Friday, April 19, 2013

Habari katika Gazeti MTANZANIA yazua tafrani kwa wahariri....


Mazungumzo yangu na Kibanda

Baada ya stori ya gazeti la MTANZANIA leo, iliyotuhumu wahariri wanne na mwanasiasa mmoja kuhusu ushiriki kwenye mtandao hatari, nimefanya utafiti kujua kilichotokea, maana nimehusishwa na uchafu na ujinga usiofanana na haiba na hulka yangu. 

Nimezungumza na watu wengi kujua mwelekeo wa habari hii na hatua za kuchukua. Hatumaye, nimezungumza na Kibanda kwa simu mnamo saa 10 jioni. 

Bahati nzuri, naye alikuwa ameshazungumza na watu kadhaa, wakiwamo wahariri na viongozi wenzake wa New  Habari. Kimsingi, amekerwa na kinachotokea kwenye  vyombo vya habari kuhusu sakata la kutesana kwake. 

Kwa kifupi, anasema stori anayoiona yeye ni jinsi ambavyo Ludovick ameweza kujipenyeza na kuwazoea wahariri na wanablogu kwa sababu anazojua yeye. 

Anasema stori si kuwahusisha wahariri na ujambazi. Anasema hii ni njama ya kufunika mambo na kuwalinda wahalifu wa kweli. Akasema anadhani wametumia njama ya kugombanisha wahariri, ili kugawa vyombo vya habari katika makundi, waweze kutimiza malengo yao.

Anasema Charles Mulinda amekuwa na hisia kwa muda mrefu kwamba Ansbert Ngurumo anamchukia. Mulinda, hata alipokwenda Afrika Kusini, alimwambia Kibanda kuwa Ansbert amekuwa anampigia Bashe simu, akimtaka amfukuze kazi. Anadai pia kwamba Ansbert ndiye alimshauri Msama amfukuze kazi katika gazeti la Dira. Anadai pia kwamba mwaka 2009 Ansbert aliporejea kutoka masomoni, alikuwa anadhamiria kumfukuza kazi, kwa madai kwamba yeye (Mulinda) ni mla rushwa.

Mulinda anadai pia kwamba timu ya wahariri inayochunguza tukio la Kibanda ilipomhoji, miongoni mwa maswali aliyoulizwa ni kwamba inasemekana amekuwa akipokea rushwa kwa jina la Kibanda. Mulinda anadai kwamba mtu aliyewapa swali hilo ni Ansbert.

Inasemekana pia kwamba Ratifa alimwambia Kibanda kuwa Ansbert amemwambia Bashe kuwa yeye (Ratifa) ni shushushu.

Hivyo, watu hawa wawili walipopata taarifa za mawasiliano ya Ludovick na Ngurumo, wakaamua kumshughulikia. Kwa maneno ya Kibanda, Mulinda na Ratifa "wametumia moyo" badala ya kichwa.

Lakini anasisitiza kwamba hata kama hayo yangekuwa kweli, haikuwa sahihi kuandika stori mbaya hivi dhidi ya wahariri. Anasema kwamba wao wamefanya hivyo kama kulipa kisasi, hasa kwa kuwa Tanzania Daima lilichapisha tamko la Marando likitaja majina na simu za watu, akiwamo Denis.

KIBANDA amesikitika kwamba newsroom ya MTANZANIA imemwacha Mulinda kufanya atakavyo. "How can you have an editor who is an unguided missile?" alisema. Anasikitika kwamba yeye ambaye angeweza kudhibiti tabia hii ndiye ameumizwa, kwa hivyo hawezi kuchukua hatua.

Amesema ana uhakika Ofisi itachukua hatua mwafaka.

Tayari amezungumza na Bashe na kutaka Mulinda ahojiwe, ataje chanzo chake cha habari hiyo, ili hatua hiyo isaidie katika hatua zinazofuata, hasa kujua wanaofanya jitihada za kutumia media kuficha wahalifu.

Amesema pia ni vema wahariri wakutane haraka iwezekanavyo na kuweka msimamo kabla ya mabaya zaidi kuwakuta. 

Tayari Jukwaa la Wahariri limeitisha Kikao cha dharura kesho, Dar es Salaam.

UFAFANUZI WA BAADHI YA KAULI

Nimemjibu Kibanda ifuatavyo:

1. Sijawahi kumfukuza kazi Mulinda. Nilimlea kazini akiwa correspondent (2006), baadaye Kibanda alipokuja akamwajiri na kumpa uhariri Tanzania Daima. Niliporejea kutoka masomoni, alijiondoa mwenyewe kwa woga, akidai kwamba nilikuwa nataka kumfukuza kazi kwa rushwa.

2. Sikuwahi kumwambia Msama amfukuze kazi. Msama mwenyewe ndiye alikuja Ofisini kwangu kuomba radhi kwa niaba ya Mulinda, kuhusu stori iliyokuwa imeandikwa kwenye gazeti la Dira kuhusu Free Media kuchelewesha mishahara, ikidai Mbowe ndiye amechota pesa na kuelekea Club Bilicanas. Msama alisema anashangaa stori hiyo kwani hata yeye alikuwa hajalipa mishahara, na Mulinda hajapokea wa kwake. Akasema Mulinda amekuwa anamgombanisha na watu anaofahamiana nao. Akaazimia kwenda kumfukuza kazi.

3. Ni kweli nilimweleza Bashe kwamba Mulinda ni mlarushwa, na haandiki stori kubwa bila kupewa pesa. Nilitilia shaka mwenendo wa stori zake kupotosha suala la Kibanda. Nikamshauri Bashe stori zao wasiwe wanamwachia Mulinda na Ratifa peke yao, bali wazijadili kwenye vikao, wakubaliane. Nilisema mkimwachia aamue peke yake atawaumiza nyie na watu wengine. Ndilo limetokea!

4. Kuhusu Ratifa, sikusema ni shushushu, bali ni msiri mno. Nikasema nimeshuhudia mara kadhaa akigombezwa na Kibanda kwa kumficha mhariri chanzo cha stori. Nikamshauri kwamba katika suala tete kama hili, ni vema waandishi wote wawe wanataja vyanzo vya habari kwa wahariri na wenzao katika Chumba cha Habari, ili kudhibiti dhuluma.

5. Nilisema chanzo cha habari yao hakikuwa na nia njema,  na wao walitumia mawasiliano ya Ludovick kama kificho cha majangili ili kuwanusuru wanaotuhumiwa kushirikiana na Ludovick kwa mabaya. 

Wasiwasi wa wengi, akiwamo Kibanda, ni kwamba chanzo cha habari cha Mulinda kinaweza kuwa kinatumiwa na UWT au Polisi kuua stori HALISI. Ndiyo maana Kibanda amependekeza kwamba Mulinda ataje chanzo chake cha Habari.
Ansbert Ngurumo
Dar es Salaam
Tanzania

No comments:

Post a Comment