Wednesday, April 10, 2013

Uzinduzi wa filamu mpya ya Marehemu Steven Kanumba.

 ofisa habari wa Steps Entertainment Myovelwa Mfwaisa katikati akizungumza na wanahabari katika ukumbi wa Maelezo, kushoto ni meneja mauzo wa Steps Ignatios Kambarage, kulia ni Moses Mwanyilu mratibu wa Steps.

Myovelwa akiwa na Mwanyilu wakati wakizungumza na wanahabari leo.

Kambarage akifafanua jambo wakati wa kipindi cha maswali na majibu na wanahabari leo.


wadau wa Steps wakiandaa mazingira katika chumba cha idara ya habari jijini leo kabla ya kuzungumza.


Kampuni ya kutengeneza filamu Tanzania Steps Entertainment ltd, imetangaza kuzindua filamu ya nguli wa Bongo Movie Tanzania Marehemu Steven Kanumba siku ya Ijumaa Aprili 12.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa idara ya habari Maelezo jijini leo ofisa habari wa Steps Myovela Mfwaisa, amesema filamu ya Love & Power ni filamu ya mwisho kutengenezwa na marehemu Kanumba na itawafikia watanzania kuanzia ijumaa wiki hii.

“Hii ni fursa pekee kwa watanzania kuona kazi bora iliyotengenezwa na gwiji wa filamu na balozi aliyeitangaza Tanzania kimataifa Steven Kanumba. Hii ni kazi ya mwisho kuifanya kabla ya kuaga dunia.

“Kanumba wakati anaaga dunia filamu hii ilishamalizika lakini ilikuwa bado haijahaririwa, hivyo mpenzi wa filamu Tanzania una nafasi nzuri ya kumuona Kanumba mara ya mwisho akiwakilisha,” alisema Myovela.

Hata hivyo kidojembe ilipotaka ufafanuzi kwa Myovela kuwa kuna filamu ya Ndoa Yangu, ambayo pia ilitangazwa ni ya mwisho kwa marehemu Kanumba alisema.

“Ni kweli hata sisi tulisikia hizo habari, lakini lazima ujue kitu kimoja Kanumba alikuwa akifanya kazi na makampuni mengi, hivyo inawezekana kila kampuni ina filamu yake ya mwisho aliyotengeneza na marehemu hivyo kwa sisi Steps hii Love & Power ndiyo filamu yetu ya mwisho kufanya na Kanumba,” Myovelwa.

Aidha wasanii wengine watakaoonekana katika filamu hiyo ni marhemu Hussein Mkiety ‘Sharo Milionea’, Patcho Mwamba, Irene Paul, Grace Mapunda, Hartman, Rammy Galis pamoja na mdogo wake Kanumba yaani Seth Bosco ambaye ndie alieonana na marehemu kwa mara ya mwisho yeye na Lulu.

Filamu hiyo imetengenewa na Steps Entertainment na mwandishi wa stori ni Ally Yakuti. Kwa kuzingatia rika lote katika mambo ya filamu Steps wamesema filamu hiyo itaangaliwa na watoto kuanzia rika la miaka 16.

Kwa mujibu wa wasambazaji wa filamu hiyo familia ya Kanumba imeamua kuchukua kiasi cha mauzo ya filamu hiyo ili kusaidia watoto yatima wanaoishi katika mazingira magumu.

HAFIDH KIDO
DAR ES SALAAM, TANZANIA
10 April, 2013 

No comments:

Post a Comment