Wednesday, April 17, 2013

"MIONGOZO MIWILI, KUPAA NA KUTUNGULIWA KWA AZIMIO LA ARUSHA"

 Aliyekuwa msaidizi wa Rais wa kwanza wa Tanzania Julius Nyerere, mzee Joseph Butiku (Kushoto) akisalimiana na Jaji mkuu wa Kenya Dk Willy Mutunga wakati wa tamasha la tano la kigoda cha taaluma cha Mwalimu Nyerere katika chuo kikuu cha Dar es Salaam kwenye ukumbi wa Nkrumah wiki iliyopita.
 Dk Willy Mutunga jaji mkuu wa kenya akichagua vitabu vya kuchukua ili kuweka kwenye maktaba yake, huku Nyagoda Profesa Issa Shivji akishuhudia na pe,beni ni Rais wa majaji wastaafu Jaji Thomas Mihayo.

 Kingunge Ngombare akifurahia jambo wakati wa tamasha la tano la kigoda cha taaluma cha Mwalimu Nyerere ukumbi wa Nkrumah chuo kikuu cha Dar es Salaam, wiki iliyopita.

Hiki ni kikundi cha Maprofesa watupu wakiteta jambo kabla ya Tamasha kuanza katika siku ya pili ambapo Profesa Gosh (Mwenye nguo nyekundu) alitoa hotuba nzuri kuhusu kilimo, chakula na ardhi.
Na Hafidh Kido

Ujenzi wa Ujamaa si lelemama bali ni Mapambano, Mapambano ya kudumu dhidi ya upebari na unyonyaji, dhidi ya wapinga maendeleo na wababaishaji wa kisiasa, dhidi ya wahujumu uchumi, majambazi, wezi, wazururaji na wazembe.

Leo upebari una vishawishi vingi zaidi nchini kuliko ulivyokuwa kabla ya Azimio la Arusha kwa sababu pamoja na kwamba sasa tuna sekta kubwa ya umma lakini kutokana na udhaifu wa kutopambana nao, ubepari umefaulu kujipanua na kujipenyeza hata ndani ya sekta yenyewe ya umma.

Na ndiyo maana ubepari sasa unathubutu kujitokeza hadharani kuukashifu ujamaa, kubabaisha baadhi ya viongozi na kututaka tubadilishe siasa zetu.

Haya ni baadhi ya maneno kuntu yaliyo katika kitabu cha ‘Miongozo miwili, Kupaa na Kutunguliwa kwa Azimio la Arusha’ Ukurasa wa 138 - 139.

Kitabu hicho kimeandaliwa na Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere juu ya umajumui wa Afrika cha Chuo Kikuu cha Dar es salaam na maandishi yamekusanywa na Dr. Bashiru Ally, Profesa Saida Yahya- Othman na Nyagoda Issa G. Shivji.

Kitabu hiki kimezinduliwa siku ya Kilele cha Tamasha la Tano la Kitaaluma la Mwalimu Nyerere, Ijumaa Aprili 12 na Jaji Mkuu wa Kenya, Dk. Willy Mutunga.

Siku ya kwanza

Ilikuwa ni fahari kubwa kumsikiliza Profesa wa Kigoda cha mwaka huu Prof. Thandika Mkandawire, kutoka Malawi ambaye alijadili kuhusiana na tafakuri ya miaka 50 ya uhuru wa Afrika katika ukumbi wa Nkrumah chuo kikuu cha Dar es Salaam.

Profesa Mkandawire ambaye alipata misukosuko sana kutoka katika utawala wa Rais Kamuzu Banda wa Malawi, kutokana na misimamo yake mikali ya kutaka mabadiliko katika nchi yake aliwataka viongozi wa Afrika wakati wanatafakari miaka 50 ya uhuru wa Afrika kuacha kukimbia kivuli cha wasomi.

Aliongeza kuwa wasomi wana mchango mkubwa kwenye maendeleo ya bara letu lakini wanapata misukosuko mingi ikiwemo kufukuzwa kwenye nchi zao au kuwekwa gerezani, hivyo kuwaasa viongozi kuacha kuukimbia ukweli.

Hata hivyo, mjadala ulipopamba moto wasomi nao wakageukiwa; naam wapo wasomi ambao wamenyamazishwa kwa kupewa kitu kidogo. Hili lilionekana kumkera sana Profesa Mkandawire, kwani alionyesha masikitiko sana kwa wasomi wenzie ambao wananunuliwa na viongozi ili waache kukosoa na badala yake wasifie.

Wanataaluma waliafikiana kitu kimoja ambacho naamini kikifanikiwa basi bara la Afrika litajikomboa; Profesa Mkandawire aliwataka wasomi wenzie kukaa pamoja ili kujadili na kufikiria namna ya kutatua matatizo ya jamii zao, bila ya kusubiri misaada ya wahisani ambayo mingi inakuja na masharti magumu yenye lengo la kibeberu.

Siku ya pili

Siku hii kulijadiliwa tatizo la ardhi na chakula katika nchi za kiafrika. Mtoa mada Profesa Jayati Gosh kutoka chuo kikuu cha Nehru nchini India, alielezea kwa ufundi mkubwa namna bara la Afrika litakavyopambana na mataifa makubwa ili kulinda ardhi yao isiingizwe sokoni.

Kikubwa alichozungumza ilikuwa ni kupinga kugeuza chakula na ardhi kuwa bidhaa, bali viwe urithi kwa mataifa ya Afrika. Alielezea kuhusu kusoma alama za nyakati katika masuala ya biashara kubwa na namna ya kupambana katika biashara hizo.

Profesa Gosh alisema ni aibu kubwa kuona bara kama Asia na Afrika wanaagiza chakula kutoka nchi za magharibi.

Kwa upande wake Waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya watu profesa Anna Tibaijuka alisema “Maendeleo ya kilimo yanaanza na makazi bora, maana ikiwa wananchi hawana pa kukaa usifikiri watapata muda wa kufikiria kilimo na wasipolima usitegemee nchi itakuwa na chakula cha kutosha.”

Falsafa yake ililenga watanzania na waafrika kwa ujumla kuthamini ardhi yao na kuona ni tunu kubwa kupata ardhi kubwa na yenye rutuba. Profesa Tibaijuka aliongeza “Ardhi na chakula si bidhaa bali ni mfumo wa maisha ya kiafrika, lakini ninashangaa sana kuona hatuwezi kuendeleza kilimo kwa manufaa ya bara letu.”

Asilimia 30 ya chakula kinachozalishwa Afrika kinapotea kabla ya kuwafikia walaji, na hii inasababishwa na kutofuata mavuno ya kisasa, usafirishaji na uhifadhi mbaya. Kwa Tanzania asilimia 35 ya chakula kinapotea kwa mtindo huo.

Hata hivyo Profesa Tibaijuka alitoa wazo zuri sana ambalo wanakigoda walionekana kutikisa vichwa vyao ishara ya kukubali. Alitaka kukuza teknolijia ya kilimo. Haiwezekani Afrika kuagiza chakula kutoka mataifa ya Ulaya yenye uhaba wa ardhi. Lazima tuache kuimba kilimo kwanza bali tufikirie kukuza teknolijia ya kilimo kwa maendeleo yetu.

Kwa mujibu wa profesa Tibaijuka asilimia 70 ya ardhi ipo vijijini, lakini sera ya kilimo kwanza haijafanya kitu kuhakikisha wanatoa elimu kwa watu wa vijijini ili wapate pembejeo za kilimo zinazoendana na karne hii ya sayansi na teknolijia.

Naye Profesa Samir Amin kutoka Misri ambaye alikuwa Profesa wa kigoda katika tamasha la mwaka 2010, alishikilia msimamo wa kuhakikisha hatugeuzi ardhi zetu kuwa bidhaa bali tuhakikishe zinatukomboa. Na hata tukiita wawekezaji tuingie mikataba ambayo itatunufaisha na si kugeuka janga kwa kizazi kinachokuja.

“Ardhi ni utambulisho wa taifa, kuiuza ardhi ni kuuza taifa kidogokidogo. Na ndiyo maana nashikilia msimamo wangu kuwa ardhi iwe mikononi mwa wananchi na isiwe mali ya Serikali,” alisema Profesa Amir.     

Kwa upande wake Profesa Ibrahim Lipumba aliyebobea katika uchumi alitoa muhtasari namna nchi nyingine zilivyofanikiwa kwa kuelekeza nguvu zao katika kilimo cha biashara.

Alitolea mfano nchi za China, Taiwan na Indonesia namna walivyopiga hatua kutokana na kilimo. Mada yake ililenga kuzifungua macho nchi za kiafrika kuacha kuagiza chakula nje bali kutafuta njia za kujikomboa katika kilimo kwa kuongeza bajeti za Wizara husika ili kutoa elimu na mikopo kwa wakulima wadogo ambao kwa kiasi kikubwa ndiwo wanaolilisha taifa.

Siku ya tatu

Siku hii ambayo ilikuwa ya kuhitimisha tamasha kulikuwa na mjadala mpana uliosimamiwa na mwanahabari wa siku nyingi Jenerali Ulimwengu, ambapo vijana wawili Rehema Tukai na Zitto Kabwe walitoa mada zilizoibua mawazo mapya kuhusiana na Azimio la Arusha.

Mada ilikuwa ni ‘Dira ya Maendeleo: Azimio la Arusha Vs Dira 2025.’ Lengo la mada hii ilikuwa ni kupambanisha Azimio la Arusha la mwaka 1967 dhidi ya Dira ya maendeleo ya Taifa iliyowekwa mwaka 1999 na kuhakikisha mpaka kufikia mwaka 2025 Tanzania iwe imepiga hatua kubwa katika maendeleo ya kiuchumi.

Kwa upande wake Rehema Tukai mwanaharakati wa masuala ya kijamii, alilizungumzia Azimio la Arusha kama Dira ya maendeleo kwa bara zima la Afrika. Kwa ushujaa kabisa alisema anashangaa kwanini viongozi wa Tanzania waliamua kulitupa Azimio la Arusha kwani lililenga kumkomboa mwafrika kutoka makucha ya ubepari uliokomaa.

Alisema msimamo sahihi wa mapambano unaotokana na nadharia sahihi ya ujamaa ungetuepusha na maamuzi na vitendo ambavyo vimerahisisha kuoteshwa kwa mizizi ya ubepari, kinyume cha msimamo wa mapambano dhidi ya ubepari.

Zitto Kabwe ambaye ni mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chadema, alisema Azimio la Arusha lilijibu changamoto za miaka ya mwanzo ya uhuru ambapo viongozi wengi walijisahau wakatumia vibaya madaraka waliyoyapata. Azimio lilikuja kuziba ombwe la uongozi kwa wakati huo.

Hata hivyo alisikitika kuwa Azimio limekosa mtu wa kulisimamia baada ya Mwalimu Nyerere kung’atuka mwaka 1984, “Azimio lilikuwa na bahati ya mtu wa kulibeba, kulitetea na kulisimamia bila aibu,” alisema Zitto.

Alipolinganisha Azimio la Arusha na Dira ya maendeleo ya mwaka 2025 Zitto alisema ni watu wachache sana wanaojua kama kuna Dira ya maendeleo nchini. Na hata utekelezaji wake ni wa kimya kimya kwani mpango wa kwanza wa Dira hiyo ulipitishwa mwaka 2011 ambapo ni mwongo mmoja tangu Dira itengenezwe.

“Huwezi kulinganisha dira ya maendeleo 2025 na Azimio la Arusha, lile lilikuwa ni Azimio la misingi ya utu, tazama Dira inajali uchumi tu bila kuangalia njia za kufikia huko, lakini Azimio limegusa kila sehemu, uchumi vijijini na taifa kuacha utegemezi.

“Kitu kingine Dira inalenga kuendeleza viwanda lakini taarifa ya uchumi inasema uchumi wa nchi umekua kwa asilimia saba kwa mwaka 2000 na 2010, viwanda vimekua kwa silimia nane lakini pato la mwananchi limekua kwa asilimia tano.

“Dira inalenga sehemu ambazo mwananchi wa vijijini ambaye ni maskini hawezi kugusa, lakini Azimio liliamini kuwa ni ujinga kufikiria fedha ni msingi wa maendeleo,” Zitto Kabwe.

Aidha mwanasiasa mkongwe nchini Kingunge Ngombare Mwiru, alipopata nafasi ya kuzungumzia Azimio la Arusha alisema, “Azimio lilikuwa na sehemu mbili sehemu ya kwanza ilihusu sera (ujamaa na kujitegemea) na sehemu ya pili ilihusu miiko ya uongozi.

“Mwalimu alipounda sera za ujamaa na kujitegemea alifikiria kupeleka maendeleo vijijini akiamini asilimia kubwa ya wananchi wa Tanzania walikuwa ni wakulima na wafanyakazi. Na kuhusu miiko ya uongozi alijua viongozi ndiwo watakaotekeleza sera zile ili kuleta maendeleo hivyo ili wasiwe wanyonyaji ni lazima wawekewe masharti na mtu akiona hawezi akae pembeni.

“Lakini kuna makosa tuliyafanya katika kutafsiri miiko ya uongozi, wakati tunaunganisha vyama vya ASP na TANU kulikuwa na wajumbe 10 kutoka bara na 10 kutoka visiwani ili kuunda katiba moja ya chama. Makosa yaliyofanyika yalikuwa ni ya kishabiki kwani sisi wa bara tulikuwa na shauku kubwa ya ujamaa na miiko ya uongozi, tukaamua ile miiko tuiingize kwenye katiba ya chama na kutamka kuwa mtu akitaka kuwa mwanachama lazima afuate miiko ile.

“Nasema ni ushabiki tu ndiwo ulituponza, maana wakati ule Mwalimu (Nyerere) alipostaafu alipewa mali nyingi sana na wananchi kama shukurani, siku moja tulipokuwa Dodoma alituita mimi na Rais Ali Mwinyi akatuuliza hivi mimi nafaa kuwa mwanachama halali wa CCM, maana nina mali nyingi sana nimepewa na wananchi.

“Swali lake lilikuwa na maana kubwa alituambia kijanja kuwa tulikosea kuweka miiko ya uongozi kwa wanachama, maana wapo wanachama ambao si viongozi wala si wakulima lakini ni wafanyabiashara je hawafai kuwa wana-CCM,” alihoji Kingunge.

Naye Jenerali Ulimwengu alipozungumzia Dira ya maendeleo 2025 alisema “Nilikuwepo wakati wa uzinduzi wa Dira ya 2025 kule Arusha, kitu kilichonishangaza hakukuwepo na Waziri yeyote wa Serikali isipokuwa Waziri wa Mipango wa wakati ule, mbali ya Rais Mkapa ambaye alikuja pale kama Rais wa nchi lakini hakukuwepo na mwanachama mwingine wa CCM ingawa kulikuwepo na viongozi wa vyama vyote ya siasa (upinzani).

“Hili lilinishangaza sana ina maana chama cha Mapinduzi walisusia dira hii ama waliona kulikuwa na makosa,” alihoji Jenerali.

Jenerali aliwaasa watanzania kuacha kuamini kuwa dola halina kazi ya kufanya katika maendeleo bali mamlaka ya kuongeza uchumi lazima yaanzie ngazi za juu. Kuamini dola liache kusimamia njia za uchumi ni sawa na kisa cha kuku na mwewe, pale mwewe alipomwambia mama kuku awaache vifaranga wake watembee peke yao ili wapate afya, hupasi kumlaumu mwewe kwa kutoa ushauri mbaya bali mlaumu mama kuku kwa kukubali ushauri wa kijinga.

Awali Jaji mkuu wa Kenya Dk Willy Mutunga alipokuwa akifungua siku ya tatu ya tamasha alisema alijiunga na chuo kikuu cha Dar es Salaam kwa masomo ya shahada ya kwanza ya sheria miezi 15 baada ya Azimio la Arusha.

Katika mambo mengi ambayo yalimvutia kuhusu Mwalimu Nyerere ni namna alivyohubiri usawa kwa binaadamu. “Usawa aliozungumzia Nyerere kuhusiana na binaadamu ni usawa uliohusiana na haki na si haki ya kisheria tu bali ni haki ya kijamii.

“Binafsi nilipigania haki kwa miaka 40 nchini kwangu ili kuhakikisha Kenya tunapata katiba mpya itakayojali utu na usawa wa kibinaadamu, hatimaye katiba imepatikana na imekuwa sababu ya mimi kuwa Jaji mkuu wa kwanza aliepatikana upitia katiba hiyo,” alisema Dk Mutunga.

Kitu kilichowafurahisha wanakigoda ni pale Dk. Mutunga aliposema ana virusi vya Azimio la Arusha na anajisikia fahari kugundua virusi hivyo vinamuandama hata baada ya kuondoka Tanzania miaka mingi iliyopita.

“Virusi vya Azimio la Arusha bado vinaniandama, mimi ni Mnyerere damu kule kwetu Kenya ndivyo tunavyoita unapomkubali mtu, najisikia raha sana kusema ni muathirika wa Azimio la Arusha.

“Nyerere alikuwa ni mtu shujaa sana maendeleo ya Afrika yalipata mtetezi, maana alikuwa na jeuri ya kiafrika. Tungekuwa na viongozi aina ya Nyerere hali ya bara letu ingekuwa tofauti kwa sasa. Lakini hatuna cha kupoteza, tuhakikishe tunamuenzi Nyerere kwa kuambukizana virusi vya Azimio la Arusha virusi hivi vitatusaidia kutukinga na ubeberu,” Dk. Mutunga.

Nyagoda Issa Shivji ambaye anamaliza muda wake wa miaka mitano mwezi wa nane mwaka huu, aliwaaga wanakigoda kwa kuwaambia wanatakiwa kushukuru sana kwa kupata wasaa wa kukaa na kujadili maendeleo, kwani ni wakati muafaka sana ambao nchi nyingine wanatamani kuzipata lakini hawapati. Profesa Shivji alitoa neno la kuwafikirisha wanakidoda pale aliposema Mwalimu Nyerere aliwahi kuulizwa kiongozi ni nani akajibu “Kiongozi ni yule anayekataa kuwa kiongozi, je viongozi wetu wanayo sifa hiyo,” alihoji.

Matamasha namna hii yakifanyika matatu kila mwaka lazima vijana wa kitanzania watabadili fikra zao na kurudi katika mapambano. Maana maneno yaliyopamba tamasha la mwaka huu yalisema ‘Maendeleo ni Mapambano.’

Na Zitto Kabwe alihitimisha mjadala kwa kusema vijana lazima wawe kituo cha mapambano hayo, wasiwaachie wanasiasa pekee kupambana kwani wanasiasa lengo lao ni moja tu, kuingia madarakani na pindi wakishapata walichokikusudia wanasahau kila kitu.

HAFIDH KIDO 
17 April, 2013
Dar es Salaam, Tanzania


 

No comments:

Post a Comment