WATU wanne wamekufa papo hapo na mmoja
kujeruhiwa vibaya baada ya malori mawili kugongana na kutumbukia bondeni katika
mteremko wa mlima kitonga wilayani Kilolo katika barabara kuu ya Iringa - Dar es Salaam .
Maroli hayo moja lenye shehena kubwa ya madini
aina ya shaba na lingine
lenye bidhaa mbalimbali za dukani yanalindwa vikali na askari Polisi wa wilaya
hiyo, ili kunusuru mali
hizo zisiibiwe.
Akizungumza katika eneo la ajali Mkuu wa
Kikosi cha Usalama Barabarani Taifa, Mohamed Mpinga alisema kwa masikitiko
kwamba ajali nyingi zinazoendelea kutokea nchini zimekuwa zikisababishwa na
uzembe wa madereva.
Tarifa kutoka kwa mashuhuda waliokuwepo
katika eneo la tukio zimedai kwamba, ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia jana
na kuwa chanzo cha ajali hiyo ni lori lenye namba za usajili T587 BGP aina la
Scania.
Mashaka Abdala alisema roli hilo lenye mali
mbali mbali za dukani lilikuwa limeharibika na kuegeshwa kando ya barabara hiyo
na liligongwa na lori lingine lenye namba za usajili T T319 BDG aina ya Scania
pia ambalo breki zake zilikataa wakati likitelemka katika mlima huo.
Akithibitisha vifo vya watu waliokuwemo
kwenye maroli hayo, Mpinga alisema taarifa za Polisi zimethibitisha watu wanne
kati ya sita waliokuwemo katika maroli hayo kufa hapo huku mmoja akijeruhiwa
vibaya na kukimbizwa katika hospitali ya mkoa wa Iringa.
Mbali na majina yao kutofahamika mara moja, mpaka tunakwenda
mitamboni maiti moja ilikuwa bado haijatolewa kutoka kwenye kibini ya moja ya
maroli hayo kilichopondwa na kufunikwa na kontena za maroli hayo, katika bonde
la mlima huo.
Taarifa za kipolisi zimedai kwamba katika
ajali hiyo kibini ya roli lilolokuwa limepakia shaba lilifunikwa na kontena za
maroli hayo baada ya kwa pamoja maroli hayo kutumbukia katika korongo la mlima
huo.
Ajali hiyo ni moja kati ya ajali nyingi
zinazoendelea kutokea mkoani Iringa huku ukiwa katika maandalizi ya kitaifa ya
kuadhimisha Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani.
Kamanda Mpinga aliwakumbusha madereva
kuzingatia sheria za barabarani na akahidi kwamba msako mkali wa wale
wanaokiuka sheria hizo utaanza kufanywa.
Mpinga alisema kikosi cha usalama
barabarani kitaweka utaratibu wa ukaguzi maalumu wa magari katika maeneo ambayo
ajali zimekuwa zikitokea mara kwa mara ikiwa ni pamoja na katika mlima huo.
No comments:
Post a Comment