Tuesday, April 16, 2013

Je unamfahamu Haji Mohammed? Soma hapa.

 Mtoto wa Haji Mohammed, Babu Eddy (mwenye shati la draft) akifarijiwa na ndugu jamaa msibani leo.

 Waumini wa dini ya kiislamu wakisalia mwili wa marehemu Haji katika msikiti wa Nambari mwembetanga kabla ya kuupeleka makaburini leo

 Jeneza likitoka msikitini tayari kuelekea makaburini kwa maziko mjini Zanzibar leo asubuhi.

 Waumini wa dini ya kiislamu wakizika leo asubuhi katika kijiji cha Shakani mjini Unguja Zanzibar leo.

 Mwimbaji wa Jahazi modern Taarab Mzee Yusuf alieshikilia gongo akishiriki maziko ya Haji Mohammed.

 Marehemu Haji Mohammed enzi za uhai wake akiwa na afya tele na tabasamu kila wakati kama ilivyo kawaida yake.


Picha zote kwa hisani ya www.Zanzinews.com

 Na Hafidh Kido

Haji Mohammed Omary, mwanamuziki mkongwe wa Taarab aliyefariki jumatatu wiki hii na kuzikwa mjini Zanzibar jumanne Aprili 16, anatajwa kuwa ni nguzo muhimu ya muziki huo iliyoanguka wakati akihitajika sana.

Baadhi ya kongwe wa muziki huo ambao walikuwepo msibani, miongoni mwao Bi Mwanahawa ally alizungumza na Raia Mwema na kumsifia Haji hakuwa mchoyo wa mawazo, alipenda kusaidia wanamuziki wote kila alipopata nafasi.

Naye katibu wa East African Melody Abuu Ruwa, alisema ‘Haji alisaidia kila mtu, hakuwa mchoyo wa mawazo kama huamini maneno yangu pita kila bendi uulize wanamuziki wote wa Taarab kama hawajawahi kufundishwa au kuelekezwa na Haji.

“Hata sijui alikuwa na kipaji cha aina gani, maana kila ulipokaa naye alizungumza kuhusu Taarab, katika bendi yetu mwanamuziki akija hapandi tu jukwaani ni lazima afunzwe kuendana na bendi yetu. Wanamuziki wengi wa Taarab walishafundishwa na Haji.

“Kwakeli sijui itakuwaje maana kuondoka kwa Haji ni pigo si kwa bendi yetu tu hata kwa bendi nyingine, hata ukienda bendi ya Gusagusa watakwambia. Kule aliimba na kila siku alikuwa akikaa na kushauriana nao kuhusu mambo ya muziki, alipenda muziki na aliujua,” alisema Abuu.


Haji Mohammed alizaliwa Septemba 9, 1962 katika hospitali ya Mnazi Mmoja Unguja akiwa mtoto wa pili katika watoto tisa waliozaliwa na mzee Mohammed Omary.

Alianza darasa la kwanza katika shule ya msingi Darajani na Sekondari katika shule hiyohiyo ya Darajani mpaka kidato cha tatu mjini Unguja. Baadaye akamalizia elimu yake ya sekondari katika shule ya Shangani hapohapo Unguja mnamo mwaka 1979..

Safari yake ya uanamuziki ilianza mwaka 1978 Zanzibar katika kikundi cha Taarab cha Razi ambacho kilikuwa mtaani kwao Vikokotoni mjini Unguja, baadaye akahamia bendi kongwe ya Nadi Ikhwan Safaa- Malindi. Wakati huo akiwa kijana mdogo akapikwa na kupikika kwenye muziki huo hasa upande wa kupiga vyombo na utunzi wa mashairi.

Baada ya kuiva katika kikundi cha Nadi Ikhwan Safaa akahamia kikundi kingine kikongwe cha muziki huo cha Culture ambacho kwa sasa ni chuo cha Taarab mjini Zanzibar ambapo yeye anatajwa kuwa miongoni mwa walimu waliofunda baadhi ya wanamuziki wanaotamba kwa sasa.

Haji anatajwa kuwa miongoni mwa watu walioanzisha Taarab ya kizazi kipya yaani Modern Taarab. Ambapo mwaka 1994 wakiwa falme za kiarabu Dubai, Haji akiwa na Mahmoud Alawi, Lamania Shaaban na Omary Mlamali, walianzisha kikundi cha East African Melody.

Mvumo wa kikundi hicho kilifika mpaka pwani ya Afrika Mashariki ambapo kwa ajabu kubwa Melody ikawa na wapenzi wengi Afrika Mashariki kuliko huko kilipoanzishwa. Ndipo wakaamua kurudi nyumbani Zanzibar na baadaye wakahamia Dar es Salaam miaka 13 iliyopita.

Kwa mujibu wa katibu wa East African Melody Abuu Ruwa ambapo Haji alikuwa mkurugenzi, Haji aliimba na kutunga nyimbo nyingi tangu alipoanza muziki na baadhi ni Karibu Habibi, Best Maridadi, Mambo yetu Bambam, Mavituz na Majamboz, Sitaki Nataka, Nitakufa kwa ahadi, Zilipendwa na nyingine nyingi ambazo zilifikia takriban nyimbo 50.

Kwa maneno yake Haji enzi za uhai wake alisema hajawahi kuona kiumbe anaeimba Taarab kwa ustadi kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki kama Rukia Ramadhani.

Haji alisema, aliwahi kutunga na kuuimba wimbo wa ‘Karibu Habibi’ lakini kwa kupenda kushirikisha watu katika sanaa akaamua kumjaribu Rukia Ramadhani auimbe wimbo huo. Basi kwa mara ya kwanza kuuimba aliuimba kwa ustadi kiasi akaona hata yeye hakuweza kuuimba kama alivyouimba Rukia, na akaamua urikodiwe upya na Rukia, hivyo ‘Karibu Habibi’ umerekodiwa mara mbili kwa heshima ya bi Rukia Ramadhani ambaye mpaka sasa anatamba katika tasnia hiyo.

Mpaka anaaga dunia jumatatu wiki hii katika hospitali ya Muhimbili kutokana na shinikizo la damu, Haji mohammed alifanikiwa kupata watoto watatu Mohammed, Ummy na Salama.

Aidha alifanikiwa kuoa wake wawili ambao wametajwa kwa jina moja moja la Fetty na Rahma ambao alitengana nao, inatajwa na ndugu zake wa karibu kuwa mpaka anafariki hakuwa na mke.

HAFIDH KIDO
16 April, 2013
Dar es Salaam, Tanzania



No comments:

Post a Comment