Na Johary Kachwamba-Maelezo
UJENZI wa Kivuko chenye uwezo wa kusafiri kwa kasi ya kilometa 40
kwa saa moja, unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi nane kwa lengo la kupunguza
msongamano wa magari jijini Dar-es-salaam.
Kivuko hicho kitakachotoa huduma ya usafiri kati ya Bagamoyo na
Kigamboni kupitia Tegeta na vituo vigine sita (6), kina uwezo wa kubeba zaidi
ya abiria 300.
Akizungumza jijini Dar-es-salaam wakati wa kusainiwa rasmi mkataba
wa manunuzi ya kivuko hicho, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli amesema pesa
zote zilizotumika katika manunuzi ya kivuko hicho zimetolewa na Wakala wa
Ufundi na Umeme (TAMESA) na hivyo ni pesa za wananchi.
"kupanda kwa nauli ya vivuko vyetu na usimamizi mzuri wa pesa
zinazopatikana katika vivuko hivyo ndiyo matunda ya kupatikana kwa kivuko hiki,
hakuna pesa ya msaada hapo ni pesa za watanzania" alisema Waziri Magufuli.
Mradi huu wa serikali umeanza na jiji la Dar-es-salaam na kuahidi
kufanya hivyo hata kwa mikoa mingine inayoweza kutumia aina hii ya usafiri, kama Kigoma na Mwanza.
Aidha Serikali ameiasa kampuni yenye dhamana ya kujenga kivuko
hicho kufuata makubaliano yaliyowekwa, kwa kukamilisha kazi hiyo kwa kiwango na
wakati ili Watanzania wapate mbadala mwingine wa usafiri haraka.
kampuni ya M/S Johns Gram Hanssen kutoka nchini Denmark ndiyo iliyoshinda Zabuni ya ujenzi wa
kivuko baada ya kuzishida kwa vigezo kampuni zingine 11 kutoka nchi mbalimbali,
na gharama ya manunuzi ni dola za kimarekani dola 4,980,000/= sawa na Bilioni
7.91 shilingi za Tanzania .
Mwezi julai, 2012 TAMESA iliitisha mkutano wa Wadau kujadili jinsi
ya kuweza kupunguza na kisha kumaliza kabisa msongamano wa magari jijini
Dar-es-salaam, miongoni mwa wadau ni Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi
Kavu na Majini (SUMATRA) na Mamlaka ya Bandari (TPA).
Moja ya mapendekezo ilikuwa ni ujenzi wa kivuko cha abiria
kitakachotoa huduma kati ya Kigamboni na Bagamoyo, nasasa ununuzi wa kivuko
hicho umekamilika, kwa usimamizi wa TAMESA ikushirikiana kwa karibu na Wizara
ya Ujenzi.
Mkurugenzi wa TAMESA, Prof. Idrissa Mshoro amesema SUMATRA na TPA watawajibika kukagua Ubora wa kivuko mara
kitakapo kamilika katika karakana ya West Marine, nchini Bagladesh, kwakuwa
ujenzi wa kivuko hiki unafanyika nchini humo.
Balozi wa Denmark
nchini Tanzania , Johnny
Flentø, amedhibitisha ubora wa huduma za kampuni yenye dhamana ya M/S Johns
Gram Hanssen, huku akiridhia ujenzi kufanyikia Bangladesh kwakuwa watajenga haraka
na kwa bei nafuu.
Kivuko hicho cha 23 kwa Tanzania , na chenye muundo wa kisasa
zaidi kuweza kustahimili mabadiliko ya hali ya hewa, kitafungiwa vifaa vya
kisasa vya mawasiliano na usalama.
No comments:
Post a Comment