TUHUMA kwamba baadhi ya
vigogo Serikali wameficha mabilioni ya fedha nchini Uswisi jana ziliibuka tena
bungeni, huku Kambi ya Upinzani ikidai kwamba inawafahamu wahusika wa ufisadi
huo na kutishia kuwataja ikiwa Serikali haitawataja.
Naibu Kiongozi wa Upinzani
Bungeni, Zitto Kabwe aliitaka Serikali kuwataja kwa majina viongozi na
wafanyabiashara wakubwa walioficha Sh315.5 bilioni nchini Uswisi, akisema
kwamba watu hao “wanafahamika”.
Juni mwaka huu, Benki
Kuu ya Uswisi ilitoa taarifa inayoonyesha kuwapo kwa kiasi cha Sh315.5 bilioni
zilizotoroshwa Tanzania
na kufichwa nchini humo na vigogo ambao ni wanasiasa pamoja na wafanyabiashara.
Akiwasilisha hotuba ya
kambi yake kuhusu Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Fedha na Uchumi bungeni
jana, Zitto ambaye pia ni Waziri Kivuli wa wizara hiyo alisema mmoja wa
viongozi wa juu wa Tanzania na baadhi ya mawaziri wa Serikali za awamu
zilizopita ni miongoni mwa wamiliki wa fedha hizo.
“Kambi ya Upinzani
bungeni imepata taarifa kuwa mmoja wa viongozi wa juu kabisa wa Tanzania na
baadhi ya mawaziri wa awamu zilizopita ni miongoni mwa fedha hizi,” alisema
Zitto.
Pia aliitaka Serikali
kuliambia taifa ni hatua gani itakazochukua kurejesha fedha hizo pia kuwataka
wamiliki wake na kama ikishindwa, wao
watawataja.
“Tunaitaka Serikali
kutoa taarifa rasmi ya hatua gani imechukua mara baada ya taarifa ile kutoka
Benki ya Taifa ya Uswisi ilipotolewa,” alisema Zitto na kuongeza:
“Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni italazimika kuweka wazi taarifa na majina ya watu wenye umiliki wa
fedha hizo iwapo Serikali haitatoa taarifa rasmi,” alisisitiza.
Fedha hizo zinadaiwa
kutokana na biashara (deals) zilizofanywa na watendaji wa Serikali na
wafanyabiashara kwenye Sekta za Nishati na Madini na kwamba sehemu kubwa ya
fedha zililipwa na kampuni za utafutaji mafuta na gesi katika pwani ya Mkoa wa
Mtwara zilizopewa mikataba kati ya mwaka 2004 na 2006.
Baada ya Zitto kumaliza
kuwasilisha hotuba yake, Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole-Sendeka
aliomba mwongozo wa Spika kuhusu suala hilo .
Sendeka alisema Zitto
alisema miongoni mwa walioficha fedha hizo ni kiongozi wa juu wa Tanzania ,
lakini akashangaa Serikali kutohoji juu ya kauli hiyo.
“Mheshimiwa Naibu Spika,
mheshimiwa Zitto amewatuhumu viongozi wa Serikali na kiongozi wa juu kabisa
kuwa wameficha fedha Uswisi,” alisema.
Alisema, lakini pamoja
na tuhuma hizo, hakuna kiongozi wa Serikali aliyesimama na kutolea ufafanuzi
hivyo akaomba mwongozi ili Zitto aruhusiwe kuwataja.
Sendeka alisema tuhuma
hizo ni nzito na zimeichafua sura ya Serikali hivyo ni vyema ijulikane ni nani
kati ya Serikali na Zitto atabeba mzigo wa kuwataja.
Naibu Spika, Job Ndugai
alisema angetoa mwongozo huo baada ya kuipitia hotuba hiyo ya Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni na kuona kama ina matatizo. Hata
hivyo, hakutoa mwongozo huo.
Chanzo:http://www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment