Mwenyekiti wa MISA-TANZANIA Mohammed Tibanyendera.
TAARIFA KWA UMMA
Taasisi ya vyombo vya
habari Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania MISA-Tanzania) inasikitika kuarifu
umma wa watanzania kwamba inapinga vikali kitendo cha serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania
kupitia Ofisi ya Msajili wa Magazeti Tanzania Bara kulifungia kutochapishwa kwa
muda usiojulikana gazeti la MwanaHalisi kuanzia tarehe 30 Julai 2012.
Katika taarifa
iliyotolewa na serikali kupitia tangazo lake lililochapishwa kwenye magazeti
mbalimbali hapa nchini na kunukuu kutolewa kwa amri hiyo kupitia gazeti la
serikali (Government Notice) toleo namba 258 la tarehe 27 Julai 2012, serikali
imeeleza kama ifuatavyo:
“Serikali imeamua
kulifungia kutochapishwa kwa muda usiojulikana gazeti la MwanaHalisi kwa mujibu
wa sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, kifungu namba 25 (i), adhabu hiyo itaanza
tarehe 30 Julai 2012”
Aidha, tamko hilo la serikali limeeleza pia kuwa sababu za msingi za
kulifungia gazeti hilo ni kufuatia machapisho
mbalimbali ya gazeti hilo
kwenye toleo Na. 302, Na. 303 pamoja na toleo Na. 304 yote yakiwa ya mwezi
Julai 2012 pamoja na machapisho mengine yaliyotangulia. Serikali imeeleza kuwa
machapisho hayo yamekuwa “yakichapisha habari na makala zenye kueneza na
kujenga hofu kwa jamii”
Hata hivyo, serikali
haikubainisha ni habari zipi katika machapisho hayo ambazo zinaeneza na kujenga
hofu kwa jamii. Kitendo hicho cha kutobainisha habari husika kinatufanya sisi kama wanahabari na watetezi wa haki ya kupata taarifa
pamoja na uhuru wa vyombo vya habari nchini na katika kanda ya kusini mwa
Afrika kutoridhia maamuzi ya serikali kwani yamehusisha masuala ambayo
hayakuwekwa bayana.
Ni kwa mashaka makubwa
ambayo yanatokana na tamko husika la serikali kwa kutumia maneno yafuatayo:
“Kuanzia sasa serikali
haitasita kuchukua hatua dhidi ya vyombo vya habari ambavyo kwa makusudi
vitatoa taarifa za uchochezi ambazo zitahatarisha hali ya amani na utulivu
uliopo nchini mwetu”
MISA–Tanzania
inasikitishwa na kauli hiyo kwani kauli hiyo ni kudhihirisha matumizi mabaya ya
sheria zilizopo katika kukandamiza uhuru wa kupata taarifa na uhuru wa vyombo
vya habari kinyume na matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya
mwaka 1977 ibara ya 18 (b) na (d) kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2005.
Haki ya kutafuta, kupata
na kutoa taarifa ni haki ya msingi ya kila binadamu na imetambuliwa hivyo na
Katiba ya Tanzania .
Haki hii imetambuliwa pia na mikataba mbalimbali ya Kimataifa ambayo Tanzania
imeiridhia bila masharti yoyote.
Kama kweli kuna taarifa
za uchochezi zilizochapishwa na gazeti la MwanaHalisi na kuhatarisha amani na
utulivu wa nchi, ni vyema serikali ingebainisha taarifa hizo kwenye chapisho
husika na siyo kuorodhesha machapisho mbalimbali kama
sababu yake ya kulifungia gazeti. Hata hivyo, mamlaka ya serikali kufungia
gazeti kupitia msajili wa magazeti ni ukiukwaji wa misingi ya haki za binadamu
na matumizi makubwa ya madaraka.
Ni kwa sababu hizo
kwamba Ripoti ya Haki za Binadamu iliyowahi kuandaliwa na kutolewa na Tume
maalumu iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kujulikana
kama Tume ya Jaji Nyalali mwaka 1992 ilibainisha sheria ya Magazeti ya mwaka
1976 kuwa ni miongoni mwa sheria arobaini ambazo zinakandamiza haki za binadamu
nchini. Sheria hiyo haina budi kufutwa kwenye vitabu vya sheria za nchi hii.
Kitendo cha kulifungia
gazeti la MwanaHalisi kwa muda usiojulikana kinaweza kusababisha hofu kubwa kwa
watetezi wa haki za binadamu na wanahabari kwa ujumla. Kitendo hicho kinafuatia
kile cha kuwakamata na kuwaweka rumande (Oysterbay Polisi) wanaharakati zaidi
ya kumi kwa tuhuma mbalimbali ikiwamo kuandamana kufuatia mgomo wa Madaktari
mnamo tarehe 9 mwezi Februari 2012.
MISA –Tanzania
inalaani vikali matumizi mabaya ya Dola katika kunyamazisha wanahabari
wanapojaribu na kuthubutu kufuatilia matukio mbalimbali na kuarifu umma kuhusu
yale waliyoyafanyia kazi kwa kina. Ni rai yetu kwa serikali kuwa ni vyema wabainishe
taarifa mahsusi zilizopelekea maamuzi ya kufungia gazeti la MwanaHalisi ili
kutuondolea hofu sisi tunaotetea haki na uhuru wa vyombo vya habari. Kuendelea
kuficha taarifa husika ni kuendelea kuikanyaga Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ,
1977 (ibara ya 18) kupitia kivuli cha Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 ambayo
kimsingi imepitwa na wakati na haiwezi kutumika kinyume na Katiba ya nchi.
Ni rai yetu pia kwa
serikali ya Tanzania kwamba
izingatie Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika yale yenye
kuhamasisha utoaji haki kuliko kujikita kwenye kifungu cha 30 cha Katiba hiyo
ambacho kimsingi kinaweka mipaka maalumu ya ukiukwaji wa haki za binadamu.
Mipaka hiyo haionekani kuzingatiwa na serikali katika kulifungia gazeti la
MwanaHalisi.
Kwa taarifa hii kwa
umma, tunaiomba pia serikali ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania kulifungulia gazeti la MwanaHalisi
mapema iwezekanavyo na bila masharti ili kuwawezesha watanzania kuendelea
kunufaika na taarifa zinazochapishwa na gazeti hilo ilmradi maadili ya uandishi wa habari
yazingatiwe. Hii ni haki ya msingi kwa kila mtu na ni vyema aione
ikitekelezeka.
Taarifa hii imetolewa na
kusaini hapa Dar es salaam leo tarehe 31 Julai 2012.
………………………….
Mohammed Tibanyendera
Mwenyekiti, MISA-TAN
No comments:
Post a Comment