Monday, April 22, 2013

Barcelona Vs Bayern Munich leo usiku.



Vita kusaka tiketi ya kusafiri kwenda jijini London kwenye mchezo wa fainali wa klabu bingwa barani Ulaya inaanza usiku huu kati ya Mabingwa wa soka nchini Ujerumani dhidi ya inayotajwa kuwa timu bora kwa vilabu vya soka duniani kwa wakati huu FC Barcelona.
Kocha wa Bayern Munich, Jupp Heynckes amesema haogopeshwi na urejeo wa nyota wa Barcelona, Lionel Messi kuelekea mchezo huo wa kwanza wa nusu fainali ya klabu bingwa barani Ulaya.
Messi hajacheza mchezo wowote wa Barcelona toka alipoingia kama mchezaji wa akiba na kuisaidia timu yake kufuzu nusu fainal katika mchezo robo fainali dhidi ya Paris St-Germain ya Ufaransa. Lakini kuna kila dalili Muanjetina huyo mwenye umri wa miaka 25 ambaye ndiye mchezaji bora wa dunia kwa sasa,akajumuishwa kwenye kikosi cha Barcelona kwenye mchezo wa usiku wa leo.
Mwezi uliopita Messi aliweka rekodi kwenye ligi ya Hispania kwa kuwa mchezaji aliyezifunga timu zote zinazoshiriki ligi kuu nchini humo maarufu kama La Liga kwa misimu miwili mfululizo.
Barcelona inapambana kutaka kutwaa taji la tatu la klabu bingwa barani Ulaya ndani ya miaka mitano,Huku Bayern Munich ambao msimu ujao watakuwa chini ya aliyekuwa kocha wa Barcelona, Pep Guardiola, wao wanapambana kutafuta nafasi ya kucheza fainali yao ya tatu ndani ya miaka minne.
Kocha wa Bayern Munich, Jupp Heynckes ambaye aliwahi kuwafundisha mahasimu wa Barcelona, Real Madrid amesema licha ya kumheshimu mrithi wake wa kiti cha ukocha kwenye timu hiyo lakini hajaomba ushauri wowote kutoka kwa Guardiola na amejiandaa kwa kila namna kuhakikisha anaifunga Barcelona usiku huu. Aliongeza kwa kusema anaijua vizuri sana timu yake kuliko mtu yeyote na anafahamu soka ya Hispania na Barcelona wenyewe kwa undani mkubwa.
Wakati Barca wakiwa hawajaweka wazi kama watamuanzisha Messi au la, Baadhi ya wachezaji wa Barcelona akiwemo Xavi Hernandez alinukuliwa siku ya jumatatu akisema, kombe la ligi kuu nchini Hispania, La Liga lina umuhimu mkubwa kuliko klabu bingwa barani Ulaya.
Mechi hiyo itachezwa kwenye uwanja wa Allianz Arena mjini Munich nchini Ujerumani,majira ya saa nne kasorobo usiku kwa saa Afrika Mashariki.
BBC SWAHILI

No comments:

Post a Comment