Tuesday, April 30, 2013

Mwenyekiti wa tume ya mabadiliko ya katiba awatupia lawama wanasiasa.


Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amewataka wanasiasa kuacha tabia ya kutaka kuhodhi mjadala wa Katiba Mpya na badala yake waheshimu uhuru wa makundi yote ya wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Jaji Warioba alisema itakuwa vigumu kupata Katiba nzuri ikiwa watataka mjadala wa Katiba uendeshwe kisiasa.
Ametoa wito kwa viongozi wa vyama vya siasa, jumuiya na taasisi nyingine kuwaacha wananchi watoe maoni yao kuhusu rasimu ya Katiba kwa uhuru bila kuwaingilia kwa kuwa mivutano ya kisiasa inaleta shida.
Jaji Warioba alionya kuwa wanapaswa kufanya uamuzi mgumu kwani wanapokea maoni kutoka kwa watu wa makundi tofauti.
“Tutafanya uamuzi mgumu kwenye mambo ya msingi kwa kuwa hapa hatutengenezi katiba ya kidini wala ya kisiasa bali, tunaandaa katiba ya wananchi,” alisema Jaji Warioba.
“Tusipoondokana na suala la kujiweka vipandevipande, hatutapata Katiba Mpya na wala kufikia mwafaka, ni lazima tufanye maamuzi magumu ili tupate Katiba Mpya.”
Alisema Tume haiwezi kufanya kazi kwa shinikizo la wanasiasa bali, watafuata mwongozo uliopo ambao utaisaidia nchi kupata katiba ya Watanzania na si matakwa ya vikundi.
Jaji Warioba alisema mawazo mengi yaliyotolewa na wananchi na vikundi pamoja na vyama mbalimbali yanakinzana kwa kuwa wapo wanaotaka Serikali mbili, wengine tatu na wengine moja, huku wengine wakitaka Muungano uvunjwe wengine wakikataa, wengine wakitaka Serikali ya majimbo, wengine wakikataa. Hivyo uamuzi mgumu unahitajika kufanyika ili kufikia mwafaka.
“Hatuwezi kuvunja sheria hii ambayo imetungwa na waheshimiwa haohao, tutaendelea na utaratibu huuhuu na watu haohao kwani wanaokataa hawatuambii tutumie watu gani,” alisema Jaji Warioba.
Alisema anastaajabu kusikia watu wanahonga na kutoa rushwa ili waingie kwenye Mabaraza ya Katiba ya Kata na yale ya Wilaya wakidhani kuwa wakiwa wengi wa upande mmoja ndiyo maoni yao yatachukuliwa kwa wingi.
“Mabaraza haya ni kwa ajili ya kuangalia pande zote na si kwamba upande mmoja ukiwa na watu wengi maoni yao yatachukuliwa kwa wingi sisi tunachotaka ni hoja ambazo zitasaidia nchi na si vinginevyo,” alisema na kuongeza.
“Vyama visifikiri kuingia kwenye mabaraza kwa wingi na kuwa wengi ili kuzungumza jambo moja ndiyo litachukuliw; sisi hatuchukui hayo. Tunataka hoja za msingi.”

Alisema haitawezekana kila mwananchi wazo lake likubalike au kila kikundi wazo lake likubaliwe, hivyo ni lazima kila mmoja awe tayari kusikiliza mawazo ya wengine.
Alisema watu wanapaswa kuondoa hofu ya maoni yao kuchakachuliwa kwani watakuwa na nafasi ya kupigia kura hiyo rasimu ya Katiba.
Hivi karibuni, Chadema kilieleza bungeni kutoridhishwa na mwenendo wa kupata Katiba Mpya kikilalamikia pamoja na mambo mengine, uchaguzi wa wajumbe wa mabaraza ya wilaya ya Katiba uliofanywa na kamati za maendeleo za kata.
Mwenyekiti wake, ambaye pia ni Msemaji wa Kambi rasmi ya Upinzani bungeni, alitaka Serikali kuwasilisha mbele ya Bunge, Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ili kufanyia maeneo kadhaa marekebisho.

NUKUU
“Vyama visifikiri kuingia kwenye mabaraza kwa wingi na kuwa wengi ili kuzungumza jambo moja ndiyo litachukuliwa, sisi hatuchukui hayo. Tunataka hoja za msingi.” Jaji Joseph Warioba
MWANANCHI

No comments:

Post a Comment