Wednesday, April 17, 2013

MJUE BIBI KIDUDE MZANZIBAR MWENYE ASILI YA MANYEMA

FATMA binti Baraka, maarufu kwa jina la Bi Kidude, ni miongoni mwa wasanii wanawake wachache ambao ni magwiji wa muziki wa taarabu nchini, ambaye kwa siku ya leo ataibeba manowari yetu ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka ifikapo Machi 8.
Bibi huyu mwenye sauti nzito na inayopenya vyema masikioni mara anapoimba, ni mzaliwa wa Zanzibar lakini asili ya kabila lake ni Mmanyema kutoka Mkoa wa Kigoma, magharibi mwa nchi.
Licha ya kuwa na umri mkubwa (113) , sauti ya Bi Kidude bado ni nzuri na yenye kuvuta hisia, hasa kwa mpenzi wa miondoko ya muziki wa mwambao.
Bi Kidude katika nyimbo zake nyingi amekuwa akiwavutia wengi kutokana na nyimbo zake kubeba ujumbe wa mahaba kama alivyoimba kwenye wimbo wake ’Ya Laiti napenda pasi kifani’ na wakati mwingine mafumbo kwa lugha ya Kiswahili yenye lengo la kufikisha ujumbe kwa watu maalumu kama alivyoimba katika wimbo wake wa ’Muhogo wa Jang’ombe’.
Hadi hapo utaona kwamba mtu mzima huyu anapaswa kupewa heshima katika siku kama hii, hasa kwa kuzingatia kwamba ni Siku ya Wanawake Duniani.
Historia na asili ya jina Kidude Fatma Baraka kwa kauli yake, anasema amezaliwa miaka 113 iliyopita huko Zanzibar ambako baba yake mzazi alilowea akitokea Kigoma (enzi za utumwa), hivyo kabila lake ni Mmanyema, tena mwenyewe anajiita ni Mmanyema asilia.
Ingawa hafahamu kijiji halisi alichozaliwa baba yake, Bi kidude anasema babu yake upande wa mama alikuwa Mngindo, wenyeji wa Kilwa.
“Mimi asili yangu ni Mmanyema wa Kigoma, baba yangu na mama yangu alikuwa Mngindo, lakini baba yangu alilowea Zanzibar, ndiyo nasisi tukazaliwa huko mpaka sasa naishi Zanzibar, lakini mie Mmanyema,” anasema Bi kidude alipozungumza na Tanzania Daima hivi karibuni.
Anasema jina la Kidude alipewa na mjomba wake wakati alipozaliwa kwa sababu alikuwa na umbile dogo. “Nimezaliwa miezi saba... njiti, nililazwa kitandani, nilikuwa mdogo, mtu hawezi kujua kama kuna kitu kimelazwa.
“Kuna mjomba wangu akaja akakaa nilipolazwa mimi, akaambiwa angalia usimkalie mtoto, akasema mtoto gani, ni kidude tu hiki, basi ndo tangu siku hiyo jina limenieleleza.
Mkongwe huyu wa taarabu nchini, ambaye kwa miaka ya hivi karibuni amejizolea umaarufu kupitia tasnia hiyo, anasema katika maisha yake hajapata kuwa na mtoto, ingawa ameweka bayana kwamba aliwahi kuolewa mara mbili.
Kwa muonekano ni kikongwe mwenye nguvu zake, anasema katika umri alionao, amepitia misukosuko ya aina tofauti za maisha. Kifupi, safari yake kimaisha ni ndefu.
Anafafanua kwamba ndoa yake ya kwanza alifunga na Ramadhani Ibrahimu, na wa pili aliitwa Juma Kombo.
“Nimeolewa vyuo viwili, cha kwanza nikaachika, nimewahi kumfumania mume wangu (nadhani anamaanisha huyo wa pili), nikampiga kwa mikia ya taa nikamwacha anachuruzika damu, nikaenda zangu na mpaka leo sijaolewa na wala sina haja ya kuwa na mume,” anasema.
“Sijisifu, ila miye mpaka kesho ukiniudhi wallahi sitafuti mtu... nitawatuma watu wakuite, ukifika mie nimeandaa fimbo yangu, nikikuchapa nayo, ikimpata mtu anasimama kama anatafuta pesa,” anasema Bi kidude na kuongeza utani, jambo linalokulazimu kuendelea kumsikiliza bila kuchoka.
Anaendelea kuwausia hususan wasichana walio katika umri wa kuolewa kwamba wanaume wa sasa hivi si wema wengi wanapenda kumkuta mwanamke ana kila kitu. “Hakuna wanaume sasa hivi, hao walikuwepo zamani, siyo leo... leo mwanaume anakufuata, umlishe, umfanyie kila kitu, waapiii! Wanaume enzi hizo,” anasisitiza Bi kidude.
Maisha yake na uimbaji Mkongwe huyu wa taarabu na muziki wa mwambao nchini anainadi siri yake katika fani kuwa ni kipaji. Katika hilo Bi Kidude anasema ameanza kuimba akiwa binti wa miaka 10, alipokuwa akitoroka kwao na kwenda nyumbani kwa marehemu Mtumwa binti Saadi, maarufu Siti binti Saad.
Kadhalika, anatanabaisha kwamba mafanikio kwa mwanamuziki bora ni yule anayetumia kichwa na dhati ya moyo wake kwenye kuimba. Anasema kubana au kuibadili sauti wakati wa kuimba si sahihi, inamtoa mwimbaji kwenye uhalisia wake.
“Mie naimba kwa kutumia kichwa, si kifua au kubana pua aaa! Sifanyi kama hao wanaojiita waimba taarabu wa siku hizi, kwanza siku hizi hakuna taarabu. Mimi nina uwezo wa kuimba bila kutumia karatasi... kwani bendi ya polisi! (kicheko kwa wanaomsikiliza).
“Enzi zetu taarabu ulikuwa mtu ukiisikiliza ufanye kazi kupata maana yake kutaka kulinda matusi na kila mmoja anaweza kuisikiliza popote. Kwanza watu walikuwa wanaanza kuimba saa nane za usiku, ikifika saa 11 unafungwa muziki. Mie nashangaa siku hizi taarabu inaanza saa mbili.
“Taarabu ya zamani mtu ulikuwa ukitisa kichwa taratibu, wanawake tulikuwa tunavaa kwa heshima, si siku hizi watu mnakatika mabuno (viuno), wanawake wanakwenda bila heshima, au kwa vile kuna matako ya Kichina?” anahoji mwanamuziki huyo huku akitoa pakiti yake ya sigara aina ya Embassy na kuvuta.
Kuhusu sigara na uimbaji, Bi kidude hakubaliani na dhana kwamba inamaliza sauti, badala yake anashuhudia kwamba ameanza kuvuta akiwa kijana lakini sauti yake haina mabadiliko.
“Nimevuta sigara mie hujazaliwa na mpaka sasa navuta sijapata TB wala ugonjwa wa mapafu, leo unaniambia mbaya! Mbona sijafa?” anahoji mkongwe huyo na kueleza kwamba alianza kuvuta sigara aina ya Seven Seven, Mkasi, Simba, Kulindondo, Gundufleki na sasa Embassy ambapo ana uwezo wa kumaliza pakiti moja kwa siku tatu.
Mbali ya kuimba, pia Bi kidude ana uwezo wa kupiga ngoma, ikiwa ni baada ya kujifunza kwenye majahazi wakati akiwa na umri mdogo alipokuwa akitoroka kwenda madrasa (chuo cha elimu ya Kiislamu).
“Nilikuwa nakimbia nyumbani, naaga naenda chuo lakini sifiki, nazuga kwa kubeba juzuu yangu kwapani lakini siendi huko, bali nakwenda kwenye majahazi kufundishwa kupiga ngoma na tumba,” anasisitiza.
Oktoba mwaka 2005 alipata Tuzo ya heshima ya msanii mwenye mafanikio makubwa iliyotolewa nchini Uingereza (tuzo ya WOMAX).
Aliyebaini kipaji chake Bi Kidude, anapasua ukweli kwamba mtu wa kwanza kuthamini kazi zake na kumtafuta hadi kufika alipo alikuwa Rais mstaafu wa Tanzania wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi.
Anasema alipokuwa Rais wa Zanzibar, aliwaomba watu wamtafute Bi Kidude ili apate kumwimbia nyimbo za Siti, kwa kuwa hakuna aliyeweza kuziba pengo japo kidogo la Siti binti Saad.
“Ali Mwinyi alikuwa akitafuta nyimbo za Siti binti Saad. Akatumwa Vuai na Khadija Baramia ambao siku nyingi hatujaonana.
“Walipotokea wakaniambia natafutwa na Ali Hassan Mwinyi, mie nikashangaa, kwa sababu nyumba zetu zilikuwa zikitizamana milango, nikaona bora niende... nikapelekwa Bwawani nikatengenezewa chumba kama kuku.
“Teena! Nikawa namwimbia Mwinyi kule Bwawani akija anaburudika... huko nikakutana na Mariam Hamdani (dada wa aliyekuwa Waziri wa Fedha, Zakhia Hamdani Meghji) alikuwa anakuja kunipiga picha anapeleka Ujerumani miye Bi Kidude sijui,” anasema.
Aidha, anafahamisha kwamba alipelekwa kwa mara ya kwanza nchini Ujerumani na Mariam Hamdani, aliyemtambulisha kwa watu mbalimbali ambapo aliweza kusimama kwenye majukwaa na kutumbuiza.
Kama hiyo haitoshi, Bi kidude anaongeza kwa kusema Mariam alimpeleka hadi kwa Malkia Elizabeth II nchini Uingereza. “Yeye ndiye alinipeleka Ulaya, sikujua Kiingereza, nikawa na mlinzi, miye nimefika hadi kwa Malkia Mtukufu Lizabet (Elizabeth)... akawa ananisalimia Shikamoo mama Kidude.
“Nimepewa cheo na Mtukufu Lizabet. Nilipofika anafunua vitabu naona sura yangu nikawa nashangaa, alinipa kidani cha dhahabu nikaamua kukiuza kulekule Uingereza, maana ningekuja nacho huku wangeniua,” anasema.
Katika hilo, Bi kidude anasema alipofika kwenye kasri la malkia alikutana na askari waliofanana na sanamu, wamevalia viatu vya chuma huku akieleza kwamba hajawahi kuliona kochi kama aliloliona huko.
“Wakati natoka kwa Mtukufu Lizabet nilijikojolea ndani ya gari kwa hofu mambo niliyoyaona makubwa,” anasema Bi Kidude ambaye ni binamu wa aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Salmin Amour.
Akiwa nje ya Tanzania, mkongwe huyo anaeleza anavyothaminiwa huku akisisitiza kwamba Mkurugenzi wa Nyumba ya Vipaji Tanzania (THT), Ruge Mutahaba, pia alimsaidia na kumfikisha alipo.
“Mimi, Ruge miye sikumjua huku, kanikuta napiga ngoma kwa Shakira, kanipenda akanichukua kaenda kunikodia hoteli alipojua naimba ndo akanikaribisha ofisini kwake, tunaongea ananihoji, kisha ananipa pesa anaondoka, mie nabaki hotelini tena.
“Siwi na shida miye, nakwenda ofisini kwa Ruge, simuombi mwenyewe ananigawia pesa, ananiuliza upo au haupo, namwambia narudi Unguja na yeye akija Unguja lazima afike nyumbani kwangu, anachukua alichonacho ananigawia, simuombi aah! Ananitumikia yeye. Hii ni mara ya pili anakuja kunichukua kwa ajili ya tamasha,” anasisitiza huku akimwomba Mungu ambariki mkurugenzi huyo.
Miongoni mwa nyimbo zinazompa umaarufu Bi kidude hadi sasa ni Muhogo wa Jang’ombe, Yalaiti, Kijiti, Arebaba na Machozi, Machozi ya huba na nyinginezo.
Anavyoijua Dar es Salaam Bi kidude anasema anaifahamu vilivyo Dar es Salaam kwa kuwa amefika hapa enzi za utawala wa Mwarabu wakati wazawa wakitoa kodi ya kichwa.
“Nchii hii kaitengeneza John Rupia miye niko hapa, mama Haambiliki alikuwa anafanya vichekesho, nimemlea miye, mama mzazi wa mwanamuziki Shakira nimemlea miye. Hao kina Mzee Yusuf nimewalea wazazi wao.
“Nimekuja hapa binti sijaolewa, nimekuja kwa madhumuni ya kuimba taarabu, nilifikia Bagamoyo, Rais Jakaya Kikwete, kazaliwa mikononi mwangu mie, nilikuwa naishi kwa Sheikh Ramia.
“Nimewahi kuishi Ajipshini (Egyptian) kwa miaka tisa,” anasisitiza gwiji huyo wa miondoko ya taarabu ambaye hivi karibuni alikonga nafsi ya Rais Kikwete na Watanzania waliohudhuria uzinduzi wa kampeni ya Mradi wa Malaria iliyokwenda kwa jina la ’Zinduka.’


Chanzo: Ukurasa wa facebook wa Damian Eligy.

Marehemu Bi Kidude akiwa katika maradhi yake, ambapo kutokana na umri wake mkubwa kila mara alikuwa akiugua na kulazwa Hospitali. Inadaiwa mwezi uliopita alilazwa Hospitali jiji Dar es Salaam na baadaye akapelekwa Zanzibar na kufariki mchana wa leo Bububu mjini Unguja.

 Bi Kidude alijitapa enzi za uhai wake kuwa alipenda kusafiri, kuvuta sigara na kunywa pombe ambapo inadaiwa baadaye aliamua kuacha kunywa.

                                            Bi Kidude akiwa jukwaani akishughulika.

 Fatma Bint Baraka alipokuwa msichana hakuwa mtu wa kujitupa, hapa akiwa kwenye vazi nadhifu.

 Joseph Haule (Profesa J) mwanamuziki wa kizazi kipya akiwa na Bi Kidude, wanamuziki wa kada zote walipenda kuimba na Bi Kidude ili kuweka historia ya sanaa zao. Kutokana na umaarufu wa bibi huyo.

 Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete akimpa Bi Kidude tuzo ya heshima ya Mwanamuziki aliyeheshimika katika muda wote nchini Tanzania, mwanzoni mwa mwaka huu jijini Dar es Salaam.

                                      Bi Kidude mpaka anazeeka bado alijipenda kwa mavazi na mapambo.

Bi Kidude akisaidiwa kushika kipaza sauti kwenye Tamasha la Muziki la sauti za Busara mjini Zanzibar.

No comments:

Post a Comment