Maoni yangu katika Sekta ya Afya: Bajeti na uhalisia!
Jana tarehe 30 Julai 2012 baada ya Hotuba ya Waziri wa Afya ya
Ustawi wa Jamii kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara kwa mwaka wa fedha
2011/2012 na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha
2012/2013; Taarifa ya Kamati ya Huduma za Jamii kuhusu Wizara husika na Maoni
ya Kambi ya Upinzani nilitaka mjadala usiendelee mpaka kwanza wabunge tupewe
nakala ya ripoti ya Kamati ya Huduma za Jamii iliyoshughulikia mgogoro kati ya
Serikali na madaktari na kuandaa mapendekezo ya kuboresha Sekta ya Afya nchini.
Nilifanya hivyo kwa kunukuu Taarifa ya Kamati ya Huduma za Jamii
ambayo pamoja na kuwa mwezi Februari 2012 bunge lilikataliwa kujadili masuala
husika mpaka kwanza kamati hiyo ikapate ukweli wa pande zote mbili na
kuwasilisha mapendekezo kwa bunge, taarifa ya Kamati hiyo kuhusu bajeti
iliyowasilishwa jana haikueleza chochote nini kamati ilibaini baada ya kukutana
na wadau mbalimbali wa sekta ya afya wala haikueleza ni ushauri gani iliutoa
kwa serikali kuupatia ufumbuzi mgogoro uliokuwepo wala haikuwasilisha bungeni
mapendekezo yoyote yaliyotokana na kazi waliyopewa na bunge. Aidha, Nilinukuu
pia maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani ambayo yalieleza bayana kuwa mwezi Juni
yalitolewa majibu yasiyokuwa ya kweli bungeni kuwa Taarifa ya Kamati hiyo
iliwasilishwa bungeni.
Kufuatia hali hiyo, na kutokana na bajeti hiyo ya afya kuwa
finyu huku ikiwa na utegemezi wa fedha kutoka nje kwa ziadi ya asilimia 90 kwa
mwaka wa fedha 2012/2013 wakati ambapo katika mwaka wa fedha 2011/2012 kiwango
cha fedha ambazo wahisani walileta ni asilimia 36 pamoja na kuahidi kuchangia
zaidi ya 90 kwenye fedha za maendeleo; hali ambayo itaendeleza migogoro kwenye
sekta ya afya.
Nikataka ili bunge liweze kuisimamia serikali kushughulikia
vyanzo vya migogoro kwenye sekta ya afya nchini; Taarifa ya Kamati ya Huduma za
Jamii iliyoshughulikia madai ya madaktari iwasilishwe na kujadiliwa bungeni,
majibu ya Naibu Spika aliyoyatoa ni kwamba taarifa hiyo haiwezi kuwasilishwa
kwa bungeni kwa kuwa kuna kesi mahakamani baina serikali na Madaktari. Majibu
hayo yamenifanya niwakumbushe taarifa hii ambayo niliitoa tarehe 29 Julai 2012
ili wadau wa afya mshiriki katika kutaka hatua muafaka toka kwa Serikali na
Uongozi wa Bunge:
BUNGE LISIZUIWE KUTUMIA HAKI, UHURU NA MADARAKA YAKE KWA MUJIBU
WA IBARA ZA 63 NA 100 ZA KATIBA YA NCHI KUISIMAMIA SERIKALI KWA NIABA YA
WANANCHI KUHUSU HALI YA SEKTA YA AFYA NCHINI NA MGOGORO KATI YA SERIKALI NA
MADAKTARI WAKATI WA MJADALA WA BAJETI YA WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII
Tarehe 30 na 31 Julai 2012 Bunge litajadili Makadirio ya Mapato
na Matumizi ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kwa mwaka wa fedha 2012/2013.
Kwa zaidi ya miezi mitatu bunge limekuwa likizuiwa kutumia haki, uhuru na madaraka
yake kwa mujibu wa ibara za 63 na 100 za Katiba ya Nchi kuisimamia serikali kwa
niaba ya wananchi kuhusu hali ya sekta ya afya nchini na migogoro kati ya
Serikali na madaktari.
Hali hii ilianza mwezi Februari 2012 Bunge lilizuiwa kujadili
suala hilo kwa
kisingizio kwamba mpaka kwanza kamati ya bunge iende kukutana na wadau wote na
kuwasilisha taarifa bungeni; ripoti ambayo mpaka sasa haijawasilishwa. Hali hii
ikashamiri zaidi mwezi Juni na Julai mwaka 2012 ambapo bunge lilizuiwa kujadili
masuala husika kwa kisingizio kwamba kuna kesi mahakamani.
Kwa chanzo cha hali duni kwenye sekta ya afya nchini na migogoro
kati ya Serikali na madaktari ni udhaifu katika utekelezaji wa bajeti ya
serikali na ufinyu wa kiwango cha fedha kinachotengwa kwa ajili ya sekta husika
kwa ajili ya madawa, vifaa tiba na maslahi ya watumishi wa umma kwenye sekta
husika; mjadala kuhusu mapatio ya utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha
2011/2012 na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa
fedha 2012/2013 iwe fursa ya bunge kuingilia kati kutafuta ufumbuzi.
Hivyo, natoa mwito kwa wananchi na wadau wa Sekta ya Afya kutaka
ripoti ya Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii iliyoshughulikia suala hilo kuanzia mwezi Februari 2012 iwasilishwe bungeni iweze
kutumika kama rejea wakati wa mjadala husika.
Maelezo yaliyotolewa bungeni na Naibu Spika Job Ndugai kuwa taarifa hiyo
ilishawasilishwa bungeni hayakuwa ya kweli, kwa kuwa wabunge hatujapewa nakala
wala kujadili ripoti husika na kama mbunge
nimeomba nakala ya ripoti husika lakini imeendelea kufanywa kuwa siri.
Aidha, uongozi wa Bunge usiendelee kutumia visingizio vya suala
kuwa mahakamani badala yake
uliwezeshe bunge kutumia ipasavyo madaraka na mamlaka yake kwa mujibu wa katiba
na kanuni za bunge kuliwezesha bunge kujadili hali ya huduma za afya nchini na
kushughulikia chanzo cha mgogoro ulioendelea kati ya serikali na madaktari
wenye athari kwa nchi na maisha ya wananchi na hatimaye kuongeza bajeti kwa
Wizara ya Afya kwenye mwaka wa fedha 2012/2013.
Ni muhimu uongozi wa bunge ukazingatia kwamba maamuzi ya Spika,
Naibu Spika na Wenyeviti wa bunge kudhibiti mijadala kwa kisingizio cha masuala
kuwa mahakamani tayari nilishayakatia rufaa toka tarehe 3 Julai 2012 hivyo
kinachotakiwa katika hatua ya sasa ni kuitishwa kwa dharura kwa kikao cha
kamati ya kanuni kuweza kubatilisha uamuzi huo ili wabunge watumie uhuru wa
kikatiba wa ibara ya 100 kuwawakilisha wananchi katika kuisimamia serikali juu
ya masuala husika
Niliwasilisha rufaa hiyo kwa katibu ambayo inapaswa kujadiliwa
na kamati ya kanuni za bunge baada ya kutopokea majibu ya barua zangu mbili za
kumshauri Spika kurekebisha miongozo iliyotolewa awali kuliwezesha bunge
kutumia ipasavyo madaraka na mamlaka yake kwa mujibu wa katiba na kanuni za
bunge kuliwezesha bunge kujadili hali ya huduma za afya nchini, jaribio la
mauji ya Dkt. Ulimboka Steven na kushughulikia chanzo cha mgogoro unaoendelea
kati ya serikali na madaktari wenye athari kwa nchi na maisha ya wananchi.
Ikumbukwe kwamba tarehe 27, 28, na 29 Juni 2012, na tarehe 2, 3
na 4 Julai 2012 kwa nyakati mbalimbali kumetolewa miongozo, maamuzi, majibu na
Mheshimiwa Spika Anne Makinda, Mheshimiwa Naibu Spika Job Ndugai na Waheshimiwa
Wenyeviti wa Bunge Sylvester Mabumba Jenister Mhagama kwamba suala la madai ya madaktari
na mgogoro uliotokana na madai hayo ni masuala ambayo hayapaswi kujadiliwa
bungeni kwa kuwa kanuni ya 64 (1) (c) ya kanuni za bunge toleo 2007 inamkataza
mbunge kuzungumzia jambo lolote ambalo linasubiri uamuzi wa mahakama.
Katika rufaa yangu kwa kuzingatia masharti ya kanuni ya 5 (4)
niliwasilisha maelezo ya kutoridhika na maamuzi yaliyofanyika kwa sababu tatu
zifuatazo:
SABABU YA KWANZA ; Taarifa za Vyombo vya habari zimeeleza kwamba kesi iliyopo
mahakamani imefunguliwa dhidi ya Chama Cha Madaktari (MAT) na si Jumuiya ya
Madaktari Nchini pamoja na vyama vingine vya watumishi na wataalamu katika
sekta ya afya na masuala mengine ya sekta husika. Aidha, ukiondoa suala la
madai ya madaktari ambayo ni kati ya hoja zilizo mahakamani masuala mengine yanayoendelea
si sehemu ya madai yaliyopo mahakamani, mathalani hali ya hivi sasa ya kudorora
kwa huduma katika hospitali za umma nchini. Hivyo, Spika kukataza masuala
husika ni kinyume na kanuni 5 (1) na ni kuingilia masharti ya ibara ya 100 ya
katiba ya nchi yanayolinda na kuhifadhi uhuru wa mawazo na majadiliano katika
Bunge.
SABABU YA PILI; hata masuala
yanayosubiri uamuzi wa mahakama ambayo yamewekewa masharti kwa mujibu wa kanuni
64 (1) (c) yanaweza kuruhusiwa kujadiliwa bungeni kwa muongozo na utaratibu
utakaowezesha majadiliano kufanyika bila kuingilia uhuru wa mahakama kwa
kuzingatia kanuni ya 5 (1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge.
Kanuni ya 5 (1) inaeleza kuwa katika kutekeleza majukumu yake
yaliyotajwa na ibara ya 84 ya katiba, Spika ataongozwa na kanuni hizi na pale
ambapo kanuni hazijatoa mwongozo, basi spika atafanya kazi kwa kuzingatia
katiba, sheria nyingine za nchi, kanuni nyingine zilizopo, maamuzi ya awali ya
maspika wa Bunge pamoja na mila na desturi za mabunge mengine yenye utaratibu wa
kibunge unaofanana na utaratibu wa Bunge la Tanzania.
Kwa kuwa maneno “jambo lolote linalosubiri uamuzi wa mahakama”
hayajapewa tafsiri kwa mujibu wa kanuni, sijaridhika na miongozo ya Spika
iliyotafsiri maneno hayo kudhibiti bunge kujadili masuala niliyoyaeleza. Hivyo,
nimeiomba kamati ya kanuni itoe tafsiri sahihi kwa kuzingatia masharti ya Ibara
ya 100 ya Katiba na sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kwa kurejea pia
maamuzi ya awali ya maspika wa bunge pamoja na mila na desturi za mabunge
mengine yenye utaratibu wa kibunge unaofanana na utaratibu wa bunge la Tanzania.
Katika maelezo
ya awali nimeiomba kamati irejee nyaraka toka maktaba ya Bunge la Uingereza
ambalo lina utaratibu kama wetu wa kibunge (
“Separation of Powers- Standard Note: SN/PC/06053) ambayo katika ukurasa wa
saba imeeleza yafuatayo kuhusu kanuni hiyo ya kukataza majadiliano bungeni
kuhusu masuala yaliyo mahakamani ambayo kwa kiingereza huitwa “Sub Judice”:
“The Sub Judice rule is intended to defend the rule of the law
and citizens’ right to fair trial. Where an issue is awaiting determination by
the courts, that issue should not be discussed in the House in any motion,
debate or question in case
that should affect decisions of the court.
However, the
sub judice rules are not absolute: The chair of proceedings of the House of
Commons enjoys the discretion to permit such matters to be discussed. Morever, sub judice does not affect
the right of parliament to legislate on any matter.
The 1999 Joint Committee on Parliamentary Privilege explained
that sub judice rules are intended to “strike a balance between two sets of
principles. On the one hand, the rights of parties in legal proceedings should
not be prejudiced by discussion of their case in Parliament, and Parliament
should not prevent the courts from exercising their functions. On the other
hand, Parliament has a constitutional right to discuss any matter it pleases”
Maelezo hayo yanathibitisha kwamba bunge linaweza kujadili
masuala yaliyo mahakamani ilimradi mjadala huo usilenge kuathiri maamuzi ya
kesi iliyo mahakamani, na pia Spika anayo mamlaka ya kutoa uhuru wa majadiliano
kwa masuala yaliyo mahakamani bila kuingilia uhuru wa mahakama na kwamba kesi
kuwa mahakamani hakuwezi kulizuia bunge kutumia haki na madaraka yake ya
kikatiba.
SABABU YA TATU; Spika badala ya
kudhibiti mjadala huo bungeni kwa kutumia kanuni 64 (1) (c) angetoa muongozo wa
kuwezesha kutolewa kwa hoja ya kutengua kanuni kwa mujibu wa kanuni ya 150
kuruhusu mjadala kwa kuzingatia masharti ya ibara ya 63 (2) na Ibara ya 100 ya
katiba ya nchi.
HIVYO kwa kuzingatia sababu nilizozieleza niliomba kamati
ibatilishe maamuzi hayo yaliyofanyika, kutoa pia muongozo wa kikanuni na pia
itoe mapendekezo kwa Kamati ya Uongozi ya Bunge ili kurekebisha udhaifu wa
kuingiliwa visivyo kwa uhuru wa majadiliano bungeni na kuathiri haki, kinga na
madaraka ya bunge ya kuisimamia serikali kuhusu maslahi ya watumishi wa afya na
hali ya sekta ya afya nchini hata kwa masuala yaliyo mahakamani. Hata kamati ya
kanuni isipokutana na kushughulikia rufaa bado Spika wabunge anaweza kurejea
ushauri niliotoa kwake kwa maandishi kwa kutumia njia nne za kikanuni zilizo
kwenye mamlaka yake na ya bunge kuwezesha mjadala wa mapitio ya utekelezaji wa
bajeti kwa mwaka wa fedha 2011/2012 na makadirio ya mapato na matumizi ya
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa mwaka wa fedha 2012/2013 kushughulikia
vyanzo vya matatizo husika bila kuingilia maamuzi ya masuala yaliyo mahakamani.
Wenu katika kuwawakilisha wananchi,
John Mnyika (Mb)
29/7/2012
No comments:
Post a Comment