TIMU ya AS FAR Rabat
ya Morocco
itakayoikabili Azam kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho imetua nchini jana Aprili 17 saa 7.30 mchana kwa ndege ya Qatar Airways.
Kwa mujibu wa ofisa habari wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) Boniface Wambura msafara wa timu hiyo wenye watu 28 kwa ajili ya
mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili itakayochezwa Jumamosi (Aprili 20 mwaka
huu) saa 10 kamili jioni Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam umefikia hoteli ya Sapphire iliyoko maeneo
ya Kariakoo, ambayo pia walifikia timu ya BYC II kutoka Liberia walipocheza na Azam wiki mbili zilizopita.
Wakati Azam imetinga hatua hiyo baada ya kuitoa
timu ya Barrack Young Controllers II ya Liberia
kwa jumla ya mabao 2-1, AS FAR Rabat
imeingia raundi hiyo moja kwa moja kutokana na nchi hiyo kufanya vizuri kwenye
michuano ya klabu Afrika.
Timu nyingine ambazo zimeingia raundi hiyo moja
kwa moja katika Kombe la Shirikisho kama ilivyo AS FAR Rabat ni Asec Mimosas ya
Ivory Coast, Atletico Petroleos (Angola), C.S.S. (Tunisia), DC Motema Pembe
(Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), El Ahly Shandy (Sudan), Enppi (Misri),
Heartland (Nigeria), Ismaily (Misri), Lobi Stars (Nigeria), U.S.M. Alger ya
Algeria na Wydad Casablanca (Morocco).
Wambura alibainisha kuwa mwamuzi Emile Fred atakayesaidiwa na Steve
Maire, Jean Ernesta na Jean Claude Labrossa wote kutoka Shelisheli ndiye
atakayechezesha mechi hiyo. Kamishna ni Abbas Sendyowa kutoka Uganda . Waamuzi
watawasili nchini leo Aprili 18 jioni.
HAFIDH KIDO
kidojembe@gmail.com
No comments:
Post a Comment