Friday, April 26, 2013

Tuulinde muungano bila kujali itikadi zetu.


LEO Muungano wetu kati ya Tanganyika na Zanzibar umetimiza miaka 49, tangu ulipoasisiwa mnamo Aprili 26, mwaka 1964. Watanzania wamehimizwa kujitokeza Uwanja wa Taifa, ambapo wataungana na viongozi mbalimbali, akiwamo Rais Jakaya Kikwete kuadhimisha sherehe hizo muhimu.

Wananchi wote bila kujali itikadi zetu za kisiasa, kabila, dini au maeneo tunayotoka, tunapaswa kuulinda na kuuheshimu Muungano wetu uliodumu na kufikisha umri huu.

Kwa kufanya hivyo pia tutakuwa tunatekeleza kauli mbiu ya mwaka huu inayosema: “Amani, utulivu na maendeleo ni matokeo ya Muungano wetu, tuuenzi na kuulinda”.

Muungano huu ni matokeo ya kazi nzuri iliyofanywa na waasisi wa taifa hili la Tanzania, ambao waliweka mbele zaidi faida za kuungana kuliko kujitenga kila mtu akaishi kivyake.

Katika kufanikisha Muungano huu, hayati Mwalimu Julius Nyerere aliwakilisha Tanganyika na hayati, Sheikh Abeid Amani Karume aliwakilisha Zanzibar.

Katika mazingira ya sasa kuungana ni bora zaidi kuliko kufarakana, kwani wakati mataifa makubwa duniani yanaungana, itakuwa vichekesho mataifa ya dunia ya tatu yakakataa kuungana.

Hata hivyo wakati Muungano wetu unatimiza umri wa miaka 49 leo, ni ukweli usiopingika kuwa Muungano wetu bado unakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Tunapenda kutumia fursa hii kuisihi Serikali kumaliza kero zote zinazoelezwa na wananchi, vinginevyo Serikali italazimika kutumia mtutu wa bunduki kuuhami Muungano.

Moja ya mambo yanayolalamikiwa ni kwamba, masuala yanayohusu Muungano yameongezwa kinyemela na kufikia 22 sasa tofauti na masuala 5 tu yaliyoainishwa katika hati ya Muungano (Article of Union).

Baadhi ya wananchi hususan Wazanzibari, wamekuwa wakilalamikia ongezeko hilo wakisema kuwa hatua hiyo imelenga kuibana Serikali yao ya SMZ.

Suala la kufaidika na rasilimali za nchi na mgao wa mapato kati ya Serikali ya SMZ na Serikali ya SMT ni miongoni mwa mambo yanayoleta ukakasi wa Muungano.

Tunatambua jitihada zinazofanywa na Serikali katika kutatua kero zinazoukabili Muungano, lakini inapaswa kuongeza kasi katika kushughulikia kero hizo ili kuudumisha.

Kupiga kelele na kutoa matamko ya vitisho dhidi ya watu wanaohoji Muungano na wale wasioutaka bila kumaliza kero hizo ni kuzima moto kwa majivu, utatuunguza.
 Amiri jeshi mkuu na Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete akiwa na mkuu wa jeshi la wananchi Generali Mwamunyange uwanja wa Uhuru leo kusherehekea miaka 49 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

 Gwaride la heshima likipita mbele ya viongozi wa Tanzania atika viwanja vya Uhuru jijini Dar es Salaam leo kuadhimisha Muungano wa nchi mbili Tanganyika na Zanzibar.



Ndege za kivita zikipita katika anga la Uwanja wa Uhuru kuonyesha uwezo wa kijeshi kwa watanzania leo.

MJENGWA BLOG

No comments:

Post a Comment