Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad
akifurahi pamoja na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Alfonso Leonhart,
aliyefika nyumbani kwake Mbweni mjini Unguja kwa ajili ya kubadilishana mawazo.
Balozi wa Marekani
nchini Tanzania , Alfonso
Lenhardt ameahidi nchi yake itaunga mkono juhudi za Zanzibar
kuwa na mipango madhubuti ya uokoaji wakati yanapotokea majanga, ili kunusuru
maisha ya watu pale inapotokea hali kama hiyo.
Amesema msaada wa
Marekani utaelekezwa zaidi kuiwezesha Zanzibar
kuwa na mfumo wa kisasa wa mawasiliano utakaosaidia kujua eneo la tukio na
kumudu kufika kwa haraka, kwa nia ya kuokoa maisha ya watu wengi zaidi
iwezekanavyo.
Balozi Alfonso amesema
hayo leo alipokuwa na mazungumzo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar , Maalim Seif Sharif Hamad huko nyumbani kwake
Mbweni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar
kuzungumzia tukio la kuzama kwa meli ya MV. Skagit ,
pamoja na mambo mengine mbali mbali. “Msaada huu wa kuepusha maafa wakati
yanapotokea majanga, utakuwa ni kwa Tanzania nzima, lakini tutahakikisha
Zanzibar inanufaika nao na inajijengea uwezo wa kuokoa maisha ya watu wake,
wakati wa maafa kama haya ya kuzama kwa meli na mengineyo”, aliahidi Balozi
Lenhardt.
Hata hivyo, Balozi huyo
wa Marekani alisifu mshikamano wa wananchi wa Zanzibar
pamoja na serikali yao ,
wakati wa maafa ya kuzama kwa MV. Skagit mwezi
uliopita, hali ambayo ilisaidia kuokolewa baadhi ya watu waliokuwemo kwenye
meli hiyo.
Naye, Makamu wa Kwanza
wa Rais wa Zanzibar , Maalim Seif Sharif Hamad
amekaribia azma hiyo ya Marekani kuisaidia Zanzibar katika kukabiliana na majanga mara
tu yanapotokea. Katika hatua nyengine Balozi Lenhardt ameisifu Zanzibar kwa hatua kubwa iliyoweza kufikia
kudhibiti ugonjwa wa Malaria ambao umekuwa ukisababisha vifo vya watu wengi
wakiwemo watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.
Balozi huyo amesema Zanzibar imejijengea heshima na hivi sasa imekuwa mfano
Duniani na wataalamu kutoka sehemu mbali mbali wanakuja Zanzibar kujifunza mbinu za kutokomeza
ugonjwa huo. Akizungumiza mafanikio hayo, Maalim Seif alisema suala la elimu
kwa wananchi juu ya kutokomeza ugonjwa huo limechangia kwa kiasi kikubwa kuwa
na uelewa wa hali ya juu kujilinda wasipate maradhi hayo.
Maalim Seif alisema
baada ya wananchi walio wengi kuelewa mbinu za kujikinga na Malaria imekuwa
rahisi kuweza kuzitumia njia wanazoshauriwa na wataalamu.
Alizitaja baadhi ya
mbinu hizo kuwa ni matumizi ya vyandarua, kupuliziwa dawa kwenye nyumba zao,
kuweka mazingira yao
katika hali ya usafi pamoja na kufika kwenye vituo vya afya kwa uchunguzi na
kutibiwa mara wanapoona dalili za kuwa na maradhi hayo.
Balozi huyo wa Marekani
pia amemhakikishia Makamu wa Kwanza wa Rais kuwa nchi hiyo itaendelea kufanikisha
miradi mbali mbali inayofadhiliwa na Marekani hapa Zanzibar .
Miongoni mwa miradi hiyo
ni utandikaji wa laini kuu ya umeme kutoka Dar es Salaam hadi Fumba kupitia
chini ya bahari na ujenzi wa barabara tafauti, ambayo yote ipo katika hatua
nzuri za utekelezaji.
Wakati huo huo Makamu wa
Kwanza wa Rais jana alijumuika katika futari iliyoandaliwa na masjid Iman
iliyoko mbweni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar .
Futari hiyo
iliwajumuisha wananchi mbali mbali wanaosali katika msikiti huo pamoja na
viongozi kadhaa wa dini na siasa wakiwemo Sheikh Habib Ali Kombo na Makamu
Mwenyekiti wa CUF Machano Khamis Ali.
Picha, Habari na Salmin Said-Ofisi ya
Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar
No comments:
Post a Comment