Serikali, kuanzia leo
tarehe 01 Agosti, 2012, imewavua hadhi ya ukimbizi wakimbizi 38,050 wa kutoka Burundi
wanaohifadhiwa katika kambi ya wakimbizi ya Mtabila iliyoko wilayani Kasulu
mkoani Kigoma.Uamuzi huu wa kuwavua hadhi ya ukimbizi umefanywa na Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi kwa Mamlaka aliyopewa chini ya
Kifungu cha 4 cha Sheria ya Wakimbizi.
Kufuatana na Sheria hiyo
mkimbizi anapoteza hadhi ya ukimbizi kama mazingira yaliyomfanya kuwa mkimbizi
yatakuwa hayapo tena, na atavuliwa hadhi hiyo kama
ataendelea kukaidi maagizo halali ya kumtaka kurejea kwao kwa hiari.
Hatua ya kuwavua hadhi
ya ukimbizi wakimbizi hawa imefikiwa baada ya Serikali za Tanzania na Burundi na Shirika la Umoja wa
Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) kujiridhisha kuwa hapakuwa tena na
sababu ya kuendelea kuwahifadhi wakimbizi hao baada ya hali ya amani kurejea
nchini mwao na hivyo kuwataka kurejea kwao.
Zoezi la kuwasaili
wakimbizi waliopo katika kambi ya wakimbizi ya Mtabila lilifanyika kuanzia
mwezi Septemba hadi Desemba mwaka 2011 kwa lengo la kubaini kama
walikuwepo wakimbizi wenye sababu za msingi za kuendelea kuwepo nchini, ambapo
ilibainika kuwa wakimbizi 38,050 hawakuwa na sababu za kuendelea kuwa
wakimbizi.
Kufuatia matokeo ya
zoezi hilo , Kikao cha Pande Tatu,
kilichojumuisha wawakilishi wa Serikali za Tanzania
na Burundi na Shirika la
Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), kilifanyika jijini Bujumbura nchini Burundi tarehe 22 Februari, 2012 na
kukubaliana kwa pamoja kuifunga kambi ya Mtabila ifikapo tarehe 31 Desemba,
2012.
Baada ya kuwavua hadhi
ya ukimbizi, raia hawa wa Burundi
sasa wataendelea kusaidiwa kurejea kwao kwa hiari hadi tarehe 31 Desemba mwaka
huu, ambapo Kambi hiyo ya Mtabila itafungwa rasmi, na wale ambao watakuwa
hawajaondoka baada ya tarehe hiyo watachukuliwa kuwa ni wahamiaji haramu, na
kushughulikiwa kufuatana na Sheria ya Uhamiaji.
Historia ya hifadhi ya
wakimbizi hapa nchini ilianza tangu mwaka 1961 ambapo Tanzania ilikuwa na idadi kubwa ya wakimbizi
kutoka nchi mbalimbali za Afrika, idadi ambayo katika miaka ya tisini ilifikia
takribani milioni moja, 641,386 kati yao wakiwa
ni wakimbizi kutoka Burundi .
Zoezi la kuwarejesha
kwao wakimbizi wa Burundi
lilianza rasmi mwaka 2002 baada ya nchi yao
kurejea katika hali ya amani na hadi sasa kambi nane zilizokuwa zikihifadhi
wakimbizi toka Burundi
zimefungwa. Kambi hizo ni Karago, Mtendeli, Kanembwa na Nduta zilizokuwa
wilayani Kibondo, na Muyovosi iliyokuwa wilayani Kasulu, mkoani Kigoma.
Kambi nyingine
zilizofungwa ni Kitali iliyokuwa wilayani Biharamulo, Lukole A na B zilizokuwa
wilayani Ngara, mkoani Kigoma.Kambi ya wakimbizi ya Mtabila ndiyo itakuwa ya
mwisho kufungwa katika mlolongo wa kambi zilizokuwa zikihifadhi wakimbizi
kutoka Burundi
hapa nchini.
Imetolewa na Isaac J.
Nantanga:
MSEMAJI WA WIZARA YA
MAMBO YA NDANI YA NCHI
No comments:
Post a Comment