Ugonjwa hatari unaoshambulia mahindi na kusababisha saratani kwa
binadamu umeingia nchini na wakulima sasa wametahadharishwa kutokula mahindi
hayo wala unga ambao haujakobolewa.
Mahindi yaliyoathiriwa na ugonjwa huo huota 'fungus' ambao ina
sumu inayoitwa 'Aflatoxin' ambayo inaweza kusababisha madhara kwa wanyama na
binadamu hususan ugonjwa wa saratani.
Mbali na kutikisa mikoa kadhaa na kusababisha hasara kubwa kwa
wakulima, ugonjwa huo ambao umeanzia nchini Kenya
unaendelea kusambaa kwa kasi na sasa umeingia pia nchini Uganda .
Awali ugonjwa huo uliripotiwa kuzikumba wilaya za Babati mkoani
Manyara na Meatu mkoani Shinyanga tu, lakini sasa umesambaa hadi katika mikoa
jirani ikiwamo Kilimanjaro
.
Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, Leonidas Gama jana alilithibitishia gazeti
hili kuwa mkoa wake umekumbwa na ugonjwa huo na tayari umesambaa katika wilaya
tatu; Moshi Vijijini, Siha na Hai. "Ni kweli baadhi ya wilaya zimekumbwa
na ugonjwa huo, bahati mbaya sana
hauna tiba na unasambaa kwa kasi... Wataalamu wanaendelea kuwaelimisha wakulima
kutambua dalili zake," alisema Gama.
Gama alisema endapo mkulima atabaini shamba lake kushambuliwa
na ugonjwa huo katika hatua za awali, anachotakiwa kufanya ni kung'oa mimea
yote ya mahindi na kuichoma moto.
Mkuu wa Wilaya ya Hai, Novatus Makunga alisema takriban hekari 14
zimeshambuliwa na ugonjwa huo katika shamba la Watawa wa Kanisa Katoliki
Mailisita na shamba la mkulima wa Lambo.
Alisema tayari wataalamu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya
Selian (SARI) ya Jijini Arusha wamefika wilayani humo na kutoa tahadhari kwa
wakulima juu ya athari za ugonjwa huo. Mfanyabiashara mashuhuri wa mjini Moshi,
John Bennett anayemiliki mgahawa wa Golden Shower aliitaka Serikali kutoa elimu
kwa wananchi na wafanyabiashara na kuchukua tahadhari.
"Utajuaje unga wa dona haukutokana na hayo mahindi au pumba
ya chakula cha mifugo hayakutokana na hayo? Hili jambo ni zito sana si la kufanyia utani hata
kidogo"alisema Bennett.
Mkulima wa Kijiji cha Kikavu Chini wilayani Hai, Justine Mvungi
alisema wataalamu kutoka SARI wamewataka kuchoma moto miche ya mahindi ambayo
watagundua imeshambuliwa.
"Wametuambia takriban shamba likishambuliwa, tung'oe mahindi
hayo na kuyachoma moto, wametuambia kama
tulishavuna basi tukoboe mahindi hayo maana kiini chake kina madhara,"alisema.
"Aliongeza kusema" hata tukikoboa mahindi tumeambiwa
zile pumba zake tusiipe mifugo kwa sababu itaathirika... Ugonjwa huu wa mmea wa
mahindi umeleta taharuki kubwa kwa wakulima na wananchi.
"CHANZO MWANANCHI
No comments:
Post a Comment