Friday, August 17, 2012

Jaji alietajwa vibaya katika utetezi wa Tundu lissu ndie atakuwa miongoni mwa wanajopo watakaosikiliza rufaa ya Godbless Lema... Imekaaje hii?


Jaji Mbarouk Salim Mbarouk alietajwa katika utetezi wa Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu, kuwa ni miongoni mwa Majaji wasio na sifa ni miongoni mwa watakaosikiliza rufaa ya kupinga kuvuliwa ubunge kwa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA), ambayo imepangwa kusikilizwa Septemba 20, mwaka huu.

Majaji wengine wa mahakama ya rufaa watakaosikiliza rufaa hiyo ni Natalia Kimaro, na Salumu Massati. Kwa mujibu wa taarifa za kikao cha Mahakama ya Rufaa cha Arusha, rufaa hiyo iliyofunguliwa na Lema akipinga uamuzi uliotengua ubunge wake kufuatia shauri lililofunguliwa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, inatarajiwa kusikilizwa kwa siku moja ambapo baada ya hapo itapangwa tarehe kwa ajili ya kutoa uamuzi. 

Awali, Lema kupitia wakili wake, Method Kimomogoro, aliwasilisha kwenye mahakama hiyo hoja 18 za madai akipinga kutenguliwa kwa ubunge wake na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Aprili 5, mwaka huu.
 

Kwenye baadhi ya madai hayo, Lema aliiomba Mahakama ya Rufaa kutengua uamuzi wa Mahakama Kuu, uliotengua ubunge wake, huku akiitaka imtangaze kuwa mbunge halali wa Jimbo la Arusha Mjini.
 

Aidha, aliitaka mahakama hiyo ya juu, iwaamuru walalamikiwa katika shauri hilo walipe gharama za rufaa hiyo pamoja na zile za kesi iliyomalizika kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.
 

Katika madai mengine, Lema anamlalamikia, Jaji Gabriel Rwakibarila, aliyesikiliza kesi hiyo kuwa, alitoa uamuzi wake kwa kuzingatia maneno ya uvumi, huku akipuuza ushahidi uliotolewa mahakamani hapo.
 

Lema anadai kuwa, Jaji alikosea wakati alipoamua kuwa mpiga kura yeyote anaruhusiwa kupinga matokeo ya uchaguzi hata kama haki zake za msingi hazijaguswa.
 

Kesi hiyo iliyotengua ubunge wa Lema, ilifunguliwa na wanachama watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM); Mussa Mkanga, Agness Mollel na Happy Kivuyo, wakidai kuwa wakati wa kampeni mbunge huyo alimdhalilisha mgombea mwezake, Dk. Batilda Burian kwa kutumia lugha za matusi.




No comments:

Post a Comment