Tuesday, September 4, 2012

Misa nao wajibabadua kutoa tamko...


TAARIFA KWA UMMA/VYOMBO VYA HABARI 
KUHUSU KUUAWA KWA MWANDISHI WA HABARI WA CHANNEL TEN NA MWENYEKITI WA KLABU YA WAANDISHI WA HABARI MKOA WA IRINGA (IPC) DAUDI MWANGOSI
Tasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Nchi za Kusini mwa Afrika (MISA Tan) imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha mwandishi na kiongozi mahiri wa waandishi hapa nchini. 
Aidha tunaungana na waandishi na wafanyakazi katika tasnia ya habari nchini, Jumuiya ya Klabu za Waandishi nchini (UTPC) pamoja na familia ya marehemu Mwangosi katika kipindi hiki kigumu ambacho tasnia yetu ya habari imelazimika kuingia matatani kutokana na matumizi ya mabavu ya Jeshi la Polisi.
Tunalaani kwa nguvu zote matumizi ya mabavu ya polisi ambayo yamesababisha kifo cha mwandishi wa habari akiwa kazini na pia akiwa chini ya ulinzi wa Polisi. Tunatambua uhasama kati ya Polisi wa mkoa wa Iringa dhidi ya waandishi wa habari uliodumu kwa muda mrefu.
Uhasama huu kiini chake ni kutokana na matumizi ya nguvu kupita kiasi yanayotekelezwa mkoani Iringa na hivyo kila mara waandishi wanaporipoti habari wanaingia katika mlolongo wa uhasama na vituko vya mara kwa mara. Hatimaye polisi kwa makusudi wameamua kuua mwandishi. Hili ni doa ambalo litaichukua Tanzania kujisafisha machoni pa jumuiya ya kimataifa.
Huu ni mwendelezo wa matumizi ya nguvu kupita kiasi yanayofanywa na polisi kwa raia wa nchi hii. Ni lini polisi watasimamia ulinzi wa raia na mali zao badala ya kugeuka kuwa jeshi la mauaji kila wananchi wanapokusanyika kwa minajili ya kutimiza ndoto zao?
Kifo cha Mwangosi kimegubikwa na sintofahamu hasa ukijua kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa Bwana Michael Kamuhanda alikuwa anamtambua kama kiongozi wa waandishi wa habari mkoa na alikuwepo kwenye tukio wakati Mwangosi akiwa mikononi mwa polisi, na kuuliwa mbele yake.
Lakini ikumbukwe kuwa siku zote hata katika vita waandishi wanafanya kazi bega kwa bega na askari ili kuwajuza wananchi nini kinachotokea kwenye uwanja wa mapambano. Kwa jeshi la polisi hapa nchini limedhihirisha kuwa baada visa na mikasa kuwatokea raia wa kawaida sasa wamewageukia waandishi wa habari na kukatisha maisha yao kikatili.
Sasa Polisi wamevunja daraja lililokuwa linawanganisha wananchi na serikali yao. Hii itazidisha chuki ya wananchi dhidi ya serikali yao kuliko kipindi kinginecho chote.
Ikumbukwe pia kuwa wakati mauaji haya yanatokea kuna mkutano mkuu wa UTPC unaoanza wiki hii huku wawakilishi wa vyama vya waandishi wa mbalimbali wa kimataifa wakitegemea kushiriki katika mkutano huo wa mwaka. Na hii itatoa taswira halisi ya jinsi Jeshi la Polisi linavyofanya kazi hapa nchini.
Jumuiya ya kimataifa itaweza kujionea hali halisi jinsi waandishi wa habari hapa nchini wanavyofanya kazi katika mazingira hatarishi na kwamba sasa Tanzania inawezekana isiwe mahali salama pa kuishi kama walivyokuwa wakisikia kwenye vyombo vya habari vya kwao. Mfano halisi ni mhanga Daudi Mwangosi ambaye ataingia katika vitabu vya kumbukumbu duniani kwa mwaka 2012.
Tunaiomba serikali ichukue maamuzi makini ya kukaa pamoja na vyama vya siasa ili kutafuta njia muafaka ya kutuliza mikusanyiko ya wananchi kwa njia za amani na sio kutumia mabavu katika kuwatawanya.
Ni imani yetu kuwa historia imeonyesha kuwa nguvu kupita kiasi kwa wananchi inaongeza chuki dhidi ya serikali yao ya wakati huo na kamwe hainyamazishi dukuduku zilizoko mioyoni mwa wananchi. Kokote kule duniani matumizi ya polisi yalipovuka mipaka yakaamsha hasira za wananchi na kuzifanya nchi hizo zisikalike.
Matumizi ya mabavu, nguvu kupita kiasi kuzima vuguvugu za wananchi kwa kile wanachokiamini pamoja na mauaji na hasa kwa wanahabari na raia wasio na silaha hayajawahi kufanikiwa kokote kule duniani. 
Tunaamini kuwa serikali yetu ni sikivu na itachukua hatua stahiki. Pamoja na kwamba uchunguzi huru sio utamaduni wa serikali yetu lakini katika hili la mwandishi akiwa na kalamu na kamera yake afie mikononi mwa polisi tunahitaji uchunguzi huru na wa kina.
Taasisi yetu imetoa ubani wa shilingi laki tano (500,000/-) kwa familia ya marehemu Mwangosi. Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi. Amen!

Tumaini Mwailenge

Mkurugenzi, 
MISA Tanzania


No comments:

Post a Comment