Sunday, April 7, 2013

Hitma ya kumbukumbu ya Kifo cha Rais wa kwanza wa Zanzibar Mzee Abeid Karume leo.

 Rais wa Zanzibar Dk Alli Mohammed Shein akiwa na Rais Jakaya Kikwete wakati wa kusoma dua ya kumuombea Mzee Karume makao makuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar leo.

Dk Shein akiweka shada la maua katika kaburi la mwasisi wa Zanzibar huru Mzee Abeid Amani Karume aliyeuwawa kwa risasi mahala hapohapo makao makuu ya iliyokuwa ASP Kisiwandui mwaka 1972.


Na Khadija Khamis –Maelezo Zanzibar     
 Mamia ya Wananchi kutoka sehemu mbalimbali leo wamehudhuria katika kisomo maalum cha kumuombea dua Muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Aman Karume kilichofanyika Makao Makuu ya CCM Kisiwandui Mjini Zanzibar.
 Katika kisomo hicho ambacho mgeni Rasmi alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohammed shein kilihudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali, Vyama vya Siasa na Mabalozi.
 Awali kisomo hicho kilitanguliwa na Dua maalum iliyoongozwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar Shekh Saleh Omar Kaab.
 Mara baada ya Dua hiyo kilifuata kisomo cha Khitma kilichojumuisha Wanaume na Wanawake waliohudhuria katika hafla hiyo.
 Akitoa Mawaidha katika Hafla hiyo Shekh wa Mkoa wa Dar es Salaam Al-had Mussa Salim aliwanasihi Waumini kufanya matendo mema kwa kuzingatia kuwa Kifo kinaweza kumtokea mtu yeyote na muda wowote.
 Naye Mtoto wa Muasisi huyo Balozi Ali Karume amesema njia pekee ya kumuenzi Marehemu Karume ni kuyaendeleza yale yote mazuri aliyoyaacha.
 Katika hatua nyingine Vingozi wa mbali mbali Akiwemo Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohammed Shein, Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. Jakaya Kikwete waliweka Mshada ya Maua katika Kaburi la Marehemu Karume ikiwa ni ishara ya kumbukumbu.
 Viongozi wengine walioweka Mashada ni Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. Gharib Bilali, Makamo wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad,Makamo wa Pili Balozi Seif Ali Idd na Marais wastaafu,Wawakilishi wa Mabalozi na Viongozi mbalimbali.
 Marehemu Mzee Abeid Amani Karume alikuwa Muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 ambapo tarehe kama ya leo mwaka 1972 aliuwawa kwa kupigwa Risasi.

Picha zote kwa hisani ya Ramadhan Othman- Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment