Friday, April 19, 2013

Maalim Seif azuiwa kufanya ziara Mtwara.


Dodoma. Yametolewa malalamiko bungeni kuwa Serikali imemzuia Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad kufanya ziara mkoani Mtwara.
Madai hayo yalitolewa na Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Mohamed Habib Mnyaa wakati akiuliza swali katika kipindi cha Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu.
Mnyaa aliitaka Serikali itoe kauli yake kuhusu mawaziri ambao wamekuwa wakiruhusiwa kwenda mkoani humo bila kizuizi.
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema Serikali haikumzuia Maalim Seif, bali ilikuwa inatekeleza agizo lake la kuzuia shughuli za kisiasa mkoani humo.
“Hatukuzuia ziara yake hata kidogo, yeye aliomba kufanya ziara ya kichama na wakati huo tulikuwa tunazuia mikutano ya vyama vyote,” alisema Pinda.
Alisema shughuli hizo zilizuiliwa ili kutoa nafasi kwa Serikali kufuatilia hali iliyokuwapo mkoani humo na kuahidi kuwa baadaye mambo yataendelea kama kawaida.
Katika swali la nyongeza, Mnyaa alitaka kujua ni lini zuio hilo litamalizika ili vyama vya siasa viendelee na shughuli zake kwa kuwa vimesajiliwa kisheria.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema haitachukua muda mrefu, hali itatulia na vyama vya siasa kikiwamo CCM, CUF na vingine vitaruhusiwa. Hivi karibuni kulizuka vurugu mkoani Mtwara baada ya wananchi kupinga ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kwenda Dar es Salaam, hali ambayo Serikali iliihusisha na uchochezi wa kisiasa.
Vurugu hizo zilikwenda mbali zaidi kwa watu wa Mtwara kufanya maandamano makubwa na siku nyingine kufanya vurugu zilizoambatana na kuchomwa kwa ofisi za Serikali, Mahakama na nyumba za baadhi ya wabunge na viongozi wa mkoani Mtwara.
MWANANCHI

No comments:

Post a Comment