Arusha. Maofisa wa Jeshi la Polisi, waliokuwa na mbwa, mabomu ya
machozi na silaha nyingine za moto, usiku wa kuamkia jana waliruka ukuta na
kuingia katika eneo la makazi ya Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless
Lema ambako walizingira nyumba yake kwa zaidi ya saa nne.
Operesheni ya kutiwa mbaroni Lema iliogozwa na Mkuu wa Polisi wa
Wilaya ya Arusha (OCD), Gillel Muroto ambaye alifuatana na askari zaidi ya 25
waliokuwa na silaha hizo.
Walifika nyumbani kwa Lema saa 5:00 usiku lakini walilazimika
kusubiri hadi saa 9:10 walipomkamata Mbunge huyo baada ya yeye mwenyewe
kujisalimisha. Habari zinasema Lema aliyekuwa akihojiwa na polisi hadi jana
jioni, alinyimwa dhamana kwa maelezo kwamba “anaweza kuhatarisha amani”.
Mashuhuda waliokuwa karibu na anakoishi Lema, eneo la Njiro
Mwisho wa Lami, walisema polisi hao walifika wakiwa kwenye magari manne na
kwamba ili kuchunguza ndani ya uzio wa nyumba yake, walipanda juu ya mabega ya
wenzao huku wakielekeza mitutu ya bunduki tayari kukabiliana na lolote ambalo
lingejitokeza.
Baada ya kuchungulia baadhi yao walitumbukia ndani ya uzio na kwenda
kusimama mbele ya milango na madirisha ya nyumba ya Lema na huku nyuma wengine
walipanda tena kwenye mabega ya wenzao kuendelea kuweka ulinzi kwa walioingia
ndani.
Askari hao wanadaiwa kwamba waliwataka walinzi wa nyumba hiyo
iliyopo karibu na Chuo cha Ufundi Veta, kuwafungulia mlango, lakini walinzi hao
walikataa hivyo kuzua mabishano makali.
Kutokana na mabishano hayo, Lema aliyekuwa ndani amelala
alishtuka na kuanza kufuatilia na kubaini kuwapo kwa polisi nje ya nyumba yake
hiyo. Mke wa Lema, Neema alimpigia simu Katibu wa Wilaya wa Chadema, Aman
Golugwa kumwarifu kuhusu uwepo wa watu walioruka ukuta.
Golugwa jana alithibitisha kupokea simu ya mke wa Lema na kwamba
alipopata taarifa hizo alimwarifu Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) wa
Mkoa wa Arusha, Camillius Wambura ambaye baadaye alimuahidi kwamba angefuatilia
suala hilo .
“Baadaye alithibitisha kuwapo kwa polisi waliotumwa kwa ajili ya
kumkamata Lema lakini akasema amewapa maelekezo ya kufuata taratibu za
kawaida,”alisema Golugwa na kuongeza:“Baada ya hapo, wale askari waliokuwa
wameruka ukuta walitoka nje ya uzio”.
Habari zinasema wakati baadhi ya askari wanaruka ukuta, wengine
walibaki nje wakizingira uzio wa nyumba ya Lema huku wakiwazuia viongozi wa
Chadema waliokuwa eneo hilo
kusogea.
Kukamatwa kwa Lema katika mtindo wa aina yake kumefanywa saa
chache tangu alipotoa kauli ya kukataa kujisalimisha polisi, kutokana na agizo
la Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo. Mulongo aliagiza Lema akamatwe kwa
tuhuma kwamba alichochea vurugu katika Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA).
Katika vurugu hizo, wanafunzi hao walimzomea Mulongo na kurushia
mawe msafara wake wakati alipokwenda kusikiliza malalamiko yao yaliyotokana na kuuawa kwa mwanafunzi
mwenzao, Henry Kago (22) ambaye alichomwa kisu na watu wasiofahamika wakati
anatoka kujisomea saa 4:00 usiku.
“Kuna taratibu za kumwita mbunge polisi, wanaweza kunipigia simu
au kuwasiliana na Spika, lakini siyo kutumia utaratibu huu wa kutangaza kwenye
vyombo vya habari kuwa mimi natakiwa kukamatwa wakati najua sina kosa,”alisema
Lema.
Kauli ya Lema
Akizungumza na Mwananchi kabla ya kujisalimisha kwa askari hao juzi usiku, Lema alisema alishangaa polisi kuvamia nyumba yake usiku wakati walikuwa na uwezo wa kumpigia simu na kumwita.
Akizungumza na Mwananchi kabla ya kujisalimisha kwa askari hao juzi usiku, Lema alisema alishangaa polisi kuvamia nyumba yake usiku wakati walikuwa na uwezo wa kumpigia simu na kumwita.
“Wapo nje ya nyumba yangu, wanatishia kupiga mabomu kama nisipotoka nje, lakini wanajadiliana na walinzi
wangu na mimi nimewataka wanipe hati ya kunikamata,” alisema Lema. Hata hivyo,
baada ya muda idadi kubwa ya wafuasi wa Chadema, walijitokeza na kuzingira
nyumba ya Lema, hali ambayo ilianza kutishia uvunjifu wa amani.
Golugwa ndiye aliyefanya majadiliano na OCD Muroto kuhusu namna
ya kufanikisha mbunge huyo kujisamilisha baada ya kuwa amewasiliana na Katibu
Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa na ilipotimu saa 9:10 usiku Lema
alijisamilisha baada ya kuhakikishiwa usalama wake.
Mmoja wa viongozi wa Chadema, Calist Lazaro alisema walikubali
Lema aende polisi, baada ya majadiliano na viongozi wa juu ya chama hicho.
“Tulitaka Polisi watuhakikishie usalama wake na pia tulitaka
suala hili lifanyike kwa uwazi kwani siyo jambo la kawaida mbunge kuvamiwa na
polisi usiku kama jambazi,”alisema Lazaro.
Polisi wanena
Kamanda wa polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabas jana, alikiri maofisa wa jeshihilo kumkamata
mbunge huyo juzi usiku na hadi jana mchana alikuwa bado yupo rumande.
Kamanda wa polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabas jana, alikiri maofisa wa jeshi
“Ni kweli tupo naye hapa polisi, anasubiri kuhojiwa kutokana na
tuhuma za uchochezi katika Chuo cha Uhasibu Arusha,”alisema Kamanda Sabas.
Alisema uamuzi wa kuendelea kumshikilia au kumwachia, utatolewa baada ya
kukamilika mahojiano.
Mapema wakili wa Lema, Hamphrey Mtui akizungumza na Mwananchi
nje ya kituo kikuu cha polisi, alisema bado alikuwa hajaruhusiwa kuonana na
mteja wake .
“Bado tunasubiri polisi wamtoe na wakati wa kuchukua maelezo
yake ndiyo wameniambia wataniita,” alisema Mtui. Baadaye Lema alihojiwa lakini
alikataliwa kupewa dhamana.
Taarifa za kukamatwa kwa Lema zilianza kusambaa juzi saa sita
kasorobo usiku na ilipofika jana asubuhi tayari tukio hilo lilikuwa limeishateka mijadala ya
mitandao ya kijamii.
Mijadala hiyo iliambatana na mkanda wa Video wa Lema wakati akizungumza
na wananfunzi wa IAA.
Hali hiyo pia iliuweka mjia wa Arusha
katika hali tete na kulikuwa na wasiwasi mkubwa kwamba wafusai wa Chadema
wangeandamana kushinikiza kuachiwa kwa mbunge huyo. Katika kituo kikuu cha
polisi kulikuwa na kundi kubwa la wafuasi wa Chadema waliokusanyika kufuatilia
hatma ya mbunge wao na kusababisha ulinzi uongezwe maradufu ili kukabiliana na
lolote ambalo lingeweza kutokea.
Imeandikwa na Mussa Juma, Moses Mashalla na Peter Saramba, Arusha.
Imeandikwa na Mussa Juma, Moses Mashalla na Peter Saramba, Arusha.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment