Sunday, April 21, 2013

Saikolijia: Wanawake na wanaume huia tofauti.




Unaitazama filamu ya msanii Kanumba. Wewe pamoja na wenzako mnatiririkwa na machozi yanayoambatana na kwikwi.
Ghafla unatazama pembeni, unamwona paka wako akikushangaa  kwa kilio chako ambacho kinatokana na tukio la filamu ambalo ni la kufikirika tu.
Unafikiri ni kwa nini binadamu analia akiwa mtoto mchanga hadi anapokuwa mtu mzima tofauti na wanyama wengine?
Wanasayansi waeleza
Watafiti wa  nchini Ujerumani walifanya utafiti kuhusu kulia na kubaini kuwa wanawake hulia kati ya mara 30 hadi 63 kwa mwaka na wanaume hulia mara 6 hadi 17 kwa mwaka.
Wanaume hulia kwa dakika mbili hadi nne wakati wanawake hulia kwa zaidi ya dakika sita.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Muhimbili, Dk Kitila Mkumbo anasema kitendo cha kulia kinatokana na mifumo ya hisia.
Anasema binadamu huweza kulia kutokana na hasira, maumivu au furaha.
Zipo aina tatu za machozi
Binadamu yeyote ana mirija ya machozi ambayo hutumika kulowanisha na kulinda macho yasiathiriwe na vumbi na vitu vingine.
Mirija hiyo ipo chini ya kope za juu na huzalisha maji yenye chumvichumvi ambayo ndiyo machozi-hayo  husambazwa katika jicho- kila  binadamu anapopepesa.
Wanasayansi wanasema, zipo aina tatu za machozi ambazo huzalishwa na macho ya binadamu.
Yapo machozi yajulikanayo kama ‘Basal’ au Basali. Machozi haya yana kazi kubwa ya kulinda jicho na kulipa unyevu.
Machozi mengine ni ya ‘Reflex’ haya yana kazi kubwa ya kutoa tahadhari kwa jicho pale linapoumia. Kwa mfano mtu akikata kitunguu au mdudu akiingia jichoni.
Machozi ya hisia au  ‘Pysch’ haya hutiririka pale ambapo binadamu hupatwa na uchungu, maumivu, msongo wa mawazo au furaha.
Tafiti zinaonyesha kuwa machozi ya hisia yana kiwango cha manganizi, chembechembe ambazo huathiri tabia au roho ya binadamu.
Machozi hayo ya hisia pia yana vichocheo vya prolactini ambavyo husimamia uzalishwaji wa maziwa.
Machozi yanayozalishwa kwa hisia yana mchanganyiko wa kemikali tofauti na aina nyingine za machozi.
Hivyo basi, binadamu anapolia, hutoa manganizi, potashiam na prolactini.  Chembechembe hizo zinatajwa kupunguza mshtuko au huzuni kwa  kuweka uwiano wa msongo wa mawazo katika mwili.
Ubongo unavyofanya kazi hadi binadamu kulia
Kwa kawaida mfumo wa fahamu (ubongo) kupitia mishipa maalumu ya fahamu huweza kuwasiliana na kutafsiri taarifa mbalimbali za kimwili na kisha mwili hutoa mwitiko baada ya tafsiri.
Machozi yatokanayo na kuhuzunika (emotion tears) huwa yanaambatana na uso kubadilika kuwa mwekundu, misuli ya uso kukunjika, kutetemeka, pumzi kukatika na mwisho huenda mwili mzima ukakamaa.
Machozi yatokanayo na hali hii ni tofauti ukilinganisha na machozi ya kawaida ya kulainisha jicho, machozi ya  hisia huwa na vichocheo aina ya prolactini na adrenocotrico.
Hali hii hudhibitiwa na mfumo usio wa hiyari ‘autonomic system.’   
Mfumo huu umepenyeza mishipa ya fahamu inayoshusha mihemko ya kimwili (parasympathetic system) katika tezi inayohifadhi machozi kitaalamu inaitwa lacrimal.
Kemikali maalumu ziitwazo ‘acetylcholine’ hupitisha taarifa za mfumo wa fahamu, kwenda katika vipokezi vilivyopo katika tezi ya lacrimal iliyopo katika kona ya jicho.
Hapo  tezi hiyo hupata mihemko na kumwaga machozi kutokana na taarifa ilivyotafsiriwa katika ubongo kam vile hasira au mtu kuudhiwa.
Mawasiliano
Wataalamu wengine wanasema kuwa kulia au machozi ya hisia ni nyanja ya mawasiliano. Kabla watoto hawajaweza kuzungumza hulia.
Hii ndiyo njia pekee kwa watoto wachanga kueleza hisia zao za  maumivu, kuumwa au woga.
Hata hivyo watu wazima hulia ili kujenga ukaribu na wenzao. Kulia kwa uchungu kunasaidia walio karibu nao kuonyesha ukaribu wao na upendo kwako.
Wengine wanadai kuwa kulia husaidia kuondoa kiwango cha sumu mwilini.
Mwanasaikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Modesta Kimonga anasema kibaolojia mtu hulia kwa sababu ya vichocheo ambavyo husimamia uamuzi.
“Kwa kawaida ubongo wa mtu hupeleka taarifa kuwa mtu anataka kulia kutokana na vichocheo vya lanchrimal” anasema Kimonga
Kimonga anasema tofauti ya kulia kati ya wanawake na wanaume husababishwa na mguso wa moyo.
Wanaume hulia kwa kiwango kidogo kwa sababu  wana mguso wa chini tofauti na wanawake.
Mwanasayansi  wa Dutch, Ad Vingerhoets ambaye ametumia miaka 20 kutafiti kwa nini na wakati gani binadamu hulia anasema machozi yanamaanisha kukosa msaada.
Vingerhoets anasema kulia ni maelezo ya hisia kwa watu wazima na ni mawasiliano.
“Watu wengine hulia ili wapate ukaribu, wabembelezwe na watengeneze uhusiano,” anasema  Vingerhoets
Mwanahistoria wa tamaduni, Thomas Dixon anasema machozi wakati mwingine  husababishwa na furaha kuliko hasira au huzuni.
“Kwa mfano mwanariadha aliyeshinda medali ya dhahabu, mwanamuziki aliyepata tuzo anaweza kulia kwa furaha,” anasema
Aina za kulia
Dk Mkumbo anasema watu wametofautiana kiwango cha kulia.
“Wapo ambao hulia hata kama wakicheka, lakini wengine ni vigumu kutoa machozi hata wakumbwe na huzuni kiasi gani” anasema
Anasema kulia kunatofautiana kulingana na kiwango cha hisia, mila, tamaduni na maadili.
“Zipo mila ambazo mwanamume haruhusiwi kulia kwani kulia kunafananishwa na woga. Wanaume wa makabila haya hurudisha machozi ndani na kubeba huzuni kwa namna nyingine” anasema Dk Mkumbo.
Kasoro za vilio
Upo ugonjwa kwa kitaalamu unajulikana kama Bell’s palsy ambapo neva za uso husababisha mtu kutokwa machozi pindi anapokula.
‘Cri du chat’, ambapo kichanga anaweza kulia sawa sawa na paka. Tatizo hili huhusishwa na mfumo wa fahamu.
Wapo wanaolia lakini machozi hayatoki, huu ni ugonjwa.
Wengine hushindwa kutofautisha matukio ya kulia au kucheka na wakati mwingine yote kwa pamoja.
MWANANCHI

No comments:

Post a Comment