Mwimbaji nguli wa muziki wa tarabu nchini Tanzania Fatma
binti Baraka, maarufu kama Bi Kidude amefariki Jumatano kisiwani Zanzibar akiwa na umri wa
zaidi ya miaka 100.
Taarifa ya kifo chake ilitolewa na mjukuu wake Fatuma Baraka
ambaye pia ni muimbaji wa Taraabu. Alisema Bi Kidude alifariki hospitalini
kutokana na maradhi ya kisukari na uvimbe kwenye Kongosho.
Bi Kidude amekuwa katika fani ya muziki wa
taarab ya kiasili pamoja na ngoma za unyago kwa zaidi ya robo tatu ya umri
wake.
Katika
miaka ya karibuni afya yake imekuwa ikizorota kiasi cha serikali ya Zanzibar kumzuia kupanda
majukwaani kuburudisha japokuwa alionekana katika tamasha la Sauti za Busara
mwezi Februari mwaka huu.
Mipango
ya mazishi ya nguli huyu inafanywa nyumbani kwake Zanzibar .
Wengi,
hasa vijana wa kizazi kipya wanamfahamu Bi. Kidude kwa uwezo wake mkubwa wa kuimba
taarabu kwa kuchanganya lugha ya kiswahili na ile ya kiarabu. Nyimbo zake za
kiarabu mara nyingi zimekuwa na ladha kama ile
ya aliyekuwa mwimbaji gwiji wa Misri Ummu Kulthumu.
Sio
uimbaji tu uliomfikisha Bi. Kidude alipofika, bali uwezo wake pia wa kutunga
mashairi, kutumia ala za mziki kama vile
kupiga ngoma na hata ngoma za unyago, vyote hivi vilimuweka Bi. Kidude katika
nafasi tofauti katika jamii.
Alikuwa
na tabia ya kumwita kila mtu 'mwanangu,' ingawa yeye mwenyewe hakubahatika
kupata mtoto. Katika mahojiano aliyofanyiwa na vyombo mbali mbali vya habari,
mwenyewe alisikika akisema, ingawa alikuwa na hamu ya kupata mtoto, lakini
Mwenyezi Mungu hakumjaalia.
Katika
miaka ya hivi karibuni, Bi. Kidude alishirikishwa sana na wasanii wengine katika kazi zao.
Miongoni mwao ni Ahmada Amelewa, Fid Q Juhudi za Wasiojiweza.
Mbali
na hayo, mashirika mbali mbali yakiwemo ya kibiashara na yale yasiyo ya
kiserikali yaliona mvuto aliokuwa nao Bi. Kidude katika jamii, hivyo wakamtumia
katika matangazo mbali mbali maarufu likiwa lile la kutokemeza Malaria.
Ni
bibi aliyebahatika kusafiri takriban duniani kote, na vilevile katika maisha
yake alijinyakulia tuzo lukuki. Miongoni mwa hizo ni ile ya 2005 WOMEX ikiwa ni
kutambua mchango wake mkubwa katika tasnia ya muziki.
Katika
siku zake za mwisho, Bi. Kidude alikuwa akiumwa, lakini wengi wanahusisha
kuumwa kwake na utu uzima aliokuwa nao.
Kifo
chake ni pigo kubwa kwa wote, lakini zaidi ni wanamziki wa kizazi kipya
waliokuwa wakimuona Bi. Kidude ni nyanya yao .
BBC Swahili.
No comments:
Post a Comment