Na: Mahmoud Ahmad Arusha
Serikali imetishia
kuwatimua wawekezaji wa kampuni ya madini ya Tanzanite one iliyopo Mererani
wilayani Simanjiro iwapo watashindwa kulipa deni la zaidi ya dola za kimarekani
milioni 2.2 zilizotokana na ukwepaji kodi .
Katibu mkuu wizara ya
nishati na madini Eliakim Maswi alitangaza msimamo wa serikali wa kupitia upya
mikataba ya makampuni ya madini hapa nchini baada ya kugundulika kuwa yapo
makampuni kadhaa yamekuwa yakiendesha shughuli zake za madini bila kulipa
ushuru wa serikali kinyume cha sheria.
Akizungumza na chama cha
wanunuzi na wauzaji wa madini nchini TAMIDA,jijini Arusha jana,Maswi alisema
kuwa kampuni ya Tanzanite one imekuwa ikikwepa kulipa kodi ya mrahaba wa madini
tangu mwaka 2004 hadi 2008 na kufikia kiasi cha shilingi bilioni 3.4 fedha za
kitanzania.
Alisema kuwa kampuni
hiyo ilikuwa ikitumia ujanja wa kukwepa kulipa mrabaha wa mauzo pale inapokuta
soko la madini nje ya nchi limeongezeka na kwamba serikali kupitia kitengo cha
ukaguzi wa madini iliweza kubaini ukwepaji huo wa kodi na kuiamuru kampuni hiyo
kulipa kiasi hicho cha fedha au ifungashe virago.
‘’tulibaini ukwepaji wa
ulipaji kodi kwa kampuni ya Tanzanite one baada ya kuanzisha kitengo maalumu za
ukaguzi wa migodi hapa nchini na tulipoifikia kampuni hiyo ndipo tulipobaini
imekwepa kulipa kodi kiasi hicho,na hivi sasa tunaanza kupitia upya ikataba ya
makampuni ya madini’’alisema Maswi
Aidha alifafanua kuwa
kampuni hiyo iligoma kulipa deni hilo ikidai ni kubwa sana ,ndipo serikali
ilipotaka kufanya ukaguzi upya ,kupitia wakaguzi wake , lakini kampuni hiyo
iligoma na kudai kuwa ipo tayari kulipa deni hilo .
Aliongeza kuwa iwapo
kampuni hiyo ingegoma kulipa deni hilo
serikali ilikuwa tayari kuwatimua na kuwamilikisha wazawa mgodi huo.
Kwa mujibu wa kamishina
wa madini kanda ya kaskazini Benjamin Mchwampaka alisema kuwa tayari kampuni
hiyo imeshaanza kulipa deni hilo na kwamba hadi
sasa imeshatoa malipo ya dola 200,000 zaidi ya fedha za kitanzania milioni
310,huku serikali ikiitaka kuhakikisha inamaliza kulipa deni hilo hadi kufikia jamuari mwaka 2013.
Hata hivyo katibu huyo
aliitaka TAMIDA kuisaidia serikali kuyafichua makampuni yanayokwepa kulipa
ushuru wa madini wakiwemo baadhi ya wafanyabiashara wakubwa ili wachukuliwe
hatua na kusisitiza kuwa kwa sasa serikali imeanza mkakati wa kupitia upya
mikataba ya makampuni ya madini hapa nchini.
No comments:
Post a Comment