MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh amesema ofisi yake imeanza ukaguzi
wa tuhuma zinazomkabili Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania
(Tanesco), William Mhando.
Julai 14 mwaka huu, Bodi
ya Wakurugenzi ya Tanesco ilimsimamisha kazi Mhando na Naibu Mkurugenzi
Mtendaji wa Huduma za Shirika, Robert Shemhilu, Ofisa Mkuu wa Fedha, Lusekelo
Kassanga na Meneja Mwandamizi wa Ununuzi, Harun Mattambo kupisha uchunguzi wa
tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.
Utouh aliwaambia
waandishi wa habari Dar es Salaam
jana kwamba ofisi yake imekabidhiwa kazi hiyo na tayari imeshaanza na imefikia
pazuri. “Ni kweli suala hilo
nimeshakabidhiwa na kazi hii tayari imeshaanza na imefikia pazuri. Kikao cha
kwanza kimekaa Jumamosi iliyopita na mimi nimeshafika kuwahakiki maofisa wangu
wanaoshughulikia hilo ,”
alisema Utouh na kuongeza kuwa kazi hiyo inaweza kukamilika ndani ya siku 60
kuanzia sasa.
Tuhuma zilizopo
Tuhuma za ufisadi
Tanesco, zilianzia katika ripoti ya CAG ya mwaka huu ambayo ilionyesha gharama
za ununuzi ziliongezeka kwa mwaka jana, kutoka Sh300 bilioni hadi 600 bilioni.
Baada ya sakata hilo , Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma
(POAC), ilitaka hatua zichukuliwe dhidi ya Bodi na Watendaji wa Tanesco na
kuhoji ongezeko hilo
kubwa la gharama za ununuzi.
Lakini wiki mbili kabla
ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, bodi hiyo iliitisha kikao cha dharura
Julai 13, mwaka huu kujadili tuhuma mbalimbali dhidi ya menejimenti ya shirika hilo na kuamua kwamba
tuhuma dhidi ya Mhando ni nzito hivyo ni vyema zifanyiwe uchunguzi huru na wa
kina.
“Hivyo, Bodi iliazimia
pamoja na mambo mengine kama ifuatavyo:
Uchunguzi wa tuhuma hizo uanze mara moja kwa kutumia uchunguzi huru na
kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Mhandisi William Mhando ili
kupisha uchunguzi huo na kwa kuzingatia matakwa ya sheria za kazi nchini.”
“Pamoja na uamuzi huo,
Bodi imechukua hatua stahiki za kuhakikisha kwamba shughuli za utendaji na
uendeshaji wa Tanesco zinaendelea kama
kawaida,” ilisema taarifa hiyo.
Sakata hilo lilipamba moto bungeni wakati wa mjadala
wa Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, kwa 2012/13. Akiwasilisha Bajeti
hiyo, waziri wake, Profesa Sospeter Muhongo alisema mbali ya tuhuma za kupanga
mgawo wa umeme kama mkakati na kampuni za
mafuta, Mhando pia anadaiwa kuidhinisha zabuni ya kusambaza vifaa vya ofisi kwa
kampuni ya mkewe, Eva Mhando. Profesa Muhongo alisema zabuni hiyo ni zaidi ya
Sh800 milioni na kwamba, Eva alitumia kampuni ya Santa Clara na Mhando aliidhinisha pasipo
kutangaza mgongano wa kimasilahi. Tuhuma hizo na nyingine zilihusisha baadhi ya
wabunge na kumfanya Spika, Anne Makinda kuivunja Kamati ya Nishati na Madini
baada ya kutuhumiwa kuhusika na vitendo vya rushwa.
Chanzo:
No comments:
Post a Comment