Friday, April 19, 2013

Chadema watangaza vita na kiti cha Spika.

Spika wa Bunge Annna Makinda akicheza dansi na mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu katika moja ya ghafla za bunge mjini Dodoma. (Picha na maktaba).


Dodoma. Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amesema kuwa watakata rufaa katika Kamati ya Kanuni ya Bunge dhidi ya mwongozo wa Spika uliobariki adhabu ya kuwatimua kwa siku tano wabunge sita wa Chadema kwa kudharau mamlaka ya Spika.
Akitoa mwongozo wake jana, Spika Anne Makinda alibariki wabunge hao kutimuliwa akisema kuwa Kanuni za Bunge zilikiukwa.
Wabunge waliofukuzwa na Naibu Spika, Job Ndugai juzi ni pamoja na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia, Mbunge wa Nyamagana, Ezekiah Wenje na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.
Juzi Mbowe aliomba mwongozo wa Spika kwa kutumia Kanuni ya 68 (7), akimtaka Spika aeleze naibu wake (Ndugai) alitumia kanuni gani ya Bunge, kuwasimamisha siku tano wabunge sita wa Chadema wasihudhurie vikao vya Bunge vinavyoendelea.
Mwongozo wa Makinda
Akitoa mwongozo huo jana, Spika Anne Makinda alisema kuwa kitendo kilichotokea hakiwezi kupuuzwa na wala kuvumiliwa na Bunge, pamoja na wananchi kwa kuwa ni utovu wa nidhamu ya Bunge na wananchi kwa jumla.
Alisema: “Kanuni ya 2(2) na 5(1), inampa mamlaka Spika ya kuleta amani bungeni.
Kanuni ya 2(2) inaeleza: “Iwapo jambo au shughuli yoyote haikuwekewa masharti katika kanuni hizi, Spika ataamua utaratibu wa kufuata katika jambo au shughuli hiyo, kwa kuzingatia Katiba, Sheria nyingine za nchi, kanuni nyingine zilizopo, maamuzi ya awali ya maspika wa Bunge na mila na desturi za uendeshaji bora wa shughuli za Bunge na uamuzi huo utaingizwa katika kitabu cha maamuzi ili kuongoza mwenendo wa baadaye wa uendeshaji wa shughuli za Bunge.”
Kanuni ya 5(1) inaeleza: “Katika kutekeleza majukumu yake yaliyotajwa katika Ibara ya 84 ya Katiba, Spika ataongozwa na kanuni hizi na pale ambapo kanuni hazikutoa mwongozo, basi Spika atafanya kazi kwa kuzingatia Katiba, Sheria nyingine za nchi, kanuni nyingine zilizopo, maamuzi ya awali ya maspika wa Bunge pamoja na mila na desturi za mabunge mengine yenye utaratibu wa kibunge unaofanana na utaratibu wa bunge la Tanzania.”
Makinda alisema kwa kutumia kanuni hizo mbili anakubaliana na uamuzi uliotolewa na Ndugai na kwamba suala hilo litaingizwa kwenye kitabu cha uamuzi wa Spika.
“Natumia Kanuni ya 2(2) na 5(1) kusema kuwa uamuzi uliofanywa na Ndugai ni halali na itaingizwa kwenye kitabu cha maamuzi ya Spika,” alisema Spika Makinda.
Kauli ya Mbowe
Mbowe jana alilieleza gazeti hili kuwa uamuzi wa Spika ulijielekeza katika jambo lisilo na kanuni inayolisimamia, tofauti na lile la kudharau mamlaka ya kiti cha Spika, lililotolewa maelekezo na Kanuni ya 74 (1).
Kanuni hiyo inasema: “Spika anaweza kutaja jina la mbunge kwamba amedharau mamlaka ya Spika na kisha kupeleka jina hilo kwenye Kamati ya Maadili na Madaraka ya Bunge; ikiwa kwa maneno au vitendo mbunge huyo anaonyesha dharau kwa mamlaka ya Spika; au Mbunge huyo atafanya kitendo chochote cha makusudi cha kudharau shughuli ya Bunge au mbunge yeyote anayeongoza shughuli hiyo.”
Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema alisema kuwa majibu ya Spika ni ya bahati mbaya kwa sababu yameonyesha mwendelezo wa kupuuza Kanuni za Bunge.
Akieleza kiini cha tatizo, Mbowe alisema kuwa ni kuyumba kwa kiti, upendeleo wa wazi, kupanga mikakati na CCM na kumpuuza Mnadhimu wa Chadema. Alisema nidhamu bungeni haitapatikana kwa kuwatimua wabunge na kwamba wapo tayari kwa hilo, hata kama wataisha wote, hadi pale Kiti cha Spika kitakapoacha upendeleo.
“Tutaliheshimu Bunge kama taasisi huru, lakini si lilivyo sasa kama taasisi ya CCM,” alisema Mbowe na kufafanua kuwa: “..Nje ya Bunge wote tunaheshimiana, lakini mambo yanakuwa tofauti bungeni kwa sababu ya Kiti cha Spika kutotenda haki.”
Alifafanua kuwa katika tukio zima, mbali na kupuuza kanuni, adhabu yenyewe ilitolewa nje ya utaratibu, ikiwa ni pamoja na kuruhusu askari wasiokuwa na sare kuingia bungeni.
“Bungeni pale kukiwa na siwa ni mahali patakatifu, lakini Naibu Spika ‘alipaniki’ akaruhusu watu wakatoka kusikojulikana bila sare na huo ni ukiukwaji wa taratibu,” alisema na kuongeza:
“Pale hata Makamu wa Rais ili aruhusiwe kuingia, lazima kanuni itenguliwe, watumishi wa Bunge na askari wanaoruhusiwa ndani, lazima wawe na sare maalumu, lakini mara hii Kiti cha Spika kimeruhusu watu wasiohusika kuingia.”
Alisema kwamba, Ndugai aliyaacha kando mambo ya msingi, akabakia kusema Tundu Lissu amesimama mara nyingi na kusahau kuwa mbunge huyo ni Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani, hivyo anaweza kusimama mara nyingi kadri ya mahitaji.
Alifafanua kuwa siku ya kufukuzwa kwa wabunge hao, Lissu alikuwa akitaka kuweka sawa kauli isiyokuwa sahihi ya Mwigulu Nchemba kuwa Dk Slaa hakufanya mkutano wa hadhara Singida wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, badala yake alifanya mkutano wa ndani ya viongozi wa dini.
Katika hatua nyingine, Frederick Katulanda, anaripoti kutoka Mwanza kuwa, wabunge watano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliosimamishwa kuhudhuria vikao vitano vya Bunge watafanya ziara katika mikoa mitano kwa ajili ya kuwaeleza wapigakura wa majimbo yao hali ya Bunge na upendeleo wa Spika wa Bunge , wanaoamini umesababisha wao kutimuliwa.
Akielezea ziara yao katika majimbo yao Mbunge wa Nyamagana, Ezekiah Wenje alisema kuwa wamefikia uamuzi huo ili kuwaeleza wananchi uonevu ndani ya Bunge na jinsi Spika na naibu wake wanavyoshindwa kusimamia kanuni kwa sababu ya kuwalinda CCM na Serikali.
Wenje alisema kwamba ratiba yao itaanzia katika Mkoa wa Mwanza, ambapo watafanya mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Sahara na kwamba wabunge wote watano watakuwapo kueleza yaliyowakuta bungeni.
MWANANCHI

No comments:

Post a Comment