Saturday, April 13, 2013

Taarifa mbalimbali kutoka shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF)


UJUMBE WA FIFA KUWASILI APRILI 15
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linapenda kuwatangazia wadau wa mpira wa miguu kuwa ujumbe wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) utawasili nchini Jumatatu (Aprili 15 mwaka huu) kwa ajili ya kushughulikia mchakato wa uchaguzi mkuu wa TFF.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka FIFA, ujumbe huo utaongozwa na Mkuu wa Idara ya Uanachama ya FIFA, Primo Covarro na utafanya kazi kwa siku tatu kuanzia siku ya ujio na kuondoka Aprili 18 mwaka huu.

Ukiwa nchini, ujumbe huo utakutana na wagombea uongozi walioathiriwa na uamuzi wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF ambao waliomba mashauri yao yaangaliwe upya, wagombea ambao walikata rufani FIFA, Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Kamati ya Rufani na Sekretarieti ya TFF.

Wajumbe hao wangependa kukutana na waziri anayehusika na michezo, hivyo TFF imeiandikia Wizara ikipendekeza kuwa ujumbe huo ukutane na Waziri na wakuu wengine wa michezo Aprili 16 mwaka huu 2013 kabla ya kuanza kazi zao.

Wagombea watakaosikilizwa na ujumbe huo wa FIFA ni:
1.   Farid Salim Mbaraka Nahdi: Mgombea wa nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ambaye alienguliwa na Kamati ya Uchaguzi na baadaye rufani yake kwa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF kutupwa na hali kadhalika ombi lake la kutaka shauri lake liangaliwe upya, kukataliwa.

2.   Elliud Peter Mvella: Mgombea wa nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ambaye alikatwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF na kukata rufani Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF kabla ya maombi yake ya kutaka shauri lake kuangaliwa upya, kukataliwa.


3.   Mbasha Matutu: Mgombea wa nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ambaye alikatwa na Kamati ya Uchaguzi na kukata rufani ambayo pia ilitupwa kabla ya kuomba shauri lake liangaliwe upya, ombi ambalo lilikataliwa.

4.   Hamad Yahya: Mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa Bodi ya Ligi ambaye alipitishwa na Kamati ya Uchaguzi, lakini mwekaji pingamizi akakata rufani ambayo ilikubaliwa na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF na kuondolewa. Aliomba shauri lake liangaliwe upya, lakini Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF ikatupa ombi lake.

5.   Jamal Emily Malinzi: Mgombea wa nafasi ya urais wa TFF ambaye alipitishwa na Kamati ya Uchaguzi, lakini mwekaji pingamizi akakata rufani ambayo ilikubaliwa na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF, hivyo kuondolewa kwenye mchakato. Aliomba shauri lake liangaliwe upya, lakini likakataliwa. Hata hivyo, alikuwa ameshakata rufani FIFA.

6.   Michael Wambura: Mgombea wa nafasi ya Makamu wa Rais wa TFF ambaye alikatwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF na rufani yake kukataliwa na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF. Hakuomba shauri lake liangaliwe upya, lakini alikata rufani FIFA.

Shirikisho linawaomba wote waliotajwa hapo juu kujiandaa kwa utetezi na maelezo ya kutosha na kwamba barua za kuwaita zinafuata. (Orodha ya waathiriwa na programu ya ujumbe wa FIFA imeambatanishwa)

YANGA, OLJORO KUUMANA MECHI ZA VPL
Ligi Kuu ya Vodacom inaendelea kesho (Aprili 13 mwaka huu) kwa mechi mbili zitakazochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, na Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Yanga itakuwa mwenyeji wa Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Taifa wakati Uwanja wa Sokoine utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Tanzania Prisons na Ruvu Shooting.

Ligi hiyo itaendelea keshokutwa (Aprili 14 mwaka huu) kwa mechi kati ya wenyeji Azam na Simba. Mechi hiyo namba 155 itachezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

WASHELISHELI KUICHEZESHA AZAM CAF
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua waamuzi kutoka Shelisheli kuchezesha mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho kati ya Azam na AS FAR ya Morocco itakayofanyika Aprili 20 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Waamuzi hao ni Emile Fred atakayepuliza filimbi akisaidiwa na Steve Maire na Jean Ernesta. Mwamuzi wa mezani (fourth official) atakuwa Jean Claude Labrossa. Kamishna wa mechi hiyo ni Abbas Sendyowa kutoka Uganda.

Wakati huo huo, CAF imemteua Mtanzania Alfred Lwiza kuwa Kamishna wa mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho kati ya Liga Muculmana ya Msumbiji na Wydad Casablanca ya Morocco.

Mechi hiyo itakayochezwa kati ya Aprili 19,20 au 21 mwaka huu nchini Msumbiji itachezeshwa na waamuzi kutoka Zimbabwe wakiongozwa na Ruzive Ruzive.


Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
  Aprili 12, 2013

No comments:

Post a Comment