Duru kutoka kwa ofisi ya rais wa Misri Mohammed Morsi
zinasema kuwa huenda mwafaka umeafikiwa ili kumaliza mzozo uliopo kuhusu idara
ya mahakama.
Baada ya mzungumzo na maafisa wakuu wa
idara ya mahakama, Jumapili, rais Morsi alisema kuwa kongamano litaandaliwa
wiki hii kutoa nafasi ya kuwalisha malalamiko yoyote na kuwa atakubali uamuzi utakaotolewa.
Mpango wa kupunguza umri wa majaji kuweza
kustaafu ulikuwa umetishia nyadhifa za maelfu ya majaji na hivyo kuighadhabisha
idara ya mahakama.
Bwana Morsi amekuwa katika mzozano na idara ya
mahakama tangu aingie mamlakani mwezi Juni mwaka jana.
Washirika wake katika chama cha Muslim
Brotherhood, wanasema kuwa mahakama imejaa majaji waliokuwa wanamuunga mkono
rais wa zamani Hosni Mubarak.
Nao wapinzani wa Morsi wanasema kuwa anajaribu
kujaza nafasi hizo na wafuasi wake.
Mgogoro ulikithiri wiki jana wakati bunge
lilipoendelea kujadili mswaada unaonuia kupunguza umri ambao majaji wanaweza
kustaafu kutoka miaka 70 hadi 60, hali itakayowaathiri majaji 13,000 na
viongozi wa mashtaka.
Mswaada huo pia ungezuia mageuzi katika idara
ya mahakama kuhusu mamlaka ya Rais aliyojiongezea mwaka jana.
Maandamano dhidi ya mswaada huo yalipangwa
kufanyika Jumatatu ingawa kwa sasa yamefutiliwa mbali.
BBC SWAHILI
No comments:
Post a Comment