Friday, April 19, 2013

Hatma ya wabunge wa Chadema kujulikana leo.

Wabunge wa Chadema wakimkinga mbunge mwenzao Tundu Lissu asitolewe na askari nje ya ukumbi.


Chanzo cha kutimuliwa ni kuwazuia askari wa Bunge kumtoa nje Lissu ambaye alikuwa ameamriwa kutoka nje na Naibu Spika, Job Ndugai baada ya kuingilia hotuba ya Mbunge wa Iramba Mashariki, Mwigulu Nchemba (CCM).
Dodoma. Spika wa Bunge, Anne Makinda amesema leo atatoa mwongozo kuhusu tukio la Naibu Spika, Job Ndugai kuwasimamisha wabunge sita wa Chadema.
Juzi, Ndugai aliwasimamisha wabunge hao Tundu Lissu (Singida Mashariki), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini), Highness Kiwia (Ilemela), Ezekiah Wenje (Nyamagana) na Godbless Lema wa Arusha Mjini kutohudhuria Bunge kwa siku tano kutokana na alichokiita kufanya vurugu ndani ya bunge.
Hatua hiyo ya Spika Makinda imekuja baada ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kumtaka aeleze Ndugai alitumia kanuni gani kuwasimamisha wabunge hao.
Jana, baada ya kipindi cha maswali na majibu, Mbowe alisimama na kuomba mwongozo wa Spika akitumia Kanuni ya 68(7) inayosema; “Hali kadhalika, Mbunge anaweza kusimama wakati wowote ambapo hakuna mbunge mwingine anayasema na kuomba “Mwongozo wa Spika” kuhusu jambo ambalo limetokea bungeni mapema, ili Spika atoe ufafanuzi kama jambo hilo linaruhusiwa au haliruhusiwi kwa mujibu wa Kanuni za Bunge na majibu ya Spika yatatolewa papohapo au baadaye, kadri anavyoona inafaa.”
Mbowe alisema Kanuni ya 73(3) ndiyo inayompa ruhusa Naibu Spika na Spika kuwasimamisha wabunge na aliisoma: “Endapo Mbunge yeyote atatakiwa kuthibitisha ukweli wa maneno aliyoyasema na hadi kufikia mwisho wa muda alipopewa amekataa au ameshindwa kutoa uthibitisho huo, Spika anaweza kumsimamisha mbunge huyo asihudhurie vikao vya Bunge visivyozidi vitano.
“Kwa mujibu wa yaliyotokea jana (juzi) ilitokea sintofahamu katika matumizi ya kifungu hiki wakati tulitegemea Kifungu cha 74(1) ndicho kingetumika kwani kama mbunge amedharau mamlaka ya Spika jina lake linaweza kupelekwa kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge,” alisema Mbowe na kuongeza: “Mheshimiwa Spika nataka mwongozo wako kujua Naibu Spika alitumia kanuni gani?”
Awali, Spika Makinda aliahidi kutoa mwongozo wake baadaye jioni kabla ya kuahidi kufanya hivyo leo wakati akiahirisha shughuli za Bunge jana.
Awali, baada ya mwongozo wa Mbowe, Spika Makinda alimruhusu Mbunge wa Kawe, Halima Mdee kuomba mwongozo wake na aliposimama alisema: “Mwongozo wangu uko palepale katika kanuni ileile iliyoombwa na kiongozi wa kambi ya upinzani.”
Kabla hajamaliza, Spika alimkatisha na kumweleza kuwa hawezi kutoa nafasi ya mwongozo wa kitu hichohicho.
Alimruhusu Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema ambaye alisema: “Waandishi walioandika kanuni hizi kwamba jambo lilitokea mapema hawakumaanisha jana.”
Kabla Jaji Werema hajamaliza, Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika alisimama lakini Spika alimzuia na kuwakatisha wote akisema: “Waheshimiwa wabunge, hakuna kitu kinachowaharibia wananchi kama kilichotokea jana (juzi), jana (juzi) hakuna kitu kilichojadiliwa zaidi ya kuleta zahama.”
Nchemba tena
Alimruhusu Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Mwigulu Nchemba kuendelea kutoa mchango wake ambao ulikatishwa kutokana na vurugu za juzi na jana nusura tena tafrani izuke kati yake na Mnyika hasa baada ya Nchemba kueleza suala la mabaraza ya Katiba kuwa utaratibu ulipitishwa bungeni na wabunge wote.
Alisema kinachotaka kujengwa na wapinzani hakipo kwa kuwa katika Jimbo la Karatu lililoko chini ya upinzani, wenyeviti wa mabaraza ya Katiba walichaguliwa wa CCM.
Mnyika alisimama akitaka kumpa taarifa Nchemba kwa kutumia Kanuni ya 63(1) akisema Mwigulu kueleza kuwa utaratibu wa kutumia mikutano ya maendeleo ya kata kuchuja wajumbe wa mabaraza WDC ulipitishwa na Bunge ni uongo kwa kuwa utaratibu huo ulipitishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Spika alimruhusu Nchemba kuendelea kuchangia, ndipo aliposema: “Tunapoongea watoto wa kiume watulie.”
Kauli hiyo ilikataliwa na Spika Makinda ambapo alimtaka Nchemba kuifuta... “Naifuta mheshimiwa Spika,” alisema Nchemba.
MWANANCHI

No comments:

Post a Comment