Friday, April 19, 2013

KILA LA KHERI AZAM FC




Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaitakia kila la kheri timu ya Azam FC katika mechi yake ya kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho dhidi ya AS FAR Rabat ya Morocco itakayochezwa kesho (Aprili 20 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.

Azam FC ina fursa nzuri ya kufanya vizuri kwenye mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi Emile Fred kutoka Shelisheli kutokana na maandalizi iliyofanya, lakini vilevile tunatoa mwito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi uwanjani kuiunga mkono.

Makocha wasaidizi wa timu zote mbili, Kalimangonga Ongala wa Azam na Lahcen Ouadani wa AS FAR Rabat wamezungumza na waandishi wa habari kuhusu mechi hiyo, kuwa wamejiandaa kuibuka na ushindi.

Kocha Ongala amesema wamepata DVD za mechi tatu za mwisho za AS FAR Rabat, moja ikiwa dhidi ya timu ya Al Nasir ya Libya ambayo waliitoa katika raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho na nyingine mbili za ligi ya Morocco ambazo wanazifanyia kazi kuhakikisha wanashinda kesho.

Naye Ouadani amesema hawaifahamu vizuri Azam, lakini wanaujua mpira wa Tanzania baada ya kuangalia mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Morocco (Lions of the Atlas) iliyochezwa jijini Dar es Salaam Machi 24 mwaka huu na Stars kushinda mabao 3-1.

Baadhi ya wachezaji ambao Azam inatarajia kuwatumia kwenye mechi ya kesho ni pamoja na Aishi Manula, Mwadini Ally, Khamis Mcha, John Bocco na Salum Abubakar ambao pia wamo kwenye kikosi cha sasa cha Taifa Stars kilicho chini ya kocha Kim Poulsen.

AS FAR Rabat ina wachezaji sita kwenye timu ya Taifa ya Morocco. Wachezaji hao ni mabeki Younes Bellakhdar, Abderrahim Achchakir, Younnes Hammal, na viungo Salaheddine Said, Salaheddine Aqqal na Youssef Kaddioui.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
 Aprili 19, 2013

No comments:

Post a Comment