Mh Mizengo Kayanza Peter Pinda.
Mh Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania Mh Mizengo
Kayanza Peter Pinda, naomba leo nizungumze na wewe kwa kutumia karamu na
karatasi kuweza kufikisha kwako matatizo ya wanafunzi wa kitanzania wanaosoma
nchini URUSI.
Mh Waziri Mkuu mimi ni miongoni mwa wanafunzi ninaosoma nchi
Urusi , kutokana na matatizo mbalimbali yanayotukabili wanafunzi wa kitanzania
hapa URUSI , nimeona nitumie karamu na karatasi kuweza kufikisha matatizo haya
kwako.
- MKOPO TUNAOPEWA
HAUTUTOSHI KWASASA.
Mh waziri Mkuu, Mkopo tunaopewa kwa mwaka na serikali kupitia bodi
ya mikopo ya elimu ya juu haitutoshelezi kulingana na gharama za maisha
zilizopo kwa sasa huku Urusi.Tumeandika barua nyingi za kuomba kuongezewa
angalau mkopo kwenda Bodi ya mikipo na wizara ya Elimu ya ufundi na mafunzo
stadi na barua zetu kupitia Ubalozi wa Tanzania hapa Urusi toka mwaka 2009
mpaka 2012 lakini tumekuwa hatupatiwi majibu. Mheshimiwa kiukweli hali ya
maisha imepanda sana hapa Urusi zaidi ilivyopanda huko nyumbani, kwani ada ya
hostel mwaka 2008/9 ilikua dolar za kimarekani 660 kwasasa tunalipa dolar za
kimarekani kati ya 1000 hadi 1200 kulingana na rate exchange ya siku utakayo
lipia. Hili ni ongezeko la karibu asilimia 100% ukilinganisha na mwaka 2008.
Mheshimiwa Waziri Mkuu kila kitu kipo juu huku mfano vyakula, usafiri , bima ya
afya, stationaries(vitabu,karamu,madaftari na vifaa vingine ). Mheshimiwa
Waziri Mkuu mkopo tunaopatiwa tunatakiwa tulipe hostel, chakula, usafiri,
stationaries, facaulty requirement na mengineyo. Mheshimiwa Waziri Mkuu ukiwa
kama mtendaji mkuu wa Serikali nakuomba uangalie upya mkopo tunaopatiwa
wanafunzi wa Urusi na mwaka huu wa fedha wa 2013/14 angalau na sisi serikali
iweze kutukumbuka kwa kutuongezea mkopo japo kidogo ili tuweze kukabiliana na
ugumu wa maisha tunaopata huku.
Naimani Mheshimiwa utarifanyia kazi swala hili kwakua wewe ni
mzazi na ni kiongozi usie bagua.
2.UCHELEWESHWAJI WA ULIPAJI WA ADA VYUONI.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, serikali kupitia bodi ya mikopo imekua ikichelewa
kulipa ada za wanafunzi katika vyuo mbalimbali hapa Urusi mpaka kupelekea
usumbufu kwa wanafunzi kuzuiliwa kuingia madarasani hata kufanya mitihani, hili
tatizo limekua likitokea kila mwaka na bodi ya mikopo imekua haionyeshi kama ipo tayari kulimaliza tatizo hili. Mheshimiwa Waziri
Mkuu tatizo hili limekua likiitia serikali yetu aibu vyuoni kwani imefikia
hatua vyuo husika havimsikilizi Balozi wetu Mh Jaka Mwambi anapokwenda vyuoni
kuomba muda wa kulipa ada na wanafunzi wasiweze kusumbuliwa madarasani.
Ninaamini kabisa kupitia ofisi yako hili tatizo la ucheleweshwaji wa malipo ya
ada unaweza kulitatua na kulimaliza kabisa kwani ni kero sana kwetu wanafunzi hapa Urusi nadhani hata
Kwa Maofisa wa Ubalozi Nchini Urusi.
3.UCHELEWESHWAJI WA MIKOPO KWA WANAFUNZI NA MAKATO YASIYO YA
LAZIMA.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, bodi ya mikopo kila mwaka imekua
ikitucheleweshea mikopo yetu bila sababu za msingi, hauwezi amini mpaka leo hii
kuna baadhi ya wanafunzi hajapatiwa mikopo yao na wakijaribu kuwasiliana na
wahusika wa bodi hakuna majibu wanayopatiwa zaidi wanadanganywa na kutopokelewa
simu zao, hawa watendaji wa bodi wanasahau kuwa sisi huku tupo ugenini hatuna
baba, mama ,shangazi wala mjomba na wazazi wetu huku ni pesa tu maana bila pesa
huku maisha ni magumu sana na watu tunapata stress za ajabu sana.
Nakuomba Mheshimiwa Waziri Mkuu uweze kuiagiza bodi ya mikopo iwalipe wanafunzi
wote ambao bado hawajapatiwa mikopo yao
ya mwaka wa masomo wa 2012/13 kwani ndugu zetu wanateseka bila sababu za
msingi. Pia Mheshimiwa naomba bodi ya mikopo iwe inatupatia mikopo mapema kwani
muhula wa masomo huku ni tofauti na nyumbani(Tanzania) kwani huku kila tarehe 1
ya mwezi septemba kila mwaka vyuo vyote hufunguliwa na wanafunzi wanaanza
kusoma siku hiyohiyo ,sasa bodi kuchelewesha mikopo hata kwa wiki moja
inatufanya tuanze semista tukiwa na msongo wa mawazo. Naimani tatizo hili
utalishugulikia ili kutuondolea usumbufu usio wa lazima.
4.ULIPAJI WA BIMA YA AFYA KWA BAADHI YA WANAFUNZI.
Mheshimiwa waziri mkuu, kumekua na mtindo kwa bodi ya mkopo
kutotupatia pesa ya bima ya afya kwa wanafunzi au kuwapatia baadhi pesa hizo na
wengine tukikosa pesa hizo, hili ni tatizo kwani inapelekea mwanafunzi kuchukua
pesa ileile ya matumizi ambayo tunalalamika haitoshi na kulipia bima ya afya, mfano
mwaka wa masomo wa 2012/13 bodi iliwapatia baadhi ya wanafunzi pesa za bima ya
afya na wengine kutopatiwa mpaka leo, inapelekea hisia mbaya miongoni mwetu juu
ya watendaji wa bodi ya mikopo kuwa wanakula pesa zetu, maana haiwezekani nusu
ya wanafunzi wapatiwe pesa ya bima ya afya wengine wasipatiwe. Naomba
Mheshimiwa uliangalie hili tatizo na ulikomeshe maana linatufanya tuone watu
wachache wanakula haki yetu. Pesa ya bima ya afya ni muhimu sana huku Urusi kwani bila bima ya afya
huwezi kupatiwa matibabu hospitali yoyote ile.
5.OMBI LA KUPEWA PESA ZA KIJIKIMU KWA WANAFUNZI WANAOFANYA VIZURI
NA KUPATA SCHOLARSHIP ZA SERIKALI YA URUSI.
Mheshimiwa Waziri Mkuu tunaomba serikali yako iangalie upya swala
la kuwapatia mikopo ya pesa ya kujikimu tu kwa wale wanafunzi wanaokuwa
wamefanya vizuri katika masomo yao mpaka kupelekea serikali ya URUSI kupitia
vyuo husika kuwapatia scholarship ya Masters, kwani wanafunzi wengi huwa
wanapata hizo scholarship lakini wanashindwa kusoma na kuamua kurudi nyumbani
kutokana na kukosa pesa za kula, maana serikali ya Urusi hutoa ada na hostel
tu. Hivyo naomba serikali kupitia wewe kama
mtendaji mkuu wa serikali uliangalie hili swala kwani lina manufaa kwa Taifa na
linaipunguzia serikali gharama ya kusomesha wataalamu nje ya nchi. Kwa
kuwakopesha wanafunzi wanaofanya vizuri na kupatiwa scholarship na serikali ya
urusi, itaamsha molari miongoni mwa wanafunzi tunaosoma huku ili tufanye vizuri
na tuendelee kupata ujuzi mbalimbali huku kwa ajiri ya maendeleo ya taifa letu.
Naimani Mheshimiwa Waziri Mkuu utalifanyia kazi swala hili kwani lina faida kwa
Taifa.
6.TUNAOMBA NYONGEZA YA NAULI KWA WANAFUNZI WANAHITIMU MASOMO YAO URUSI.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, karibu kila mwaka wanafunzi wa kitanzania
wanahitimu masomo yao katika vyuo mbalimbali Nchini Urusi na inatakiwa warudi
nyumbani kujenga na kuitumikia nchi yetu kwa kurudisha fadhira kwa serikali na
watanzania kwa ujumla, Hivyo naomba serikali kupitia bodi ya mikopo kuangalia
upya kiwango cha pesa ya nauli na mizigo inayotolewa kwa mwanafunzi anapohitimu
kwani ni kidogo ukilinganisha na vitu alivyonavyo mwanafunzi aliyekaa karibu
miaka sita (6) huku Urusi. Pia kuna wakati wanafunzi wanalazimika kuacha baadhi
ya vitu vyao kwa kushindwa kusafirisha kutokana na ukata unaowakabili. Kwakua
naamini serikali yako ni sikivu hivyo swala hili utalifanyia kazi mapema.
Mheshimiwa Waziri Mkuu naimani waraka huu utakufikia popote pale
ulipo, Pia nichukue fursa hi kukutakia majukumu mema ya kitaifa uliyonayo hasa
katika kipindi hiki kigumu cha Bunge la bajeti ya 2013/2014.
Wako katika ujenzi wa Taifa
Mwanafunzi wa kitanzania nchini Urusi.
No comments:
Post a Comment