Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph
Warioba akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo (Jumatatu,
Aprili 29, 2013). Kulia ni Katibu wa Tume, Bw. Assaa Rashid.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba imesema imejipanga kuandaa rasimu ya
katiba itakayoweka mbele maslahi ya taifa na kuwaomba wananchi waijadili na
kutoa maoni yao
katika mabaraza ya katiba yatakayokutana kuanzia mwezi Juni mwaka huu (2013).
Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Jospeh Warioba amesema leo (Jumatatu,
Aprili 29, 2013) jijini Dar es Salaam
kuwa katika kuandaa rasimu hiyo, Tume yake haitapokea shinikizo kutoka taasisi,
asasi, makundi au vyama vya siasa.
"Tume haitengenezi katiba ya vikundi au vyama, tunaandaa
katiba ya nchi," amesema Jaji Warioba katika mkutano wake na waandishi wa
habari katika ofisi za Tume na kufafanua kuwa Tume inazingatia uzito wa hoja
zilizotolewa na wananchi na sio idadi ya watu waliotoa maoni.
Jaji Warioba amewataka wananchi kutokubali kutumiwa na makundi,
asasi, taasisi na vyama wakati wa kujadili na kutoa maoni katika mabaraza ya
katiba ya wilaya.
Mabaraza ya Wananchi wenye ulemavu
Akizungumza kuhusu ushiriki wa walemavu katika mabaraza ya katiba,
Jaji Warioba amesema Tume yake inatarajia kuunda mabaraza ya Katiba ya watu
wenye ulemavu ili kuwapa fursa walemavu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kutoa maoni yao
kuhusu rasimu ya Katiba itakayotolewa na Tume.
Hatua hii inafuatia ombi la Shirikisho la Vyama vya Watu wenye
ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) na Umoja wa Watu wenye ulemavu Zanzibar (UWAZA)
waliloliwasilisha kwa Tume.
Jaji Warioba amesema Baraza moja litaundwa Tanzania Bara na
jingine Zanzibar
na kwamba yatashirikisha wananchi kutoka ngazi ya chini ya wilaya hadi Taifa.
"Tunaelewa kuwa watu wenye ulemavu ni karibu asilimia 10 ya
watanzania wote na mchakato huu hauwezi kuwatenga katika ngazi yoyote,"
amesema Jaji Warioba na kuongeza kuwa taarifa ambazo Tume yake inazo
zinaonyesha baadhi ya watu wenye ulemavu wamependekezwa na mitaa, vijiji,
vitongoji na shehia kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya.
Chaguzi za Wajumbe Mabaraza ya Katiba ya Wilaya.
Aidha, Jaji Warioba amezungumzia mafanikio na changamoto
zilizojitokeza katika chaguzi zilizofanyika nchini kote hivi karibuni za
kuchagua Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba kuanzia ngazi ya mitaa, vijiji,
vitongoji na shehia.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, tathmini ya Tume inaonyesha kuwa kwa
kiwango kikubwa viongozi na watendaji katika ngazi za vijiji, mitaa, shehia na
kata walizingatia mwongozo uliotolewa na Tume na kuwa maeneo mengi wananchi
walichaguana kwa amani na utulivu.
"Kwa mfano jumla ya shehia 323 sawa na asilimia 96.4 kati ya
shehia 335 kwa upande wa Zanzibar zimekamilisha vizuri mchakato huu, hali
kadhalika jumla ya Kata 3,331 sawa na asilimia 99.8 kati ya Kata 3,339 kwa
Tanzania Bara nazo zimekamilisha mchakato wa kuwapata wajumbe wa Mabaraza ya
Katiba ya Wilaya kwa kuzingatia utaratibu uliotolewa kwa mujibu wa
Mwongozo," amesema Jaji Warioba.
Kuhusu hatua inayofuata baada ya chaguzi hizo, Jaji Warioba
alisema Tume inaendela kupokea majina kutoka kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa
na ya wananchi wote waliopendekezwa kutoka katika Kata na Shehia na kazi hiyo
inatarajia kukamilika ifikapo tarehe 30 Aprili mwaka huu (2013).
Changamoto
Akizungumzia kuhusu changamoto zilizojitokeza katika chaguzi hizo,
Jaji Warioba amesema kuwa pamoja na mafanikio yaliyopatikana pia kulijitokeza
changamoto kadhaa ambazo zilisabishwa na misimamo ya kisiasa na kidini
"Katika baadhi ya maeneo mikutano ya uchaguzi ngazi za
vijiji, mitaa na shehia ilishindwa kufanyika kutokana na mivutano ya kisiasa na
kidini zilizosababishwa na baadhi ya wananchi kufangamanisha chaguzi za Wajumbe
wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya na masuala ya kisiasa na kidini," amesema
Jaji Warioba.
Jaji Warioba ametaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja na baadhi
ya wananchi kujiingiza katika vitendo vya rushwa katika chaguzi hizo ili
wapendekezwe kuwa wajumbe wa mabaraza hayo ya katiba.
"Tumepokea pia malalamiko ya vitendo vya rushwa,"
alisema Mwenyekiti huyo na kusema vitendo hivyo ni kinyume cha sheria na
kuongeza kuwa taasisi zenye mamlaka ya kupambana na vitendo hivyo zinapaswa
kushughulikia malalamiko hayo.
Aina na Majukumu ya Mabaraza ya Katiba
Katika mkutano huo uliofanyika katika katika Ofisi za Tume
zilizopo mtaa wa Ohio jijini Dar es Salaam , Mwenyekiti huyo pia alizungumza
kuhusu aina na majukumu ya Mabaraza ya Katiba.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura
ya 83 imetoa fursa ya kuundwa kwa mabaraza ya aina mbili ambayo ni Mabaraza
yatakayoundwa, kusimamiwa na kuendeshwa na Tume katika muda na tarehe
itakayopangwa na Tume.
Aina ya pili, kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, ni Mabaraza ya Katiba
ya Asasi, Taasisi na Makundi mbalimbali yenye malengo yanayofanana. Mabaraza
haya yatajiunda, yatajisimamia na kujiendesha yenyewe na kisha kuwasilisha
maoni yao kuhusu
rasimu ya Katiba ndani ya muda utakaopangwa na Tume.
"Kazi kubwa ya Mabaraza ya Katiba ya aina zote mbili ni
kuipitia, kuijadili na kuitolea maoni rasimu ya Katiba itakayokuwa imeandaliwa
na Tume kutokana na maoni yaliyokusanywa kutoka kwa wananchi," alisema
Jaji Warioba na kuziomba taasisi, makundi, asasi na vyama mbalimbali kutumia
fursa hiyo ya kisheria kuunda mabaraza na kutoa maoni yao kuhusu rasimu ya
Katiba itakayotolewa.
MJENGWA BLOG
No comments:
Post a Comment