Monday, August 6, 2012

Waziri mkuu Syria ajiuzulu...


Riad Hijab


Waziri mkuu wa Syria Riad Hijab, amejiuzulu kutoka kwa serikali ya rais wa Bashar al-Assad na kujiunga na harakati za mageuzi.
Bwana Hijab aliteuliwa kwa wadhifa huo chini ya miezi miwili iliyopita na kujiuzulu kwake kunamfanya yeye kuwa afisaa wa ngazi ya juu zaidi kujiuzulu kutoka kwa serikali ya Assad tangu harakati za mageuzi kuanza mwezi Machi mwaka jana.
Inaarifiwa familia yake pia imekimbia kutoka Syria.
Riad ambaye ni wa madhehebu ya Suni, anatoka eneo la Deir al-Zour mashariki mwa Syria, eneo ambalo limenaswa katika vita vinavyoendelea vya kumng'oa mamlakani rais Assad.
Msemaji wake , Mohammed el-Etri amesema kuwa yeye na familia yake wako salama nchini Jordan.
Duru zinasema kuwa hatua hii ni dalili ya serikali ya Assad kuonekana dhaifu na kuwa hata wakuu wa majeshi wanaaza kuhisu shinikizo hizi za kuondoka.
Habari kutoka kwa waasi zinasema mawaziri wengine wawili wa serikali ya rais Assad pia wameasi.

Lakini wanasema waziri wa fedha, Mohammad Jalilati alikamatwa alipojaribu kutoroka.
Taarifa hiyo imekanushwa na televisheni ya serikali ambayo imetangaza mahojiano ya simu na Bwana Jalilati, akisema anaendelea na kazi kama kawaida.
Mwezi mmoja uliopia, Brigedia Generali Manaf Tlas, aliyesemekana kuwa mshirika wa karibu sana wa rais Assad pia alijiuzulu.
Majenerali wengine thelathini wamesemekana kuvuka mpaka na kuingia nchini Uturuki.
Hata hivyo taarifa tete zinasema kuwa waziri mkuu huyo alifutwa kazi ingawa serikali ya Syria haikutoa taariza zozote kuelezea hatua ya kumfuta kazi.
Omar Ghalawanji, ndiye atachukua nafasi yake. Taarifa za mapema za awali zlisema kuwa shambulizi la bomu lilifanywa katika mojawapo ya vituo vya televisheni na redio vya serikali,mjini Damascus, na kuwajeruhi watu watatu.
Chanzo: BBC Swahili.

No comments:

Post a Comment