Release No. 131
Agosti 3, 2012
LIGI DARAJA LA KWANZA SASA TIMU 24
Ligi Daraja la Kwanza
(FDL) kuanzia msimu huu wa 2012/2013 itakuwa na timu 24 kutokana na mabadiliko
ya mfumo wa mashindano yaliyofanywa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Kamati ya Utendaji ya
TFF ilikutana Julai 29 mwaka huu ambapo pamoja na mambo mengine ilifanya
mabadiliko ya mfumo wa mashindano ikiwemo FDL kuchezwa kwa mtindo wa nyumbani
na ugenini badala ya ule wa awali wa vituo.
Kutokana na mabadiliko
hayo, timu za FDL zitagawanywa katika makundi mawili ya timu 12 kila moja
kutokana na ukaribu wa kanda na kucheza kwa mtindo wa nyumbani na ugenini
Ti.mu ya kwanza kutoka
kila kundi itapanda kucheza Ligi Kuu msimu unaofuata wakati ya tatu
itakayoungana na hizo mbili itapatikana kwa mechi za nyumbani na ugenini kwa
timu zilizoshika nafasi ya pili katika kila kundi.
Sasa timu 24 za FDL ni
Ashanti United (Dar es Salaam), Burkina Moro (Morogoro), Green Warriors (Dar es
Salaam), Kanembwa JKT (Kigoma), Kurugenzi Mafinga (Iringa), Majimaji (Ruvuma),
Mbeya City (Mbeya), Mkamba Rangers (Morogoro), Mlale JKT (Ruvuma) na Morani
(Manyara).
Nyingine ni Moro United
(Dar es Salaam), Mwadui (Shinyanga), Ndanda (Mtwara), Pamba (Mwanza), Polisi
(Arusha), Polisi (Dodoma), Polisi (Iringa), Polisi (Mara), Polisi (Tabora),
Rhino Rangers (Tabora), Small Kids (Rukwa), Tessema (Dar es Salaam), Transit
Camp (Dar es Salaam), Villa Squad (Dar es Salaam)
Timu nne zitashuka
daraja kurudi Ligi ya Mkoa. Timu hizo ni mbili zilizoshika nafasi za mwisho kwa
kila kundi. Timu nne zitakazopanda kucheza FDL zitapatikana kwa mchujo
utakaohusisha mabingwa wa mikoa.
Kwa mfumo huo mpya wa
mashindano, ligi za mikoa zitakazosimamiwa na kuendeshwa na vyama vya mpira wa
miguu vya mikoa zinatakiwa kuwa na timu zisizopungua 16 na zisizozidi 20. Ligi
za mikoa pia zitachezwa mwaka mzima kwa mikondo miwili (nyumbani na ugenini).
Ligi ya mkoa itashusha
timu mbili na kupandisha nyingine mbili kutoka ligi ya wilaya. Ligi za wilaya
zitakazosimamiwa na kuendeshwa na vyama vya mpira wa miguu vya wilaya
zinatakiwa kuwa na timu zisizopungua 10 na zisizozidi 20.
Kwa wilaya zenye timu
zaidi ya 20, chama husika cha mpira wa miguu kitapanga utaratibu wa kuzichuja
kwa mashindano ili kupata zile bora 20 zitakazocheza ligi rasmi ya wilaya.
Mabingwa wa wilaya
katika mkoa husika watacheza mechi za kuchujana (play offs) ili kupata timu
mbili zitakazopanda daraja kucheza ligi ya mkoa husika.
Kutokana na mabadiliko
hayo ya mfumo wa mashindano, sasa madaraja rasmi ya ligi ni Ligi Kuu, Ligi
Daraja la Kwanza , Ligi ya Mkoa (Ligi Daraja la
Tatu) na Ligi ya Wilaya (Ligi Daraja la Nne).
TFF inasisitiza kuwa kwa
mujibu wa kalenda yake ya matukio, kipindi cha usajili wa wachezaji kwa
madaraja yote ni kimoja, na ligi zitachezwa kwa wakati mmoja.
Usajili wa hatua ya
kwanza ni kuanzia Juni 15 hadi Agosti 10 mwaka huu wakati kipindi cha pili cha
usajili ni Agosti 21 hadi Septemba 4 mwaka huu. Usajili wa dirisha dogo ni
Novemba 15 hadi Desemba 15 mwaka huu.
Ligi kwa madaraja yote
zitaanza Septemba. Ligi Kuu itaanza Septemba Mosi mwaka huu, Ligi Daraja la Kwanza ni Septemba 15 mwaka huu, Ligi ya Mkoa na ile ya
Wilaya zenyewe zitaanza Septemba 8 mwaka huu.
Mechi za kufungua msimu
kwa madaraja yote (Ngao ya Jamii) ambazo kwa sasa zinakutanisha bingwa na makamu
bingwa zitachezwa Agosti 25 mwaka huu wakati michuano ya Kombe la FA itaanzia
wilayani Septemba 24 mwaka huu.
BINGWA MICHUANO YA
BANCABC SUPER 8 KUPATA MIL 40/-
Bingwa wa michuano ya
BancABC Super 8 inayoanza keshokutwa (Agosti 5 mwaka huu) katika miji ya Dar es
Salaam, Zanzibar, Mwanza na Arusha atapata sh. milioni 40 wakati makamu bingwa
sh. milioni 20. Pia timu mbili zitakazoishia hatua ya nusu fainali kila moja
itapata sh. milioni 15 wakati zilizobaki kila moja itapata sh. milioni 5.
Timu zimepangwa katika
makundi mawili ya A na B. Kundi A lina timu za Simba (mabingwa wa Tanzania
Bara), Jamhuri, Zimamoto na Mtende zote za Zanzibar . Kundi ni Super Falcon (mabingwa wa Zanzibar ), Azam, Mtibwa
Sugar na Polisi Morogoro zote za Tanzania Bara.
Mechi za ufunguzi
keshokutwa (Agosti 5 mwaka huu) ni Simba vs Jamhuri (Dar es
Salaam ), Zimamoto vs Mtende (Mwanza), Mtibwa Sugar vs Polisi
Morogoro (Arusha) na Super Falcon vs Azam (Zanzibar ). Awali mashindano yalikuwa yaanze
Agosti 4 mwaka huu lakini yamesogezwa mbele kwa siku moja.
Hatua ya makundi
itamalizika Agosti 12 mwaka huu. Mechi za nusu fainali na fainali zote
zitachezwa Dar es Salaam .
Nimeambatanisha ratiba.
Mdhamini bancABC
atagharamia usafiri wa ndege kwa timu zote kutoka kituo kimoja hadi kingine,
malazi na jezi. Yanga imejitokea kwenye mashindano hayo na nafasi yake
imechukuliwa na Mtibwa Sugar ambayo ilishika nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu ya
Vodacom.
KOZI YA UONGOZI YA FIFA
KUANZA AGOSTI 6
Kozi ya Uongozi na
Utawala ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) itafanyika Msimbazi Center
jijini Dar es Salaam
kuanzia Agosti 6-11 mwaka huu ikiwa na washiriki 30.
Washiriki wa kozi hiyo
itakayonedeshwa na wakufunzi kutoka FIFA ni viongozi kutoka TFF, Chama cha
Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), vyama vya mpira wa miguu vya mikoa, klabu za
Ligi Kuu na viongozi wa mpira wa miguu wa wanawake.
Walioteuliwa kushiriki
ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa TFF, Athuman Nyamlani, Rais wa ZFA Amani
Makungu, wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF; Ahmed Mgoyi, Blassy Kiondo,
Stanley Lugenge, Khalid Abdallah, Hussein Mwamba na Eliud Mvella.
Wengine ni Katibu Mkuu
wa ZFA, Kassim Salum, Katibu Msaidizi wa ZFA, Masoud Attai, wenyeviti wa vyama
vya mpira wa miguu vya mikoa ya Kagera (Jamal Malinzi), Dodoma (Nassoro
Kipenzi) na Pascal Kihanga (Morogoro).
Makatibu wa vyama vya
mpira wa miguu vya mikoa ya Mara (Mugisha Galibona), Mtwara (Vincent Majiri),
Morogoro (Hamisi Semka), Kagera (Salum Chama), Tanga (Beatrice Mgaya) na Dodoma
(Stuart Masima). Pia yumo Mwenyekiti wa Coastal Union ,
Ahmed Hilal na Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga.
Washiriki wengine ni
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, Mkurugenzi wa Ufundi, Sunday Kayuni, Ofisa
Habari, Boniface Wambura, Mkurugenzi wa Masoko na Matukio, Jimmy Kabwe,
Mkurugenzi wa Mashindano, Saad Kawemba, Ofisa Sheria wa TFF, Neema Lucumay,
Ofisa wa Mpira wa Miguu wa Wanawake, Grace Buretha, Amina Karuma (Mpira wa
miguu wa wanawake) na nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Shadrack Nsajigwa.
STARS KUIKABILI BOTSWANA AGOSTI
15
Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Agosti 15 mwaka huu
itapambana na Botswana
(Zebras) katika mchezo maalumu wa Kalenda ya FIFA utakaofanyika jijini Gaborone .
Tayari Kocha Kim Poulsen
alishatangaza kikosi cha wachezaji 21 kitakachoingia kambini Agosti 8 mwaka huu
tayari kwa mechi hiyo ya kirafiki ya kujipima nguvu.
Boniface Wambura: Ofisa
Habari
Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment