BUNGE LISIZUIWE KUINGILIA KATI MGOGORO KATI YA WALIMU NA
WANAFUNZI DHIDI YA SERIKALI KWA KISINGIZIO CHA KESI KUWA MAHAKAMANI
Tarehe 1 Agosti 2012 niliieleza Ofisi ya Waziri Mkuu
kupitia swali langu la msingi bungeni kwamba serikali hutoa ruzuku
(capitation grants) kwa wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari za Umma
zikiwemo za Jimbo la Ubungo, japo utekelezaji wa sera husika huwa unasuasua
sana kwa kiwango kilichowekwa kutokulingana na mahitaji halisi ya wanafunzi;
viwango vinavyotengwa katika Bajeti ni chini ya vinavyotajwa kwenye Sera na
Fedha hazitolewi zote isipokuwa hutolewa kidogo kidogo na hazifiki kikamilifu
mashuleni; nikahoji ni lini serikali itarekibisha hali hiyo ili kuboresha
elimu nchini.
Ofisi ya Waziri Mkuu katika majibu yake imekiri kwamba
kweli viwango vya ruzuku kwa ajili ya uendeshaji wa shule za msingi na
sekondari havijafikiwa mpaka sasa na hata fedha zinazotengwa kwa mujibu wa
bajeti hazitolewi kwa kiwango kilichopitishwa na bunge kwa kile alichoeleza
kuwa ni makusanyo ya Serikali.
Niliuliza maswali mawili ya nyongeza; nilihoji ni lini
serikali itatekeleza sera husika kwa kuwa upungufu wa ruzuku kwa shule za umma
ni kati ya vyanzo vya kuporomoka kwa elimu kutokana na kuathiri uendeshaji wa
shule ikiwemo upatikanaji wa vifaa shuleni, na kwa kuwa kwenye vyombo vya
habari jana na leo kati walimu na wanafunzi wameeleza kwamba hali hiyo ni kati
ya sababu za mgomo unaoendelea hivyo nikata serikali itoe kauli bungeni ya
kuutafutia ufumbuzi mgogoro unaoendelea.
Hata hivyo Spika wa Bunge alimkataza Naibu Waziri asijibu
swali kuhusu mgogoro kati ya walimu na wanafunzi dhidi ya serikali na kutaka
kujibiwa kwa swali ya lini ruzuku itaanza kutolewa kwa kuzingatia viwango vya
sera hata hivyo serikali ilitaja kiwango cha fedha ya ruzuku kwa mwaka wa fedha
2012/2013 bila kueleza iwapo viwango kwa mujibu wa sera vitafikiwa kwenye ngazi
zote ikiwemo katika shule za msingi.
Kwa mara nyingine tena Bunge limezuia kupewa taarifa
kuhusu masuala hayo kwa kisingizio cha kesi kuwa mahakamani hatua ambayo
inadhihirisha kwa mara nyingine tena umuhimu wa kusikilizwa kwa rufaa
niliyokata tarehe 31 Julai 2012 ili suala la mgomo wa walimu, madai ya
wanafunzi na hatma ya sekta ya elimu lijadiliwe kwa dharura bungeni.
Nimefanya hivyo kwa niaba ya walimu, wanafunzi na wadau
wengine wa elimu katika Jimbo la Ubungo na Tanzania kwa ujumla ili bunge
lipewe fursa ya kutimiza wajibu wake wa kikatiba kuisimamia serikali itekeleze
madai ya walimu na kuepusha athari za migogoro inayoendelea katika shule za
umma nchini.
Tarehe 30 Julai 2012 kwa nyakati mbalimbali kumetolewa
miongozo na maamuzi na Mheshimiwa Naibu Spika Job Ndugai ya kukataa hoja kwa
mujibu wa Kanuni ya 47 ya kuahirishwa kwa Shughuli za Bunge kujadili
jambo la dharura la mgomo wa walimu na yatokanayo na mgomo huo kwa kutumia
kanuni ya 64 (1) (c) ya kanuni za bunge toleo 2007 ambayo inamkataza mbunge
kuzungumzia jambo lolote ambalo linasubiri uamuzi wa mahakama.
Nimewasilisha rufaa kwa mujibu wa kanuni ya 5 (4)
kueleza kutoridhika na uamuzi wa Naibu Spika wa kutumia kanuni ya 64 (1)
(c) kudhibiti Bunge kutumia uhuru na mamlaka yake kwa mujibu wa katiba ya nchi;
sheria ya haki, kinga na madaraka ya bunge na kanuni nyingine za Kanuni za
Kudumu za Bunge kwa sababu tatu.
Mosi, Suala la yatokanayo na mgomo wa walimu hususani hali
tete ya sekta ya elimu kwenye shule za umma haliko mahakamani, kilichopo
mahakamani ni mgogoro kati ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT) na serikali
kuhusu madai ya walimu:
Pili, hata masuala yanayosubiri uamuzi wa mahakama ambayo yamewekewa
masharti kwa mujibu wa kanuni 64 (1) (c) yanaweza kuruhusiwa kujadiliwa bungeni
kwa muongozo na utaratibu utakaowezesha majadiliano kufanyika bila kuingilia
uhuru wa mahakama kwa kuzingatia kanuni ya 5 (1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge.
Tatu; izingatiwe pia kuwa masuala yanayosubiri
uamuzi wa mahakama ambayo yamewekewa masharti kwa mujibu wa kanuni 64 (1) (c)
yanaweza kuruhusiwa kujadiliwa bungeni kwa muongozo na utaratibu utakaowezesha
majadiliano kufanyika bila kuingilia uhuru wa mahakama kwa kuzingatia kanuni ya
5 (1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge.
Kwa kuzingatia sababu nilizozieleza, nimeomba kamati ya kanuni
ibatilishe maamuzi yaliyofanyika na kutoa pia muongozo wa kikanuni; hivyo
nimeomba Katibu wa Bunge amtaarifu Spika kwa mujibu wa kanuni ya 5 (4) na
kuitisha kikao cha dharura cha kamati ya kanuni kwa mujibu wa kanuni ya 5 (5)
ya kanuni za Kudumu za Bunge na kulijulisha bunge kuhusu uamuzi utakaotolewa.
Wako katika kuwawakilisha wananchi,
John Mnyika (Mb)
Mbunge wa Jimbo la Ubungo, CHADEMA
01 Agosti, 2012
No comments:
Post a Comment