Thursday, September 13, 2012
SIJARIDHIKA NA MAJIBU YA TANESCO KUHUSU UCHAFUZI WA MAZINGIRA, FIDIA YA WANANCHI WANAOISHI MAENEO HATARISHI YA KARIBU NA MITAMBO YA KUFUA UMEME UBUNGO IHARAKISHWE
Tarehe
9 Septemba 2012 baadhi ya vyombo vya habari viliandika habari kwamba wakazi
zaidi ya 500 wa eneo la Ubungo Darajani karibu na Riverside wanalalamika kuishi
kwenye mfereji wa maji taka wenye mafuta ya mitambo na mchanganyiko wa kemikali
kadhaa zinazodaiwa kuzalishwa na Shirika la Umeme nchini (TANESCO).
Sijaridhika
na majibu yaliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Felichism
Mramba kwamba shirika hilo limedhibiti mfumo wa maji taka na haihusiki na
tatizo hilo la kuchafua makazi na mazingira.
Kufuatia
kauli hiyo, natoa wito kwa Wizara ya Nishati na Madini na TANESCO kutoa majibu
ya wazi kwa wananchi ni kampuni gani hasa inahusika na uchafuzi huo wa
mazingira na kuchukua hatua zinazostahili kurekebisha mfumo uliopo.
Ikiwa
hatua hazitachukuliwa nitaungana na wananchi kufikisha malalamiko yao kwenye
mamlaka zinazohusika na usimamizi wa mazingira katika Manispaa ya Kinondoni na
katika Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Waziri
wa Nishati na Madini na Kaimu Mkurugenzi wa TANESCO watoe majibu ya wazi kwa
wananchi ni lini fidia ya wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi
yanayozunguka mitambo ya kuzalishia umeme ya Ubungo itaanza kulipwa katika
mwaka wa fedha 2012/2013 kutokana na kiasi cha shilingi bilioni 10 ambacho
tayari kimeshaingizwa kwenye bajeti.
Izingatiwe
kwamba tarehe 04 Aprili 2012 nilifanya
mkutano na wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama wamachinga zaidi ya 500
katika kata ya Ubungo ambapo pamoja na mambo mengine nilitoa siku tatu kwa
Wizara ya Nishati na Madini na TANESCO kueleza hatua walizochukua katika
kutekeleza ahadi waliyoniahidi kwa
nyakati mbalimbali kwenye mwaka wa fedha 2011/2012 wakati wa vikao vya kamati
ya nishati na madini nilipohoji kuhusu hatma ya wananchi wanaoishi katika
maeneo hatarishi jirani na mitambo ya umeme ikiwemo kuhusu uchafuzi wa
mazingira unaoendelea.
Ikumbukwe
kwamba mwaka 2004 baada ya mitambo kulipuka serikali iliahidi kuwalipa fidia
wananchi husika na kuwahamisha, mwaka 2009 Serikali ikarudia tena ahadi hiyo
lakini mpaka tarehe 4 Aprili 2012 ilikuwa haijatekelezwa hata kwa mtu mmoja.
Ndani
ya siku hizo tatu, TANESCO ilitoa ahadi ya kuwa suala la fidia kwa wananchi
litaingizwa katika bajeti ya serikali mapema iwezekanavyo na tayari kiasi cha
shilingi bilioni 10 kimetengwa kwa ajili ya kuanza kulipa fidia ikiwa ni sehemu
ya Mradi wa Kuboresha Mifumo ya Umeme
Katika Jiji la Dar es salaam (Kasma 3154).
Ili
kuhakikisha kwamba mpango wa kulipa fidia ikiwa ni sehemu pia ya kuboresha
mazingira ya eneo husika tarehe 27 Julai 2012 katika hotuba yangu bungeni kwa
niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani niliitaka Wizara ya Nishati na Madini ieleze
iwapo kiasi cha 10,000,000,000 kilichotengwa kwa ajili ya kulipa fidia wananchi
wanaoishi katika maeneo hatarishi yanayozunguka mitambo ya kuzalishia umeme ya
Ubungo kitatosha kukamilisha kazi hiyo kwa mwaka wa fedha 2012/2013 ili
kuepusha uwezekano wa gharama kuongezeka kutokana na riba ya kuchelewa kufanya
malipo kama ilivyotokea kwa miaka iliyopita.
John
Mnyika (Mb)
09 Septemba 2012
No comments:
Post a Comment