Na Joachim Mushi,
Thehabari.com
BODI ya Mikopo ya Elimu
ya Juu nchini pamoja na Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) imewaengua zaidi ya
wanafunzi 3074 walioomba vyuo na mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka 2012/13.
Kwa mujibu wa taarifa
iliyotolewa na taasisi hizo kupitia mitandao yao
(website) Agosti 10 na 12, 2012 zaidi ya wanafunzi 3074 wameenguliwa katika
maombi yao kwa
kuwa na dosari mbalimbali.
Taarifa hiyo imeeleza
kuwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) pekee imeorodhesha zaidi ya
wanafunzi 2,649 ambao imebaini kuwa na mapungufu kadhaa katika maombi yao ya kupewa mikopo ya
vyuo.
Miongoni mwa makosa ama
dosari ambazo bodi imezibaini kwa walioenguliwa kwa sasa ni pamoja kukosekana
kwa vyeti vya kuzaliwa kwa muombaji, sahihi ya mdhamini/muombaji, kukosekana
kwa picha ndogo ya muombaji/mdhamini, kukosekana kwa sahihi za viongozi wa Serikali
za mitaa/vijiji kwa waombaji na nyaraka nyingine muhimu kwa waombaji.
Kwa upande wake TCU
imewaengua jumla ya waombaji 425 kwa dosari na makosa mbalimbali, ambayo
imeyabainisha katika taarifa yake.
Miongoni mwa dosari
ambazo zimetajwa na TCU kwa wanafunzi hao ni pamoja na baadhi yao kukosea namba
za vyeti vya masomo kwa vidato vya nne na tano (O’ level na A’ level Index
number), miaka ya kumaliza masomo (year of completion), mawasiliano sahihi kwa
muombaji (Contact information e.g. Mobile phone number, email address and
postal address) pamoja na uchaguzi wa masomo (Programme selected).
Waweza kuingia katika
linki hii hapo chini na kuona majina ya waliobainika kuwa na dosari anuai
katika maombi yao
kwa TCU http://www.tcu.go.tz
Pia waweza kutembelea
linki zifuatazo na kushuhudia majina ya waliobainika kuwa na dosari hizo katika
maombi yao kwa
bodi ya mikopo;-http://www.heslb.go.tz
Hata hivyo taasisi hizo
mbili zimetoa muda kwa walioenguliwa sasa kutokana na dosari hizo kurekebisha
na kutuma tena maombi yao
kupitia mitandao kwa mujibu wa maelekezo waliyotoa.
No comments:
Post a Comment