ALIYEKUWA mgombea nafasi ya uenyekiti katika uchaguzi mkuu wa
Chama cha Netiboli Tanzania
(CHANETA), Shyrose Bhanji, amempongeza Anna Kibira kwa ushindi katika nafasi
hiyo nyeti katika kupigania mafanikio ya mchezo huo.
Pongezi hizo zilitolewa juzi usiku ikiwa ni saa chache baada ya
kwisha kwa uchaguzi huo, ambapo kwa nafasi ya uenyekiti, Kibira aliyewahi kuwa
katibu mkuu wa chama hicho katika uongozi uliomaliza muda wake, alishinda kwa
kura 61 dhidi ya 21 za Shyrose.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Kigali, Rwanda, anakoshiriki
kikao cha Bunge la Afrika Mashariki, Shyrose alisema amefarijika chama hicho
kufanya uchaguzi na anautakia heri na mafanikio uongozi mpya.
“Nampongeza dada Kibira (Anna) kwa ushindi na ninamtakia mafanikio
yeye na uongozi wake katika kupigania mafanikio ya mchezo wa netiboli, naamini
ushindi wake ni ushindi wa mchezo huo,” alisema.
Alisema kutokana na upenzi wake katika michezo, pamoja na
kutoshinda kwa nafasi hiyo, atakuwa tayari kushirikiana na uongozi mpya katika
kuendeleza harakati za kupigania mafanikio ya mchezo huo kwa maslahi ya vijana
na taifa.
“Kwa upande wangu naahidi jambo moja kwamba niko tayari kusaidiana
na uongozi mpya kama utahitaji kwa maslahi ya
mchezo wa netiboli, nikiamini michezo sasa si burudani na afya tu, pia ni ajira
kwa vijana wenye vipaji,” alisema Shyrose aliyekuwa makamu mwenyekiti katika
uongozi uliopita chini ya Anna Bayi.
Wengine waliochaguliwa juzi ni Zainab Mbiro Makamu Mwenyekiti,
Agness Hatib Mweka Hazina huku wajumbe wa Kamati ya Utendaji ni Yasinta
Silvester, Fortunata Kabeja, Asha Sapi, Penina Igwe, Hilda Mwakatobe na Judith
Ilunda.
No comments:
Post a Comment