Taarifa za awali kutoka chuoni hapo ambazo bado hazijathibitishwa
na Jeshi la Polisi zinaeleza kwamba kijana huyo anahisiwa kuchomwa kisu na
vibaka wakati akirejea kwenye maeneo yao
ya malazi (hosteli) eneo la ESAMI.
Inaelezwa kuwa, kabla ya kufika hostel, alipigiwa simu na mwenziye
kuwa amsubiri ili waongozane pamoja kuelekea hostel. Wakati akisubiri rafiki
yake amfikie, ndipo watu wasiofahamika waliokuwa wanadai wapatiwe fedha,
walimvamia na kumchoma kisu tumboni na shingoni.
Rafiki wa marehemu naye pia alichomwa kisu tumboni.
Mbunge wa Arusha Mjini, Mhe. Godbless Lema alifika chuoni hapo na
kuzungumza na wanafunzi hao ili kuwatuliza baada ya kutaarifiwa kuwa kuna
vurugu zilizotokana na hasira ya Wanachuo kumshutumu Mkuu wa Chuo kutokuwapa
msaada wa haraka hasa baada ya wao kulalamika kwa muda mrefu sasa kuhusu hali
duni ya usalama katika chuo hicho. Mwaka jana mwanafunzi mmoja aliuawa na
katika nyakati tofauti, wanafunzi wamekuwa wakivamiwa na kuibiwa vifaa vyao.
Taarifa pia zilimfikia Mkuu wa Mkoa, Magessa Mulongo ambaye
aliwasili chuoni hapo na kuzungumza na wanachuo lakini ilizuka tafrani ndipo
Wanachuo walianza kurusha mawe.
Kikosi maalumu cha Askari Polisi wa kutuliza ghasia, FFU, kipo
katika eneo hilo
kwa ajili ya kufanya kazi yake.
CHANZO:WAVUTI
No comments:
Post a Comment