HOTUBA YA MHE. DKT.
JAKAYA MRISHO KIKWETE,
RAIS WA JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA ,
KWA WANANCHI, TAREHE 31
JULAI, 2012
Ndugu Wananchi;
Naomba nianze kwa kuomba
radhi kwa kutoa hotuba ya mwisho wa mwezi wa saba, leo tarehe 01 Agosti, 2012
badala ya jana tarehe 31 Julai, 2012. Hii ni kwa sababu ya msiba uliotukuta
katika familia na mimi kwenda Lindi kushiriki maziko ya marehemu wetu. Tofauti
na miezi iliyopita leo, pamoja na hotuba ya kawaida ya mwisho wa mwezi nimetoa
fursa kwa Wahariri wa vyombo vya habari nchini kuniuliza maswali nami kujibu.
Kwa upande wangu nina mambo matatu ambayo nitayazungumzia leo.
Ajali ya Kuzama kwa Meli
ya MV SKAGIT
Ndugu Wananchi;
Jambo la kwanza ni ajali
ya Meli ya MV SKAGIT iliyotokea tarehe 18 Julai, 2012. Meli hiyo ilikuwa na
watu 290, wakiwemo mabaharia 9,abiria watu wazima 250 na watoto 31. Juhudi za
uokoaji zilianza mara baada ya taarifa ya kuzama kwa meli hiyo kupatikana.
Maofisa na askari wa JWTZ, Polisi na KMKM walishiriki pamoja na meli na watu
binafsi katika uokoaji. Waokoaji walifanikiwa kuwapata ndugu zetu146 wakiwa hai
na maiti 126 hadi tarehe 27 Julai, 2012. Kwa maana hiyo basi, watu 18 hawajulikani
walipo na inahofiwa kuwa nao pia hawako hai. Huenda wamezama pamoja na meli au
walizama baharini lakini miili yao
haikuweza kupatikana.
Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi
hii kurudia kutoa mkono wa rambirambi na pole nyingi kwa wale wote waliopoteza
ndugu, jamaa na marafiki katika ajali ile. Nampongeza sana Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein na
viongozi wenzake wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwa kazi kubwa na
nzuri waliofanya kuongoza juhudi za uokoaji pamoja na huduma walizotoa kwa
waliokolewa, waliojeruhiwa na waliofariki. Kwa wale ambao walikuwa wenyeji wa
Unguja na Pemba , SMZ ilitoa sanda na
usafirishaji wa maiti mpaka makwao kwa mazishi. Kwa wale wasiokuwa na ndugu
Serikali ilibeba jukumu la kuwazika kule Kama ,
Kusini Unguja.
Natoa pongezi za pekee
kwa wale wote walioshiriki katika uokoaji kwani juhudi zao ziliwezesha ndugu
zetu wengi kusalimika na maiti nyingi kupatikana.
Ndugu Wananchi;
Kutokea kwa ajali ile
kumetonesha jeraha la huzuni, majonzi na mashaka makubwa yaliyolipata taifa
letu miezi 11 iliyopita kufuatia ajali ya kuzama kwa meli ya MV Spice Islander.
Katika mkutano maalum wa Baraza la Usalama wa Taifa niliouitisha tarehe 20
Julai, 2012 kuzungumzia ajali ya MV SKAGIT tulifanya mapitio ya utekelezaji wa
maagizo yetu ya mkutano wa tarehe 11 Septemba, 2011 kufuatia ajali ya MV Spice
Islander. Kwa ujumla tumeridhika kuwa utekelezaji umekuwa mzuri kwa upande wa
mamlaka zinazohusika na usafirishaji majini yaani SUMATRA ,
Zanzibar Maritime Authority na mamlaka za Bandari za nchi zetu mbili.
Ushirikiano baina ya mamlaka hizo sasa ni mzuri kwa mambo yote muhimu ambayo
Baraza liliagiza wafanye hivyo. Pamoja na hayo Baraza limetaka ushirikiano huo
uzidishwe na kuimarishwa.
Kwa mfano, Baraza
limefurahishwa na kupongeza kitendo cha mamlaka hizo kutumia Dar es Salaam
Maritime Institute kwa ushauri kuhusu ubora wa meli na huduma za usafirishaji
majini. Baraza limeagiza vyombo hivyo viwe na hadidu za rejea zinazofanana kwa
vigezo vya ubora ili nchi yetu iwe na viwango vinavyofanana vya ubora wa meli
na huduma za usafirishaji baharini kwa pande zetu mbili za Muungano. Bahari ni
moja na vyombo vinahudumia watu wale wale, kuwa na vigezo tofauti vya ubora wa
meli na viwango vya huduma ni jambo lisilostahili kuwepo tena, ni la hatari.
Baraza pia limeagiza pawepo na ukomo wa umri wa meli zilizokwishatumika
zinazoruhusiwa kutumika hapa nchini.
Aidha, Baraza limerudia
kuagiza pawepo na usimamizi makini zaidi kuhusu upakiaji wa mizigo na abiria.
Mamlaka husika, yaani SUMATRA , ZMA na maofisa
wa bandari wahakikishe kuwa uwezo wa meli uliohakikiwa na kutambuliwa
unaheshimiwa ipasavyo. Pia, meli zikaguliwe mara kwa mara na vigezo vifanane.
Ndugu Wananchi;
Pamoja na hayo, Baraza
la Usalama wa Taifa limeona kuwa wakati umefika kwa Serikali yetu kuwa na Coast
Guards, yaani kikosi maalum cha uokoaji na usalama majini. Aidha, Baraza
limetaka hatua za makusudi zichukuliwe kuimarisha KMKM na Police Marines.
Mwisho, Baraza lilipongeza uamuzi wa SMZ wa kuunda Tume ya kuchunguza ajali ile
kama ilivyofanya wakati wa ajali ya MV Spice
Islander.
Utafutaji na Uchimbaji
Gesi Nchini
Ndugu Wananchi,
Jambo la pili
ninalopenda kulizungumzia leo ni kuhusu maendeleo ya sekta ya gesi asili
nchini. Juhudi za kutafuta mafuta nchini zilianza mwaka 1952 na mwaka 1954
wakati kampuni ya BP ilichimba kisima cha kwanza kule Mafia. Bahati mbaya
kisima hicho hakikuzaa matunda yaliyotarajiwa na juhudi za utafutaji mafuta
zikafifia kabisa mwanzoni mwa miaka ya 1960. Miaka kumi baadae, juhudi hizo
zilianza upya na kuendelea kwa kiwango na kasi za namna mbalimbali hadi sasa.
Katika miaka ya hivi karibuni juhudi zimekuwa kubwa na kuhusisha makampuni
kadhaa ya kimataifa yakiwemo makubwa na madogo.
Ndugu Wananchi;
Tangu mwaka 1954, mpaka
sasa visima 61 vimechimbwa, kati ya hivyo, gesi asili imegunduliwa katika
visima 22, visima 14 vya nchi kavu na maeneo ya maji mafupi na visima 8vya
bahari ya kina kirefu. Hatujabahatika kupata mafuta lakini tumefanikiwa kupata
gesi asili katika maeneo kadhaa baharini na nchi kavu katika mikoa ya Mtwara,
Lindi na Pwani.
Kwa mujibu wa taarifa
zilizopo kutokana na visima vilivyochimbwa mpaka sasa, akiba ya gesi asili
iliyopo nchini inakadiriwa kuwa kati ya futi za ujazo trilioni 25.4 – 28.9.
Yapo matumaini makubwa ya gesi nyingi zaidi kugundulika katika miaka michache
ijayo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba shughuli za utafutaji mafuta na hasa
gesi baharini zilizoanza mwaka 2004 kukiwa na kampuni moja sasa zipo 18. Baada
ya ugunduzi wa kwanza wa gesi mwaka 2010, shughuli za utafutaji sasa zimepamba
moto na zimekuwa na mafanikio. Naamini gesi nyingi zaidi itaendelea kupatikana.
Fursa za Maendeleo
Ndugu Wananchi;
Kwa kiasi cha gesi asili
kilichokwishagunduliwa na kwa matumaini yaliyopo ya gesi zaidi kupatikana
kunaifanya Tanzania
kuwa moja ya nchi za kutumainiwa duniani kwa upatikanaji wa gesi asili miaka
michache ijayo. Hali hiyo inaipa nchi yetu fursa kubwa ya kuweza kujiletea
maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii muda si mrefu kutoka sasa.
Gesi asili ni rasilimali
inayoweza kutumika kuzalisha mbolea na hivyo kusaidia katika kuendeleza kilimo
nchini kwa kurahisisha upatikanaji wake na kuwa ya bei nafuu. Gesi asili
inaweza kutumika kuzalisha umeme na hivyo kuiwezesha nchi kupata umeme wa kutosha
na kuwepo ziada ya kuuza nje. Hivi sasa, katika gridi ya taifa megawati 350za
umeme zinatokana na gesi asili na hata lengo letu la kuzalisha megawati 3,500
ifikapo maka 2015 tunategemea zaidi gesi asili kuwezesha hilo kutimia. Ujenzi
wa bomba la gesi kutoka Mtwara kuja Dar
es Salaam una shabaha hiyo.
Ndugu Wananchi;
Vile vile, gesi asili
inaweza kutumika kutoa nishati viwandani badala ya kutumia mafuta na hivyo
kupunguza gharama za uzalishaji. Watu majumbani wanaweza kutumia gesi asili
kupikia hivyo kupunguza matumizi ya umeme, mafuta, mkaa na kuni. Inapunguza
gharama za maisha na kusaidia kuhifadhi mazingira kwa kupunguza ukataji wa
miti. Ni kutokana na kutambua ukweli huo ndiyo maana TPDC inatekeleza mradi wa
kutengeneza gridi ya mabomba ya kusambaza gesi majumbani katika jiji la Dar es
Salaam.
Jambo lingine muhimu
kuhusu rasilimali hii ni kwamba tukiuza nje gesi nchi yetu itapata mapato mengi
tena ya fedha za kigeni. Kwa vile gesi ni nyingi mapato ya Serikali
yataongezeka sana ,
hivyo kuijengea uwezo wa kutimiza majukumu yake vizuri zaidi. Kama
matumizi yatakuwa mazuri, gesi asili itakuwa kichocheo kikubwa cha kukuza
uchumi wa nchi. Maendeleo ya haraka yatapatikana na hivyo kusaidia kuwaondoa
wananchi wengi kutoka katika lindi la umaskini tulionao sasa.
Changamoto Muhimu
Ndugu Wananchi;
Pamoja na ukweli kwamba
kuwa na gesi asili nyingi kunaipa nchi yetu fursa kubwa ya kujiletea maendeleo,
zipo pia changamoto zake. Hatuna budi kuzitambua na kuzitafutia ufumbuzi ili
gesi iweze kunufaisha ipasavyo nchi yetu na watu wake. Changamoto zipo nyingi
lakini kubwa zipo za namna tatu.
Changamoto ya kwanza ni
ile ya kujenga uwezo wetu wenyewe wa kudhibiti shughuli zinazofanywa na
makampuni ya mafuta ili tuhakikishe kuwa tunapata malipo yanayostahili.
Inatulazimu tuwe na wataalamu wetu wazalendo wa fani za taaluma zihusuzo gesi kama vile uhandisi, kemia, jiofizikia, uhasibu, ukaguzi
na sheria. Tusipojenga uwezo wetu wenyewe kwenye maeneo hayo kuna hatari ya
kudhulumiwa na kupata hasara. Pengine ipo haja ya kuwa na chombo maalum kwa
ajili hiyo kama tulivyofanya kwa mafanikio kwa
upande wa dhahabu.
Changamoto ya pili ni
ile ya kupata Watanzania wengi wenye ujuzi na taaluma zinazohitajika na soko la
ajira la sekta ya gesi. Tusipofanya hivyo makampuni yataajiri watu hao kutoka
nje na hivyo kufanya Watanzania kutokunufaika na fursa za ajira zilizopo.
Ndugu Wananchi,
Kwa changamoto hizi
mbili, jawabu lipo kwenye elimu na mafunzo tunayotoa kwa vijana wetu katika
shule, vyuo vya ufundi na vyuo vya elimu ya juu. Kwanza
kabisa lazima tuboreshe elimu ya sayansi na hisabati katika shule zetu za
msingi na sekondari. Katika vyuo vya ufundi tutoe mafundi mchundo wa taaluma
zinazohitajika na tasnia ya gesi na mafuta. Hivyo hivyo kwa upande wa vyuo
vikuu nako wafundishe wataalamu wa fani zinazohitajika kama vile utafutaji wa
gesi na mafuta, uendelezaji wa mafuta na gesi, uchumi na biashara ya mafuta na
gesi, uhasibu na ukaguzi wa mafuta na gesi pamoja na sheria za mafuta na gesi
na mikataba ya utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuwahakikishia
kuwa tayari tumejipanga kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo. Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam kinajiandaa kuanza kutoa mafunzo ya Chemical and Environmental
Lab for Oil and Gas na fani ya Exploration and Production Software
Technologykatika mwaka huu wa masomo. Chuo cha Madini Dodoma kitaanza kutoa
mafunzo ya diploma ya Petroleum Geoscience kuanzia Septemba mwaka huu. Chuo
Kikuu cha Dodoma , Chuo cha Sayansi na Teknolojia
cha Nelson Mandela Arusha, na Chuo cha Teknolojia cha Mbeya na kile cha Dar es Salaam pia
wameanza kufundisha mitaala hiyo. Aidha, VETA Makao Makuu na VETA Mtwara nao
wanafundisha masomo yahusuyo gesi. Wizara ya Nishati na Madini itawadhamini
wanafunzi 50 kutoka Mkoa wa Mtwara kwenda kupata mafunzo hayo ya gesi asili
katika chuo cha VETA Mtwara.
Ndugu Wananchi;
Wizara ya Nishati na
Madini pia inatekeleza mpango mkakati wa kuwapata wataalamu wa sekta hiyo kati
ya 40-50 kati ya sasa na mwaka 2016. Taaluma zinazotiliwa mkazo ni Petroleum
Geoscience, Petroleum Geophysics, Petroleum Geochemistry, Petroleum
Engineering, Petroleum Modeling, Oil and Gas economics, Oil and Gas Accounting
and Auditing na Oil and gas Legal Regimes and Contract Negotiations. Kwa upande
wake, Serikali itatoa upendeleo maalum kwa kulipia gharama zote za mafunzo ili
tuweze kuwapata wataalamu hawa mapema iwezekanavyo. Nawaomba vijana wetu
wachangamkie fursa hizi za masomo na watakapohitimu mafunzo wawe tayari
kuitumikia nchi yetu kwa bidii.
Kujenga Uwezo Wetu wa
Kutumia Mapato ya Gesi
Ndugu Wananchi,
Changamoto nyingine
kubwa sana ni
ile ya kuhakikisha kuwa mapato yatokanayo na gesi yanatumika vizuri na kwa
manufaa ya taifa na watu wake. Lazima tuanze sasa kufikiria na kujipanga kwa
ajili hiyo. Si vyema tukangojea mpaka hapo mapato yatakapoanza kupatikana ndiyo
tufikirie na kutengeneza mfumo mzuri wa kusimamia na kutumia mapato yatokanayo
na gesi. Tutakuwa tumechelewa, watu laghai na waovu watakuwa wameanza kunufaika
hivyo watakuwa wagumu kutengeneza mfumo utakaowanyima fursa ya kuliibia taifa.
Jambo hili ni muhimu sana kufanya kwani ipo
mifano hai ya nchi zenye rasilimali nyingi za mafuta na gesi lakini nchi na
wananchi wake hawanufaiki sawia. Mauzo yanafanyika na fedha nyingi kupatikana
lakini manufaa kwa nchi na watu wake ni madogo au hayapo kabisa. Wanaonufaika
ni viongozi na baadhi ya maofisa wa umma wanaohusika na usimamizi wa shughuli
zihusuzo rasilimali hizo. Na, hata sisi tunaweza kujikuta katika hali hiyo kama tusipojipanga vizuri sasa ambayo badala ya
rasilimali kuwa baraka zinageuka kuwa balaa au hata laana.
Ndugu Wananchi;
Zipo nchi duniani ambazo
zina usimamizi mzuri wa mapato ya rasilimali za mafuta na gesi na kuleta baraka
na neema kwa taifa na watu wake. Nchi hizo zimeweza kuhifadhi na kutumia vizuri
mapato yake kukuza uchumi wa nchi kwa jumla na kuboresha upatikanaji wa huduma
za kiuchumi na kijamii kwa watu. Matokeo yake ni watu wa nchi hizo kuishi
maisha yaliyo bora kuliko walivyokuwa kabla ya kupatikana kwa rasilimali hizo.
Lakini, hii imewezekana kutokana na usimamizi mzuri na matumizi mazuri ya
mapato yatokanayo na mafuta na gesi.
Tumeamua kujifunza kutoka
nchi za wenzetu waliofanikiwa ili na sisi tunufaike. Na sisi tunajiandaa
kutengemeza Sera ya Gesi Asili na kurekebisha Sheria ya Utafutaji na Uzalishaji
wa Mafuta na Sheria ya Menejimenti ya Mapato ya Serikali yatokanayo na gesi
zitakazotoa majibu hayo na kuliwezesha taifa kuwa na mfumo mzuri wa usimamizi
wa utafutaji na uchimbaji wa gesi asili pamoja na usimamizi na matumizi mazuri
ya mapato yatokanayo na gesi hiyo. Wapo wenzetu kwa mfano, wanacho kitu
kinachoitwa Sovereign Funds ambapo mapato yote huhifadhiwa na baadae hutolewa
kwa utaratibu maalum.
Tunataka tujifunze
kutoka kwao ili na sisi tutengeneze chombo chetu cha namna hiyo ili tunufaike.
Ndugu Wananchi;
Mambo hayo tumeshaanza
kuyafanyia kazi. Katika mazungumzo yangu na baadhi ya wakuu wa nchi rafiki na
mashirika ya maendeleo ya kimataifa, nimewasilisha maombi ya kusaidiwa na
kushirikiana kwa mambo mawili. Kwanza kwa
kuwawezesha Watanzania kupata mafunzo ya haraka kwa wataalamu watakaosaidia
kusimamia shughuli za utafutaji, uendelezaji na biashara ya gesi asili nchini.
Pili, watusaidie kupata watu wenye ujuzi na uzoefu ili watushauri kuhusu namna
ya kutengeneza mifumo bora ya kusimamia na kutumia mapato ya gesi kwa mujibu wa
mifano ya wenzetu waliofanikiwa.
Nafurahi kwamba maombi
yetu yamepokelewa vizuri na nchi zote na mashirika yote ya kimataifa
tuliozungumza nao. Baada ya muda si mrefu kazi itaanza.
Mgomo wa Walimu
Ndugu Wananchi;
Jambo la tatu na la
mwisho ni mgomo wa walimu. Pengine ni mapema kusema kwa vile kesho Mahakama
itaamua kuhusu shauri hilo .
Lakini napenda kuwahakikishia walimu kuwa tunawajali, tunawathamini na kutambua
mchango wao muhimu kwa taifa letu. Wakati wote tumekuwa tunashughulikia madai
ya haki zao na malimbikizo mbalimbali. Madai ya safari hii ni makubwa mno,
yametuzidi kimo. Athari za kuyatimiza yalivyo yataifanya bajeti ya Serikali
kutumia asilimia 75kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa Serikali na kubakiza asilimia
25kwa kuendeshea Serikali na kutimiza majukumu ya maendeleo kwa wananchi.
Haitakuwa sawa. Ndiyo maana tumeshindwa kuelewana walipokataa rai hiyo na wao
kusisitiza kugoma.
Wakati tunaendelea
kusubiri uamuzi wa Mahakama, nina maombi mawili kwa walimu: Moja,
wasiwalazimishe walimu wasiotaka kugoma wafanye hivyo, wawaache waendelee na
kazi. Pili, wasitumie watoto isivyostahili kujenga hoja zao. Nawasihi warudi
kwenye meza ya mazungumzo.
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kumaliza hotuba
yangu naomba nitumie fursa hii kuwatakia Waislamu wote nchini kheri na baraka
tele kwa swaumu ya mwezi mtukufu wa Ramadhan. Wakati wote, mjiombee wenyewe kwa
Mwenyezi Mungu awajaalie toba na malipo mema katika mfungo huu. Mkumbuke pia
kuiombea nchi yetu amani, upendo na mafanikio mema.
Baada ya maneno hayo,
naomba sasa niishie hapo. Nawashukuru sana
kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment