Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen ametangaza
timu ya pili ya Taifa (Young Taifa Stars) atakayoitumia kuangalia wachezaji
ambao baadaye anaweza kuwajumuisha kwenye timu ya wakubwa.
Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam leo (Aprili
23 mwaka huu) kabla ya kutaja kikosi hicho, Kim amesema timu hiyo ni sehemu ya
Mpango wa Maendeleo wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
uliozinduliwa Aprili 4 mwaka huu ukilenga kuendeleza wachezaji.
Amesema timu hiyo inajumuisha wachezaji ambao
wamepita umri wa kuchezea timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20
(Ngorongoro Heroes) na wakubwa ambao hawajapata fursa ya kuingia Taifa Stars,
lakini atatumia Young Taifa Stars kuangalia uwezo wao.
“Timu hii ni kiungo kati ya vijana na wakubwa.
Wengi wa wachezaji watakuwa vijana, lakini wakubwa wachache watapata fursa ya
kuwemo ili kuangalia uwezo wao hata kama uko
nyuma waliwahi kuchezea Taifa Stars. Lakini timu hii vilevile ni changamoto wa
wachezaji wa Taifa Stars kuwa wapo wanaosubiri wazembee ili wachukue nafasi
zao,” amesema.
Young Taifa Stars yenye wachezaji 30 itakuwa na
kambi ya siku tano jijini Dar es
Salaam kuanzia Mei 2 hadi 6 mwaka huu.
Wachezaji walioitwa ni Aishi Manula (Azam),
Hussein Shariff (Mtibwa Sugar) na Ali Mustapha (Yanga) ambao ni makipa. Mabeki
ni Kessy Hassan (Mtibwa Sugar), Kennan Ngoma (Barnsley FC, Uingereza), Himid
Mao (Azam), Ismail Gambo (Azam), David Mwantika (Azam), Miraji Adam (Simba),
Mohamed Hussein (Kagera Sugar), Waziri Salum (Azam), Samih Nuhu (Azam) na Emily
Mgeta (Simba).
Viungo ni Haruna Chanongo (Simba), Edward
Christopher (Simba), Mudathiri Yahya (Azam), William Lucian (Simba), Jonas
Mkude (Simba), Hassan Dilunga (Ruvu Shooting), Jimmy Shoji (JKT Ruvu), Abdallah
Seseme (Simba), Ramadhan Singano (Simba), Farid Mussa (Azam) na Vicent Barnabas
(Mtibwa Sugar).
Washambuliaji ni Hussein Javu (Mtibwa Sugar),
Jerome Lambele (Ashanti United), Zahoro Pazi (JKT Ruvu), Twaha Hussein (Coastal
Union), Abdallah Karihe (Azam) na Juma Luizio (Mtibwa Sugar).
AFRICAN LYON, JKT RUVU KUUMANA CHAMAZI
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa
Tanzania Bara inaendelea kesho (Aprili 24 mwaka huu) kwa mechi moja kati ya
wenyeji African Lyon na JKT Ruvu.
Mechi hiyo namba 165 itachezwa Uwanja wa Azam
Chamazi, Dar es Salaam chini ya usimamizi wa
Kamishna Hamisi Kisiwa wa Dar es
Salaam . Waamuzi wa mechi hiyo itakayoanza saa 10
kamili jioni ni Hashim Abdallah, Omari Kambangwa, Abdallah Selega na Said Ndege
wote wa Dar es Salaam .
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF)
Aprili 23, 2013
No comments:
Post a Comment