Sunday, April 21, 2013

Tathmini ya mechi saba ligi kuu ya Uingereza jana... BBC SWAHILI.


Patashika ya ligi kuu soka nchini England imezidi kushika kasi wakati msimu wa mwaka 2012/13 ukielekea ukingoni kwa kila timu kubakisha michezo isiyozidi mitano kumaliza ligi na bingwa kujulikana.


Jana Jumamosi nyasi za viwanja saba zilikuwa kwenye hekaheka kwa timu 14 kupambana,nyingine zikitaka kusalia ligi kuu na nyingine zikitafuta nafasi ya kushiriki mashindano makubwa ya vilabu barani ulaya msimu ujao.
Arsenal wao wameweza kuibuka na ushindi finyu wa bao moja kwa bila dhidi ya Fulham katika mchezo mkali wa watani wa jadi wa jiji la London.
Mfungaji wa bao pekee la Arsenal alikuwa ni Per Mertesacker aliyefunga bao hilo kwa kichwa. Mchezo huo ulishuhudia kadi mbili nyekundu zikitoka, Steve Sidwell wa Fulham akionyeshwa kadi nyekundu ya mapema kabisa kunako dakika ya 12 ya mchezo baada ya kumchezea rafu mbaya Mikel Arteta wa Arsenal. Sidwell amerejea kwenye mchezo wa leo akitoka kutumikia mechi tatu alizokuwa amefungiwa,Naye Olivier Giroud alizawadiwa kadi ya moja kwa moja nyekundu zikiwa zimesalia dakika mbili mchezo kumalizika kwa kumchezea rafu mbaya Stanislav Manolev. Arsenal sasa imerejea kwenye nafasi ya tatu wakiwa na pointi 63 nyuma ya Man City wenye pointi 68 kwenye nafasi ya pili.
Nao Reading baada ya kuonyesha uhai katika mchezo uliopita kwa kutoka sare na Liverpool,hii leo wamejikuta wakizidi kuchungulia shimo la kuteremka daraja la ligi baada ya kutandikwa 2-1 na Norwich katika mchezo ambao magoli mawili ya Norwich yalifungwa ndani ya dakika mbili za 50 na 52,mabao yaliyofungwa na Ryan Bennett na Elliott Bennett huku Garath McCleary akiifungia bao la kufutia machozi Reading.
QPR nao wakiwa nyumbani walijikuta wakizidi kuwa na hali mbaya na kuendelea kupoteza matumaini ya kusalia ligi kuu msimu ujao baada ya kutandikwa mabao mawili kwa sinia na Stoke City kwenye uwanja wa Loftus Road. Mabao ya Stoke City yalifungwa na Peter Crouch dakika ya 42 ya mchezo na baadaye Jonathan Walters aliyefunga kwa mkwaju wa penati baada ya Crouch kuvutwa jezi kwenye eneo la mstatili. Matokeo haya yana maanisha kuwa endapo Aston Villa itaifunga Manchester United kwenye mchezo wa jumatatu,basi QPR itakuwa imeaga rasmi ligi kuu na msimu ujao watakuwa wakishiriki ligi ya Championship nchini Uingereza,Na pia Manchester United ikipata ushindi dhidi ya Aston Villa watakuwa wamejihakikishia ubingwa wa ligi kuu msimu huu ambao utakuwa ubingwa wa 20 kwenye ligi kuu soka nchini Uingereza.
Katika mchezo mwingine, Swansea wametoka sare ya bila kufungana na Southampton huku West Brom wakitoka sare ya 1-1 na Newcastle United. Yoan Gouffran alianza kuipatia Newcastle bao la kuongoza kunako dakika ya 8 ya mchezo kabla ya Billy Jones ajaisawazishia West Brom kunako dakika ya 64.
Na mchezo wa mwisho uliwakutanisha wafua vyuma wa mashariki mwa jiji la London West Ham United maarufu kama The Hammers ambao walikuwa nyumbani kwenye uwanja wa Upton Park kuwakaribisha Wigan Athletic katika mchezo ambao ulikuwa na kila aina ya burudani ya ushindani.
Matthew Jarvis alianza kupatia West Ham bao la mapema dakika 21 baada ya mchezo kuanza,bao ambalo lilidumu hadi kipindi cha kwanza kinamalizika. Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Wigan ambao wameingia hatua ya fainali ya kombe la FA wakisubiri kucheza na Manchester City baadaye mwezi ujao,wakionekana kutaka kurudisha bao hilo,lakini vijana wa Sam Allardyce walidhibiti vyema lango lao. Dakika kumi kabla ya mchezo kumalizika nahodha wa West Ham Kevin Nolan aliwakikishia mashabiki wa The Hammers ushindi kwa kufunga bao la pili na la ushindi.
Kwa matokeo haya, West Ham sasa imefikisha pointi 42 na kushika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi na hivyo kufuta hofu ya kuteremka daraja na kuji hakikishia nafasi ya kusaka taji la ligi kuu msimu ujao wakati ambapo wanajiandaa kuanza kuutumia uwanja wao mpya uliotumika kwenye michezo ya Olympiki mwaka 2012.
ligi hiyo Itaendelea tena leo kwa Michezo mingine miwili ambapo Tottenham watakuwa nyumbani White Hart Lane kuwakaribisha Manchester City huku Liverpool wakicheza na Chelsea kwenye uwanja wa Anfield,mchezo ambao BBC Ulimwengu wa soka itakutangazia moja kwa moja kuanzia saa 12 jioni kwa saa Afrika Mashariki.
BBC SWAHILI

No comments:

Post a Comment