Dkt. Gabriel Upunda
KAIMU MWENYEKITI
BODI YA WADHAMINI
No comments:
Post a Comment